Dola milioni 710 zahitajika kusaidia wasomali milioni 4.5 wanaokabiliwa na ukame-OCHA

21 Mei 2019

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yamezindua ombi la kukabiliana na ukame la dola milioni 710 kwa ajili ya msaada wa dharura kwa ajili ya kuwasaidia watu milioni 4.5 wanaothriwa na ukame nchini Somalia kwa ajili ya kipindi kuanzia sasa hadi mwezi Disemba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, miaka mbili tangu kushuhudiwa kwa ukame wa muda mrefu mwaka 2016/2017 ambapo mbinu za kujipatia kipato ziliharibiwa na watu takriban milioni moja kufurushwa.

OCHA imesema licha ya kwamba ukame huo ulisababisha kuongezeka kwa msaada wa kibinadamu kwa ajili ya kukabiliana na njaa, mabadiliko ya tabianchi ikijumuishwa na vichochezi vingine ikiwemo mzozo wa kujihami, ufurushwaji na ongezeko la kufurushwa kwa wakimbizi wa ndani vinasukuma Somalia katika hali ya dharura ya kibinadamu, huku  maeneno ya kaskazini na kati kati mwa Somali yakiathirika zaidi.

Taarifa ya OCHA imeonya kuwa idadi y watu walioko kwenye mzozo huenda ikapanda zaidi na kufika milioni 2.2 kufikia Julai iwapo, misaada haitaimarishwa. Hii ni zaidi ya asilimia 40 mwezi Januari mwaka huu. Utapiamlo, magonjwa yatokanayo na ukame, ufurushwaji vyote vimeongezeka. Aidha visa vya unyafuzi miongoni mwa watoto vinaongezeka kwa kazi hususan miongoni mwa wakimbizi wa ndani.

Somalia ipo katika wakati muhimu

Kaimu naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, George Conway amesema kwamba, “hali ya ukame nchini Somalia imezorota kwa kasi kubwa na kuongezeka kuliko ilivyoshuhudiwa katika muongo uliyopita. Somalia iko katika wakati muhimu na iwapo kuna raslimali za kutosha, tunaweza kujenga upya mifumo iliyozuia nja mwaka 2017.”

Bwana Conway ameongeza kwamba, “wakati tukiendelea kufanya kazi chini ya uongozi wa mamlaka Somalia na kuwajengea mnepo na kutatu sababu ambazo zinasababisha majanga ya mara kwa mara na ni muhimu kwamba kila mtu ikiwmeo, wasomali walioko ndani nan je mwa nchi, wafadhili na sekta binafsi wakaungana katika juhudi za kukabiliana na kuzuia.”

Licha ya mahitaji yaliyopo lakini upungufu wa raslimali ni ndio changamoto kubwa kwani ni asilimia 20 tu ya ombi la msaada wa kibinadamu kwa mwaka 2019 la bilioni 1.08 ndio imefadhiliwa.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter