Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milini 70 zahitajika kuwasaidia waathirika wa kimbuga Freddy Malawi: UN

Kimbunga Freddy kimesababisha uharibifu mkubwa wa barabara na miundombinu nchini Malawi.
© UNICEF Malawi
Kimbunga Freddy kimesababisha uharibifu mkubwa wa barabara na miundombinu nchini Malawi.

Dola milini 70 zahitajika kuwasaidia waathirika wa kimbuga Freddy Malawi: UN

Msaada wa Kibinadamu

Mwishoni mwa wiki Umoja wa Mataifa na washirika wake wa misaada ya kibinadamu wametoa ombi la dola milioni 70 ili kuwasaidia watu zaidi ya milioni moja nchini Malawi walioathirika na kimbunga Freddy kilichoikumba nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika mwezi uliopita.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini New York Marekani hii leo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema “ombi hili jipya limekuja kama ziada ya ombi lililotolewa mapema mwaka huu la dola milioni 45 ili kupambana na mlipuko wa kipindupindu na hivyo kufanya ombi la msaada kuwa jumla yad ola milioni 116.”

Fedha za ombi hilo zinalenga kusaidia hatua zinazoongozwa na serikali za kupambana na athari za mafuriko na ugonjwa wa kipindupindu kwa kutoa msaada wa malazi, lishe, huduma za afya, maji, usafi na huduma za kujisafi yaani WASH.

Tangu kimbunga Freddy kilipopiga Stephane amesema “Sisi pamoja na washirika wetu tumewafikia Zaidi ya watu 370,000 kwa msaada wa kibinadamu ikiwemo wa maji safi, usafi wa mazingira na huduma za kujisafi, Pamoja na msaada wa chakula ili kuunga mkono juhudi za serikali za msaada.”