Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la Idhaa za Kiswahili: Kiswahili kinaweza kutumika kupigania haki za mwanamke

Mjadala ukiendelea wakati wa  kongamano la Idhaa za Kiswahili lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Zanzibar, Tanzania.
UN/Anold Kayanda
Mjadala ukiendelea wakati wa kongamano la Idhaa za Kiswahili lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Zanzibar, Tanzania.

Kongamano la Idhaa za Kiswahili: Kiswahili kinaweza kutumika kupigania haki za mwanamke

Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo ni siku ya kwanza ya Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani linalofanyika visiwani Zanzibar nchini Tanzania, wadau wa matumizi ya lugha ya Kiswahili hususani katika vyombo vya habari vya kimataifa wameanza kutoa maoni yao kuhusu mada mbalimbali nyingi zikiwa ni kuhusu lugha yenyewe ya Kiswahili na wanahabari.

Ni siku ambayo imeanza kwa shamrashamra ya ngoma ya kitamaduni ya wakazi wa Zanzibar ambapo wanenguaji na waimbaji wamezikonga nyoyo za wahudhuriaji.

Kisha Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, mgeni rasmi wa Kongamano hili akawa na wito kwa washiriki wa kongamano hili la Idhaa za Kiswahili Duniani, “wito wangu kwa washiriki wa kongamano hili, mtumie vema taaluma mtakayoipata na bila ya shaka mtajifunza mambo mengi yanayohusu Kiswahili, Utangazaji na uandishi wa habari. Ninaamini kwamba wataalamu walioandaliwa watatoa taaluma muhimu ya matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili itakayokuongezeeni umahiri na kukujengeeni uwezo zaidi”.

Edith Nibhakwe Mwanahabari kutoka nchini Rwanda, Mtangazaji wa kipindi cha Televisheni cha Longa Nami kupitia Isango TV ni mmoja wa waliohudhuria Kongamano hili la siku mbili. Yeye ameenda mbali zaidi ya mada zilizokuwa zinajadiliwa leo kama ‘Changamoto za Matumizi ya Kiswahili katika kazi ya Utangazaji ndani ya vituo vituo vya kazi’ akazunumzia namna lugha ya Kiswahili inavyoweza kutumika kupigania haki ya msichana na mwanamke na hususani akitolea mfano ukanda wa Afrika mashariki akianzia na ukuzaji wa uchumi anasema, “kwa mfano sisi ambao tuko Rwanda tunapakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Na biashara za kuvuka mipaka sanasana zinafanywa na wanawake, na wale wanawake wanawasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano. Ninaweza nikawa ninazungumza na lafudhi yangu ya Rwanda na mwezangu anazungumza Kiswahili lafudhi yake ya Congo, lakini tunaelewa. Nikileta bidhaa ananunua na nikileta bidhaa ananunua. Kwa hiyo pale tunajiendeleza kama wanawake. Tunaendeleza nchi zetu.”

Edith anaendelea kufafanua kuhusu namna ambavyo upana wa ufikiaji lugha fulani unavyoweza kuathiri kwa uchanya au uhasi katika kupigania haki za msichana na mwanamke anasema, “kwa mfano unapotoa lada mafunzo kuhusu haki za wanawake nikitumia Kinyarwanda, nikitumia Kirundi au Kiganda mafunzo yangu yatawafikia watu wachache lakini tukiweza kuwasiliana katika lugha pana ya Kiswahili ninaweza nikawafikia watu wengi.”

Kongamano hili lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wengine, limewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa na wadau wengine wa lugha ya Kiswahili kama vile Vyuo Vikuu.

Mwaka 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO liliitambua lugha ya Kiswahili kuwa moja ya lugha za kimataifa na takwimu zinaonesha kuwa ndio lugha ya kibantu yenye wazungumzaji wengi zaidi barani Afrika.