Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwani una nafasi kubwa katika kufanikisha SDGs- Ripoti ya UNCTAD

Wanawake nchini Tanzania wakivuna seaweed kama sehemu ya mradi wa kilimo bora cha hali ya hewa.
UN Women/Phil Kabuje
Wanawake nchini Tanzania wakivuna seaweed kama sehemu ya mradi wa kilimo bora cha hali ya hewa.

Mwani una nafasi kubwa katika kufanikisha SDGs- Ripoti ya UNCTAD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Utafiti mpya uliotolewa na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara, UNCTAD inaonesha Tanzania kuwa inaongoza barani Afrika kwa kilimo na uuzaji nje ya nchi wa zao la mwani, huku wanawake wakulima wa zao hilo nchini Kenya wakiwa mstari wa mbele kuondokana na matumizi ya Kamba za plastiki katika kilimo cha zao hilo linalozidi kupata umaarufu duniani kila uchao kutokana na faida zake za kiafya.

Utafiti huo umechapishwa mwezi huu wa Machi huko Geneva, Uswsi, makao makuu ya UNCTAD, utafiti ambao ulilenga kuchunguza nafasi ya mwani katika kuchochea ukuaji uchumi, uendelevu wa mazingira na uwezeshaji wanawake kiuchumi. Nchi zilizomulikwa katika utafiti huo ni Tanzania, Kenya na Ureno.

Tanzania ni ya 8 kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa kilimo cha mwani duniani

Ripoti inasema kuwa bara la Afrika ndio kwanza linaanza kuvumbua uwezo wake katika uzalishaji wa mwani ingawa kwamba bado zao hilo halijaingizwa kwenye orodha ya bidhaa zinazonufaika na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika, AfCFTA.

Mathalani katika Tanzania, kilichobainika ni kwamba taifa hilo la Afrika Mashariki linaongoza barani Afrika kutokana na kilimo cha aina ya mwani Eucheuma na Kappaphycus huko visiwani Zanzibar. Mwaka 2015 uzalishaji ulifikia kiwango cha juu cha tani 178,000 kabla ya kuporomoka mwaka 2021 hadi tani 81,000. Takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuwa Tanzania ni ya 8 kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa uzalishaji wa mwani duniani.

Ingawa hivyo kuyumbayumba kwa uzalishaji wa mmea huo umesababisha nafasi ya Tanzania kwenye soko la kimataifa kutokuwa imara ikilinganishwa na wazalishaji wakubwa ambao wanaongeza thamani kwenye zao la mwani.

Mwaka 1989, kwa mujibu wa utafiti huo, wavuvi huko Zanzibar walianza kilimo cha mwani ili kupanua mawanda ya kujipatia kipato. “Wakati wanaume waliendelea na uvuvi au utalii, wanawake walitawala kilimo cha mwani kwani waliona ni kilimo ambacho hakikuwa kinatiliwa maanani. Wanawake walio katika mazingira hatarishi wakiwemo wajane, waliopewa talaka, waliona kilimo cha mwani kuwa ni mkombozi.”

Bidhaa za urembo zinatengenezwa kwa kutumia mwani. Ukulima wa mwani visiwani Pemba wachangamshwa na mradi wa IFAD na GEF.
IFAD
Bidhaa za urembo zinatengenezwa kwa kutumia mwani. Ukulima wa mwani visiwani Pemba wachangamshwa na mradi wa IFAD na GEF.

Joto la maji baharini liliyumbisha uzalishaji

Takwimu hata hivyo zinaonesha kuwa katikati ya miaka 2010 uzalishaji wa mwani ulipungua kutokana na ongezeko la joto la maji ya bahari lililosababisha uzalishaji kusongeshwa mbali zaidi baharini, huku wanawake wakiwa hawana uwezo wa kuogelea.

“Kuhakikisha wanawake na wakulima wegine, vikundi vya utafiti na wadau wa sekta hiyo walianzisha mafunzo ya kuogelea kwa wanawake.”

Licha ya changamoto hizo, wanawake wameendelea kufanya kazi katika mazingira yenye changamoto ikiwemo chini ya jua kali na hata kwenye maji ya chumvi.

“Kupitia mafunzo yanayotolewa na wanawake, elimu na rasilimali kutoka kwa wadau mbali mbali ikiwemo serikali, Zanzibar imeanza kutatua changamoto hizo.”

Bidhaa zitokanazo na mwani

Utafiti unasema Zanzibar imeanza kusongesha sekta ya mwani kama fursa muhimu katika kuendeleza na kushirikisha wanawake kiuchumi.

“Hatua zaidi zinatakiwa katika kuongeza thamani, mipango na matumizi ya teknolojia za kisasa na kutengeneza bidhaa tofauti tofauti na hatimaye kuwa na bei nzuri ya bidhaa hiyo kwa wakulima Zanzibar na maeneo mengine ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”imependekeza ripoti hiyo.

Kwa sasa mwani unatumika kutengeneza sabuni, bidhaa za kutunza ngozi, vyakula na bidhaa za kujisafi. “Bidhaa hizi kwa sasa zinauzwa ndani ya jamii lakini wanawake wameonesha nia ya kupanua wigo wa soko hadi barani kote Afrika na hatimaye dunia nzima,” umesema utafiti huo.

Wakulima wanawake wa mwani Kenya na harakati za kutokomeza matumizi ya plastiki

Nchini Kenya, kilimo cha mwani kimekuwa kikipigiwa chepuo cha kuwa kilimo rafiki kwa mazingira. Hata hivyo matumizi ya Kamba za plastiki kushikilia viunzi vya shamba baharini yameanza kugeukiwa kwani yanaharibu mazingira.

“Kamba chakavu na zinazotupwa baada ya kutumika huchomwa moto au hutelekezwa kiholela. Ongezeko la joto duniani limechagiza wakulima kuhamishia mashamba yao ya mwani kwenye maeneo ya maji baridi zaidi na hivyo kusababisha uwezekano wa Kamba zao kupotea.”

Amiri Juma Amiri mkulima huyu wa mwani akiwa na mwani aliovuna kutoka shambani kwake baharini kufuatia mradi unaofadhiliwa na taasisi ya utafiti wa majini na viumbe vya  bahari ya Kenya.
UN/ Kenya
Amiri Juma Amiri mkulima huyu wa mwani akiwa na mwani aliovuna kutoka shambani kwake baharini kufuatia mradi unaofadhiliwa na taasisi ya utafiti wa majini na viumbe vya bahari ya Kenya.

Ili kuondokana na tatizo hilo, taasisi ya Catchgreen kwa ubia na Taasisi ya Kenya ya Utafiti wa viumbe vya baharini, KMFRI, Baraza la usimamizi wa fukwe la Kibuyuni, BMU, nchini Kenya na UNCTAD, wameanzisha mradi kifani wa matumizi ya Kamba ziitwazo Biodolomer® .

Kamba hizi zinaoza na zimeundwa kupunguza uchafuzi wa bahari kupitia Kamba za plastiki. Kamba hizo huoza katika kipindi cha miaka 2 bila kuacha taka zozote zile za sumu kwenye bahari.

Utafiti wa kamba zinazooza waleta nuru

Tayari wanawake wa kijiji cha Kibuyuni nchini Kenya wanatumia Kamba hizo ambapo sasa wamepanda mwani kwa kutumia Kamba hizo mpya sambamba  na zile za zamani ili kuweza kuona tofauti na ubora.

Majaribio hayo yalianza mwezi Agosti mwaka 2023 na yanaonesha ukuaji kwenye Kamba mpya ni sawa na ukuaji kwenye Kamba za plastiki.

Soma ripoti nzima hapa.