Uhifadhi wa mazingira ya baharí ni muhimu katika maeneo yote- Tanzania

17 Juni 2019

Mkutano wa 20 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa matumizi ya baharí UNCLOS ukianza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani, Umoja wa Mataifa umetaka matumizi endelevu ya baharí kuu na eneo mahsusi la kiuchumi baharini ili kuepusha madhara zaidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia wajumbe amerejelea kile alichoshuhudia kwa nchi za pasifiki ambazo baadhi ya visiwa viko hatarini kuzama kutokana na uchafuzi wa mazingira na shughuli za kibinadamu zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la kina cha baharí.

Awali akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa Mzee Ali Haji ambaye ni Naibu  Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, amesema kuwa suala la uharibifu wa mazingira na tathmini ya madhara kwenye mazingira ni jambo ambalo linatiliwa maanani.

Bwana Haji amesema suala la tathmini ya hali ya mazingira, “ni moja kati ya maeneo ambayo yamepewa kipaumbele. Tathmini ya hali ya mazingira kabla ya kufanya shughuli yoyote ile ni lazima ifanyike, na sisi kama Tanzania hilo tumelisimamia, na tunahitaji tuone kwamba suala la uharibifu wa mazingira lazima liwekewe mikakati ya kulizuia. Isiwe kwamba watu wanachafua mazingira na tunapochafua mazingira wanaoumia ni viumbe vilivyopo baharini na binadamu pia. Kwa hiyo sisi tunakubaliana na kundi la Afrika na lile la nchi zinazoendelea na China, kuhakikisha kwamba mazingira ya baharí yanalindwa hata katika hilo eneo la nje ya mipaka ya baharí.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter