Kampeni ya chanjo ya kipindupindu yaanza Msumbiji.

3 Aprili 2019

Shirika la afya duniani WHO, shirikisho la kimataifa la chama cha msalaba mwekundu na mwezi mwekundu IFRC, Madaktari wasio na mipaka MSF na shirika la Save the Children wanaisaidia serikali ya Msumbiji kupitia Wizara ya afya ya Msumbiji  wameanza leo  kusambaza chanjo ya matone ili kudhibiti kipundupindu na  kuwalinda manusura wa kimbunga Idai mjini Beira nchini Msumbiji.

Kufuatia madhila yaliyosababishwa na kimbunga Idai, takribani watu 900,000 watapata chanjo kutoka shirika la muungano wa chanjo duniani Gavi.

Tayari kuna ripoti za kifo kilichotokana na kipundupindu na takribani visa 1,500 vya maambukizi ya kipindupindu vimeripotiwa baada ya kimbunga ambacho kilisababisha mafuriko nchini Msumbiji, Zimbabwe, Malawi na Madagascar. Vituo tisa vya kutibu kipindupindu, vikiwa na vitanda 500 tayari vinawapokea na kuwalaza wagonjwa.

Mkurugenzi mtendaji wa Gavi Dkt Seth Berkley anasema, “madhila ya kimbunga Idai yameyaacha maji na miundombinu ya kujisafi ya mji wa Beira katika hali mbaya hivyo kuweka mazingira mazuri kwa ugonjwa wa kipindupindu kusambaa. Kimbunga hiki tayari kimesababisha madhila makubwa kote kusini Mashariki mwa Afrika, tunatakiwa kuwa na matumaini kuwa chanjo hizi zitasaidia kuzuia uwezekano wa mlipuko mkubwa na kuepuka mateso zaidi.”

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Adhanom Ghebreyesus, anasema, “maelfu wanaishi katika mazingira mabaya kwenye makazi ya muda bila maji salama na huduma za kujisafi, hali inayowaweka katika hatari kubwa ya kipindupindu na magonjwa mengine. Jambo la muhimu ni kuhakikisha watu wanaweza kupata maatibabu ya haraka, maji safi na huduma za kujisafi. Chanjo ya kipindupindu ni hatua muhimu ya dharura ambayo itasaidia kuokoa maisha na kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu mbaya.”

Katika mlipuko wa kipundupindu uliotokea mwezi Februrai mwaka 2018 nchini Msumbiji, watu 2000 walipatwa na ugonjwa huo.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter