Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia za kutumia silaha dhidi ya shule zimeongezeka mara tisa Haiti katika mwaka mmoja: UNICEF

Inakadiriwa kuwa watoto milioni moja hawako shuleni nchini Haiti kutokana na ukosefu wa usalama na sababu nyingine.
© UNICEF
Inakadiriwa kuwa watoto milioni moja hawako shuleni nchini Haiti kutokana na ukosefu wa usalama na sababu nyingine.

Ghasia za kutumia silaha dhidi ya shule zimeongezeka mara tisa Haiti katika mwaka mmoja: UNICEF

Utamaduni na Elimu

Vitendo vya unyanyasaji wa kutumia silaha dhidi ya shule nchini Haiti, vikiwemo vya risasi, uporaji, unyang’anyi na utekaji nyara vimeongezeka mara tisa katika kipindi cha mwaka mmoja, huku ongezeko la ukosefu wa usalama na machafuko makubwa vikianza kulemaza mfumo wa elimu nchini humo, limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika taarifa yake iliyotolewa mjini Pout-au-Prince na New York huku likiongeza kuwa watoto walipoteza wastani wa siku moja na nusu ya shule kwa wiki katika mwezi Januari mwaka huu 

Katika miezi minne ya kwanza ya mwaka wa masomo  kuanzia Oktoba - Februari, UNICEF imesema shule 72 ziliripotiwa kulengwa ikilinganishwa na shule 8 katika kipindi kama hicho mwaka jana.  

“Hii ni pamoja na takriban shule 13 zinazolengwa na makundi yenye silaha, shule moja kuchomwa moto, mwanafunzi mmoja kuuawa, na angalau wafanyakazi wawili kutekwa nyara, kulingana na ripoti za washirika wa UNICEF.  

Katika siku sita za kwanza za Februari pekee, shule 30 zilifungwa kutokana na kuongezeka kwa vurugu katika maeneo ya mijini, wakati zaidi ya shule 1 kati ya 4 imesalia kufungwa tangu Oktoba mwaka jana.” 

Badala ya shule iuwa mahali salama sasa ni mlengwa 

Kwa mujibu wa mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti Bruno Maes “Nchini Haiti, shule zimekuwa zikizingatiwa na kuheshimiwa kama mahala salama, lakini katika miezi michache iliyopita zimekuwa shabaha za ghasia. Katika baadhi ya maeneo ya miji ya nchi hiyo, makundi yenye silaha yanafikiria uporaji shule kama njia mbadala yenye faida kwa aina nyingine za unyang'anyi na uhalifu. Hili lazima likomeshwe. Kulengwa kwa shule na makundi yenye silaha kunaleta athari kubwa kwa usalama wa watoto, ustawi na uwezo wa kujifunza." 

Watoto milioni 1 hawako shuleni Haiti 

Kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, asilimia 60 ya mji wa Port-au-Prince inadhibitiwa na makundi yenye silaha.  

Vikundi vinapolenga shule, mara kwa mara hupora vifaa vya shule, ikiwa ni pamoja na madawati, makabati, mbao, kompyuta ndogo, mashine za kupiga picha, betri, na paneli za sola.  

Vingine wanabvyopora ni magunia ya mchele, unga, na mahindi yanayotumika kwa chakula cha shule  ambachi ni njia ya maisha kwa watoto wengi sana nchini Haiti, pia wameiba vifaa vya kantini. 

Shule moja huko Port-au-Prince, moja ya shule nyingi katika mji mkuu wa Haiti ambazo zimeharibiwa na ghasia.
© UNICEF
Shule moja huko Port-au-Prince, moja ya shule nyingi katika mji mkuu wa Haiti ambazo zimeharibiwa na ghasia.

Shule nyingi zimefungwa 

Wakati machafuko ya kijamii yakiongezeka wiki hizi za hivi majuzi, wakuu wengi wa shule wamechukua uamuzi wa kufunga shule ili kuwalinda watoto dhidi ya mashambulizi yanayoweza kutokea.  

Na matokeo yake mwezi Januari 2023, watoto walipoteza wastani wa siku moja na nusu ya shule kwa wiki.  

Bila hatua za dharura za kulinda shule dhidi ya ghasia, UNICEF inatabiri kuwa wanafunzi watapoteza takriban siku 36 za shule kufikia mwisho wa mwezi Juni. 

Shirika hilo la Watoto limeongeza kuwa mbali na vurugu za kutumia silaha, machafuko ya kijamii pia yameathiri uwezo wa watoto kujifunza shuleni.  

Tarehe 26 Januari, kwa mfano, watoto walilazimishwa kuhama shule huku maandamano ya vurugu mitaani kuhusu mauaji ya polisi 14 yakienea kote nchini. 

Hakuna dalili ya kurejea haraka kwa usalama 

“Watoto wanapokabiliwa na athari za unyanyasaji wa kutumia silaha, ukosefu wa usalama nchini Haiti hauonyeshi dalili ya kupungua," amesema Maes na kuongeza kuwa "Vurugu zinaendelea kuathiri sana maisha ya watoto ndani na katika viunga vya Port-au-Prince, na shule hazijalindwa tena. Mtoto ambaye anaogopa kwenda shule ni mtoto aliye katika hatari zaidi ya kuajiriwa na makundi yenye silaha. Ni lazima tuchukue hatua za haraka ili kulinda maisha na mustakabali wa watoto." 

Licha ya kuongezeka kwa ghasia na ukosefu wa usalama nchini humo, Wizara ya Elimu ya Haiti imeongeza juhudi zake za kufungua shule, huku shule 3 kati ya 4 zikifunguliwa ilipofikia Desemba 2022, ikilinganishwa na chini ya shule 1 kati ya 10 mwezi Oktoba. 

UNICEF inawataka wahusika wote kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyohatarisha haki ya watoto ya kupata elimu.  

UNICEF pia inatoa wito kwa Serikali ya Haiti kuhakikisha shule ziko salama na kuwawajibisha makundi na watu binafsi wanaodhuru au kutishia watoto shuleni.