Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde Haiti kipaumbele kiwe kuokoa maisha:UN

Hospitali nchini Haiti zinakabiliwa na upungufu wa mafuta kuweza kutoa huduma muhimu zinazohitajika za mama na mtoto
© UNICEF/Ulises Daniel Diaz Mercado
Hospitali nchini Haiti zinakabiliwa na upungufu wa mafuta kuweza kutoa huduma muhimu zinazohitajika za mama na mtoto

Chonde chonde Haiti kipaumbele kiwe kuokoa maisha:UN

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema bado ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Haiti, ambayo inakabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu huku kukiwa na kuzorota kwa hali ya usalama ambayo imeilemaza nchi hiyo. 

Katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York Marekani Antonio Guterres amesema “Uzuiaji wa kituo cha mafuta cha Varreux umesababisha huduma muhimu zinazohitajika ili kuzuia kuenea kwa haraka kwa ugonjwa huo kusimama, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa maji ya kunywa. “ 

Ameongeza kuwa kwa mara nyingine sekta za watu wa Haiti zilizo hatarini zaidi za idadi ndizo zilizoathiriwa zaidi.  

Guterres amesisitiza kuwa “Kipaumbele lazima kiwe kuokoa maisha.” 

Katibu Mkuu anaitaka jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na wajumbe wa Baraza la Usalama, “kuzingatia kwa dharura ombi la serikali ya Haiti la kutumwa mara moja kwa kikosi maalumu cha kimataifa kushughulikia mgogoro wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji kwa uhuru wa huduma za maji, mafuta, chakula na vifaa tiba kutoka kwenye bandari kuu na viwanja vya ndege kwenda kwa jamii na vituo vya huduma za afya.” 

Katibu Mkuu leo ​​amewasilisha kwa Baraza la Usalama barua yenye chaguzi za kuimarishwa kwa msaada wa usalama kwa Haiti, kama ilivyoombwa na Baraza katika azimio lake nambari 2645 (2022). 

Katibu Mkuu ametoa wito kwa wadau wa Haiti kuondokana na tofauti zao na kushiriki, bila kuchelewa zaidi, katika mazungumzo ya amani na jumuishi juu ya kusonga mbele kwa taifa hilo.  

Amesema “Umoja wa Mataifa unasimama na watu wa Haiti na utaunga mkono juhudi za kujenga maelewano, kupunguza ghasia na kukuza utulivu nchini humo.”