Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwarejesha watoto shuleni katika Haiti iliyosambaratishwa na magenge ya uhalifu

Mama akimsaidia mtoto wake kusoma katika uwanja wa ndondi wa Delmas 4 Olympique ambapo sasa wanajihifadhi.
© UNOCHA/Giles Clarke
Mama akimsaidia mtoto wake kusoma katika uwanja wa ndondi wa Delmas 4 Olympique ambapo sasa wanajihifadhi.

Kuwarejesha watoto shuleni katika Haiti iliyosambaratishwa na magenge ya uhalifu

Utamaduni na Elimu

Kutokana na hali ya janga la kibinadamu na ghasia za magenge ya uhalifu nchini Haiti, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kwamba watoto wanateseka sio tu kwa kukosa shule bali pia kwa kushuhudia vurugu na ghasia zisizo na kifani.

Wanafunzi katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince wamekosa mamia ya saa za muda wa masomo katika mwaka uliopita na sasa zaidi ya Wahaiti milioni moja wanakabiliwa na viwango vya dharura vya uhaba wa chakula, kwa mujibu wa ripoti mpya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Wakati vitisho vikubwa kwa usalama wa shule vikiendelea huko Port-au-Prince, na sehemu za kaskazini za eneo la Artibonite, UN News imechunguza hali hiyo na jinsi Umoja wa Mataifa unavyokabiliana na changamoto hiyo kubwa kwa elimu.

Kambi ya mahema ya watu ambao wamekimbia makazi yao sasa yana Gymnasium Vincent, shule na uwanja wa michezo katikati mwa jiji la Port-au-Prince.
© UNOCHA/Giles Clarke
Kambi ya mahema ya watu ambao wamekimbia makazi yao sasa yana Gymnasium Vincent, shule na uwanja wa michezo katikati mwa jiji la Port-au-Prince.

Shule nyingi zimefungwa

Kufikia mwisho wa Januari mwaka huu, jumla ya shule 900 zilikuwa zimefungwa kwa muda hasa huko Port-au-Prince, na kuwanyima karibu watoto 200,000 haki yao ya kupata elimu, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Shule nyingine nyingi zilifungwa ghafla huko Port-au-Prince mwishoni mwa mwezi wa Februari, wakati magenge ya wahalifu yenye silaha yaliporatibu uvamizi katika magereza, na kuwaachia huru wafungwa 4,500.

Magenge yanaripotiwa kuwa sasa yanadhibiti asilimia 80 hadi 90 ya mji mkuu, na katika machafuko yaliyofuata, mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliripoti visa vya makundi yenye silaha kuwasajili watoto, kuongezeka kwa vurugu, uporaji na uharibifu.

"Wakazi wa Haiti wamekumbwa na janga," amesema Catherine Russell, mkuu wa UNICEF akiongeza kuwa “Nafasi za watoto zimegeuzwa kuwa viwanja vya vita. Kila siku inayopita inaleta unyonge na mambo ya kutisha kwa watu wa Haiti.”

Usalama wa msingi unahitajika kwa dharura kwa huduma za kuokoa maisha na wafanyakazi wa misaada kuwafikia wale wanaohitaji sana msaada huo, amesema, akitoa wito wa ulinzi wa shule, hospitali na miundombinu mingine muhimu ambayo watoto wanaitegemea na kwa kulinda maeneo ya kibinadamu.

Uwanja wa michezo wa watoto umekuwa kimbilio la watu katika eneo la Tabarre la Port-au-Prince, Haiti.
© UNOCHA/Giles Clarke
Uwanja wa michezo wa watoto umekuwa kimbilio la watu katika eneo la Tabarre la Port-au-Prince, Haiti.

Madarasa yamegeuka makazi

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, ghasia zilikuwa zimewafurusha makwao takriban watu 362,000, huku wengi wao wakiwa wamekwama katika mji mkuu uliozingirwa na maelfu wakipata makazi ya muda katika majengo ya umma, zikiwemo shule.

Kila darasa liligeuka kuwa nyumba ya muda kwa familia nyingi. Viwanja vya michezo vikawa vibanda vya mahema. Majumba ya mazoezi ya mwili yalibadilishwa kuwa mabweni ya wazi kwa wale wanaotafuta usalama.

"Shule nyingi hazifikiki huku ghasia zikizidi kuzizunguka," amesema mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti, Bruno Maes.

Ameongeza kuwa "Zingine zimekaliwa na magenge, zingine na watu waliofurushwa makwao na bado nyingi zaidi zimeporwa au kuharibiwa."

Alasiri ya tarehe 25 Machi, vikundi vilivyojihami vikali viliingia katika shule ya katikati ya jiji la Port-au-Prince na kuchoma moto madarasa 23. Mashirika ya misaada yalilaani vikali tukio hilo.

Katika kisa kingine katika kitongoji cha Port-au-Prince cha La Saline, watoto 3,500 walikwama katika shule mbili huku magenge ya wahalifu yakipigana karibu nao. 

UNICEF ilishauriana na makundi hayo yenye silaha kwa siku nne kabla ya kukubali kuachiliwa kwa usalama kwa watoto hao.

UNICEF imezitaka pande zote kuwalinda wanafunzi, walimu, wazazi na miundombinu ya elimu kwa kuzingatia Azimio la Shule Salama, ahadi ya kisiasa ya kimataifa iliyoidhinishwa na nchi 119, ikiwa ni pamoja na Haiti, kwa hatua bora za ulinzi na msaada kwa ajili ya kuendelea na elimu wakati wa migogoro ya silaha.

Bruno Maes (katikati), mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti, akitembelea shule moja huko Artibonite.
© UNICEF/Herold Joseph
Bruno Maes (katikati), mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti, akitembelea shule moja huko Artibonite.

Wametiwa kiwewe na kutishwa

"Hali ni mbaya kwa watoto," amesema Bwana Maes wa UNICEF. "Watoto wanauawa, kujeruhiwa, kubakwa, kuhamishwa na kunyimwa huduma za msingi, ikiwa ni pamoja na elimu," akiongeza kuwa "wanatishwa na kujeruhiwa, wengine baada ya kushuhudia miili iliyochomwa moto mitaani”.

Ameendelea kusema kuwa “Huku kukiwa na hatari za wazi, wazazi "bado wanataka kuwapeleka watoto wao shule. Elimu ni kiini cha kila familia ya Haiti watu wanaithamini sana.”

Wakati magenge yanaendelea kupanua wigo wa udhibiti wao wa barabara na bandari muhimu, mtego wao unaenea nje ya mji mkuu na tishio kwa usalama wa shule linaongezeka.

Licha ya hayo, shule nyingi nje ya maeneo yenye matatizo yanayodhibitiwa na magenge ya uhalifu la Port-au-Prince na Artibonite bado zinafanya kazi. Wengi wamekubali watoto ambao wametoroka kwa sababu ya ghasia na ukosefu wa usalama, ingawa baadhi ya wazazi wanashindwa kulipa karo kutokana na kuongezeka kwa umaskini.

Watoto wa shule nchini Haiti wakipata  mlo kupitia programu ya mlo shuleni inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini humo.
© WFP/Jonathan Dumont
Watoto wa shule nchini Haiti wakipata mlo kupitia programu ya mlo shuleni inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini humo.

Hatua jumuishi kwa mzozo wa Haiti

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi pamoja ili kutoa mahitaji muhimu ya kuokoa maisha, kama vile chakula, maji na makazi, kwa maelfu ya Wahaiti wanaohitaji msaada na kusaidia kuwarejesha watoto shuleni kwa kutumia mbinu mpya.

Juhudi hizo ni pamoja na mpango wa Shirika laUmoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, unaotoa msaada wa kisaikolojia kwa wanafunzi waliolazimishwa kuacha shule kutokana na ghasia, na wa sirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, unaounga mkono milo ya moto kwa watoto 250,000 kote nchini.

Sehemu ya kazi ya UNICEF ni kusaidia familia zilizoathiriwa na unyanyasaji na kufurushwa makwao ili kuwajumuisha watoto katika elimu rasmi. 

Ambako hili haliwezekani kwa sasa shirika linafanya kazi na washirika kuanzisha mazingira mbadala, salama na ya muda ya kujifunza.

Wafanyakazi wa kujitolea wakitayarisha milo ya shule kwa kutumia viambato vilivyokuzwa katika eneo la Gonaives, kaskazini-magharibi mwa Haiti.
© WFP/Pedro Rodrigues
Wafanyakazi wa kujitolea wakitayarisha milo ya shule kwa kutumia viambato vilivyokuzwa katika eneo la Gonaives, kaskazini-magharibi mwa Haiti.

Tathimini mpya kuhusu shule

Lengo ni kuwarejesha watoto katika kujifunza na katika programu za mlo shuleni, kulingana na ripoti ya UNICEF, iliyochapishwa kwa Kifaransa mwishoni mwa mwezi Machi.

Ikiwa shule zitaendelea kufungwa, masomo ya masafa marefu yanaweza kutumwa kupitia redio, televisheni na majukwaa ya kujifunza kielektroniki. 

UNICEF inashirikiana na wizara ya elimu kutafuta njia ya kuwasilisha hili kupitia matangazo ya Radio Télé Éducative (RTE) kwenye redio ya taifa ya Haiti.

Fursa zingine za kushirikisha wanafunzi wakati wa migogoro ni pamoja na kuongeza uwezo katika shule zinazochukua wanafunzi waliotawanywa na machafuko.