Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aziomba jumuiya za kimataifa kuwasaidie wananchi wa Haiti

Mwanamke aliyehamishwa na Ghasia katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince akifua nguo katika bustani ya jiji.
© UNICEF
Mwanamke aliyehamishwa na Ghasia katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince akifua nguo katika bustani ya jiji.

Guterres aziomba jumuiya za kimataifa kuwasaidie wananchi wa Haiti

Msaada wa Kibinadamu

Ulimwengu lazima uchukue hatua sasa kukomesha ghasia na ukosefu wa utulivu nchini Haiti, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo wakati akitoa ombi la wadau wote kuchukuliwa hatua za haraka za kusaidia masuala ya kibinadamu, usalama na kisiasa.

Akizungumza akiwa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Guterres aliwaeleza waandishi wa habari kuhusu kuwa wiki iliyopita alifanya ziara nchini Haiti na pia kushiriki mkutano wa kilele wa viongozi wa kanda ya Karibea uliofanyika Trinidad na Tobago, ambako kulikuwa na kikao maalum kuhusu Haiti.

Amesema wananchi wa Haiti "wamekwama katika ndoto mbaya" huku magenge yenye silaha yakizunguka mji mkuu wa Port-au-Prince, kufunga barabara, kuzuia upatikanaji wa chakula na huduma za afya, na kudhoofisha utoaji wa misaada wa kibinadamu."

Aliwaambia wanahabari kwamba magenge ya utekaji nyara huko yanatumia utekaji nyara na unyanyasaji wa kingono kama silaha kutisha jamii nzima.

"Nimesikia simulizi za kutisha za wanawake na wasichana kubakwa na genge, na watu kuchomwa moto wakiwa hai," alisema.

Katika ziara yake ya siku moja nchini Haiti, Guterres alikutana na Waziri Mkuu wan chi hiyo Ariel Henry na wawakilishi kutoka sekta nyingine za kijamii, na kukiri kuona dalili za matumaini na uwezekano wa kutatua changamoto zinazowakabili.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema inahitaji kuchukuliwa hatua katika nyanja kadhaa na utambuzi wa ukweli wa msingi.

"Hakuwezi kuwa na usalama endelevu bila suluhu za kisiasa zinaloruhusu kurejeshwa kwa taasisi za kidemokrasia. Na hakuwezi kuwa na suluhu za kisiasa za kudumu na shirikishi bila kuboreshwa kwa hali ya usalama.”

Maeneo 3 muhimu yakufanyiwa kazi

Ameitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua katika kile alichokiita maeneo matatu muhimu, 

Mahitaji ya dharura ya kibinadamu

Akianza na kushughulikia mahitaji ya dharura ya kibinadamu nchini humo. Mpango wa dola milioni 720 kusaidia zaidi ya watu milioni tatu ambao kwa sasa unafadhiliwa kwa asilimia 23 pekee.

"Ninatoa wito kwa ulimwengu kupanua njia ya kusaidia na kujaza pengo hilo la kifedha bila kuchelewa," alisema.

Kulisaidia jeshi la polisi

Katibu Mkuu pia alitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa "na nchi zote zinazoweza kuchangia" kuunda mazingira ya kuruhusu kutumwa kwa jeshi la kimataifa Kwenda kusaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti, suala lililoombwa na serikali ya Hait mwezi Oktoba 2022.

"Narudia: Hatuitishi ujumbe wa kijeshi au wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa," alisema. "Tunatoa wito kwa kikosi chenye nguvu cha usalama kilichotumwa na Nchi Wanachama kufanya kazi bega kwa bega na Polisi wa Kitaifa wa Haiti ili kushinda na kusambaratisha magenge ya kihalifu na kurejesha usalama nchini kote."

Aliongeza kuwa jeshi la polisi pia litahitaji fedha, mafunzo na vitendea kazi, ambavyo vyote ni muhimu katika kurejesha mamlaka ya Serikali na utoaji wa huduma muhimu.

Utangamano wa kitaifa kusaka suluhu kisiasa

Guterres pia alitoa wito kwa wahusika wote wa kijamii na kisiasa nchini Haiti kuongeza juhudi kuelekea kutafuta suluhisho la kisiasa linalohitajika sana. 

Pia alionesha kuunga mkono kikamilifu juhudi za upatanishi zinazofanywa na kambi ya kikanda, CARICOM.

"Zikichukuliwa pamoja, hatua hizi tatu muhimu na kwa wakati mmoja litakuwa jamno la msingi katika kuvunja mzunguko wa mateso ya wananchi wa Haiti, kwani itakuwa wameweza kushughulikia changamoto kubwa za kibinadamu na usalama na kutengeneza njia ya kisiasa kutoka kwa shida," alisema Guterres.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litajadili ripoti ya hivi karibuni zaidi ya Katibu Mkuu kuhusu Haiti wakati wa mkutano wao hii leo.