Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu wapoteza maisha katika tetemeko Türkiye na Syria UN iko tayari kusaidia

Wafanyakazi wa uokozi wakiwatafuta manusura katika jengo moja mjini Samada, Syria lililoharibiwa na tetemeko la ardhi la Februari 6.
© UNOCHA/Ali Haj Suleiman
Wafanyakazi wa uokozi wakiwatafuta manusura katika jengo moja mjini Samada, Syria lililoharibiwa na tetemeko la ardhi la Februari 6.

Maelfu wapoteza maisha katika tetemeko Türkiye na Syria UN iko tayari kusaidia

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema amesikitishwa sana na taarifa kuhusu hasara kubwa ya kupotea kwa maisha ya watu iliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililoathiri maeneo ya kusini mwa Türkiye na kaskazini mwa Syria mapema leo. 

Katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York Marekani Antonio Guterres amesema “Zaidi ya watu 1,500 wameripotiwa kupoteza maisha na wengine wengi kwa maelfu kujeruhiwa na idadi ya vifo inaendelea kuongezeka huku juhudi za uokoaji zikiendelea.” 

Ameendelea kusema kwamba “Moyo wangu unawaendea watu wa Türkiye na Syria katika saa hii ya msiba mkubwa. Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia ahueni ya haraka wote waliojeruhiwa. Umoja wa Mataifa umejitolea kikamilifu kuunga mkono hatua za uokozi na kuwasaidia wenye uhitaji. Timu zetu ziko huko kutathmini mahitaji na kutoa msaada.” 

Guterres pia amesema anaitegemea jumuiya ya kimataifa kusaidia maelfu ya familia zilizokumbwa na janga hili, wengi wao wakiwa tayari wanahitaji sana misaada ya kibinadamu katika maeneo ambayo fursa ya ufikiaji ni changamoto. 

Rais wa Baraza Kuu 

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 77 Csaba Kőrösi akiongeza sauti yake katika zahma hii kabla ya kutoa taarifa yake kwenye kikao cha kuwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu kazi za shirika aliwataka nchi wanachama kusimama na kuwa na muda wa ukimya ili kuwaenzi waathirika wa tetemeko hilo nchini Türkiye na Syria. 

Kisha akasema,  

"Kabla ya kuendelea na masuala ya ajenda yetu ningependa, kwa niaba ya Baraza Kuu, kutoa pole na rambirambi zetu za dhati kwa serikali na watu wa Türkiye na jamhuri ya Syria kwa kupoteza maisha na uharibifu mbaya ambao umetokana na tetemeko la ardhi hivi karibuni. Sasa ninawaalika wanachama kusimama na kutumia dakika moja ya ukimya katika kuwakumbuka waliopoteza maisha.” 

Mwathirika wa tetemeko la ardhi la Februari 6 akitibiwa Samada, Syria.
© UNOCHA/Ali Haj Suleiman
Mwathirika wa tetemeko la ardhi la Februari 6 akitibiwa Samada, Syria.

Hatua zinazochukuliwa na UN 

Timu za matibabu ya dharura kutoka shirika la afya la Umoja wa Mataifa ulimwenguni, WHO, zimeruhusiwa kutoa huduma muhimu kwa waliojeruhiwa na walio hatarini zaidi, amesema mkuu wa WHO Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia mtandao wake wa tweet. 

Timu za wataalamu wa Umoja wa Mataifa kutoka ofisi ya tathmini na uratibu wa maafa ya Umoja wa Mataifa (UNDAC) pia wametuma ujumbe kupitia ukurasa wao wa Tweeter wakisema kwamba wako tayari kutumwa Kwenda kusaidia, huku kukiwa na machapisho mengi ya kutisha ya mitandao ya kijamii yanayoonyesha majengo makubwa yakiporomoka. 

Katika taarifa iliyotolewa pia kupitia Twitter, Umoja wa Mataifa nchiniTürkiye umeonyesha masikitiko makubwa ya kupoteza maisha na uharibifu wa mali.  

Timu hiyo imetoa salamu za rambirambi kwa familia za waathirika pamoja na watu na Serikali ya nchi hiyo na kuwatakia majeruhi wote ahueni ya haraka. 

"Umoja wa Mataifa Türkiye unaonyesha mshikamano wake na nchi ya Türkiye na uko tayari kusaidia." 

Msaada wa kuokoa maisha Syria umeathiriwa 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA imesisitiza kwamba tetemeko la awali la kipimo cha Rishta 7.8 lilipiga katika kilele cha majira ya baridi.  

Kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa kusini mwa Türkiye, ambapo ni karibu na Gaziantep kituo muhimu cha misaada cha Umoja wa Mataifa kaskazini mwa Syria na hivyo kituo hicho kuwa miongoni mwa miji iliyoathiriwa. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi nchini Syria (UNHCR) nalo limeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba "limehuzunishwa sana na vifo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi la asubuhi ya leo," na kuongeza kuwa "linaratibu kikamilifu hatua za misaada na Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wahusika wengine wa kibinadamu kutoa msaada kwa wale wanaohitaji nchini Syria”. 

Maeneo mengine yaliyoathirika 

Ingawa tetemeko la ardhi lilisikika mbali kama vile nchini Lebanon, lakini eneo la karibu na nyumbani, Aleppo kaskazini mwa Syria na Idlib pia yameripotiwa kuona maelfu ya majengo yakiporomoka, zikiwemo hospitali mbili. 

Mahitaji ya kibinadamu kaskazini mwa Syria tayari ni makubwa, kwani eneo hilo ni makazi ya mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita vya muda mrefu vya nchi hiyo. 

Theluji na mvua vimetatiza kazi ya vikundi vya uokoaji, ambavyo familia zao pia ni miongoni mwa zile zinazoaminika kuzikwa chini ya majengo yaliyoporomoka. 

Majengo mjini Idlib, Syria, yameharibiwa na tetemeko la ardhi lililolikumba eneo hilo.
© UNOCHA/Ali Haj Suleiman
Majengo mjini Idlib, Syria, yameharibiwa na tetemeko la ardhi lililolikumba eneo hilo.

Msaada wa UN kote 

Baada ya ombi rasmi la msaada wa kimataifa kutoka Ankara, shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia watoto, UNICEF, lithibitisha kuwa liko tayari kusaidia jibu la dharura. 

"Mioyo na mawazo yetu yako kwa watoto na familia huko Türkiye na Syria walioathiriwa na matetemeko makubwa ya ardhi. Rambirambi zetu za dhati kwa wale waliopoteza wapendwa wao,” amesema mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Catherine Russell. 

Iikirejelea ujumbe huo wa msaada, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, lilisema kuwa ghala hilo huko Gaziantep limetayarisha bidhaa zisizo za chakula na misaada muhimu tayari kutumwa inakohitajika.  

"Timu za IOM pia zinafanya tathmini za chini kwa chini ili kujulisha hatua zinazochukuliwa", amesema msemaji wa shirika hilo Safa Msehli. 

Mkurugenzi mkuu wa IOM Antonio Vitorino ametuma salamu za mshikamano wake na watu huko Türkiye, Syria, Lebanon, maeneo ya Palestina, Jordan na wale wote walioathiriwa kufuatia tetemeko la ardhi lililosababisha vifo ya watu wengi. Ameongeza kuwa “Tutafanya kazi kwa karibu na serikali katika eneo hili kusaidia wale walioathiriwa na kusaidia kupunguza mateso yao.” 

Hali halisi ya maafa 

Duru zinasema karibu watu 2000 wamepoteza maisha kwenye matetemeko matatu yaliyotokea moja baada ya lingine Kusini mwa Uturuki na kutikisha maeneo ya Jirani ikiwemo Syria na Lebanon 

Serikali ya Türkiye imesema hili ni tetemeko lenye nguvu kuwahi kuikumba nchi hiyo tangu mwaka 1939. 

Mishtuko mingine 78 imeripotiwa baada ya tetemeko la pili kutokea katika majimbo ya Ekinozu na Kahramanmaras. 

Serikali ya Uturuki imetangaza hali ya dharura na kuomba msaada wa kimataifa.