Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji dola milioni 397 kukabiliana na zahma ya tetemeko la ardhi Syria: Guterres

Jamii zimehifadhiwa kwenye msikiti katika wilaya ya Al-Midan ya Aleppo, Syria, ambayo imegeuzwa kuwa makazi ya pamoja.
© UNHCR/Hameed Maarouf
Jamii zimehifadhiwa kwenye msikiti katika wilaya ya Al-Midan ya Aleppo, Syria, ambayo imegeuzwa kuwa makazi ya pamoja.

Tunahitaji dola milioni 397 kukabiliana na zahma ya tetemeko la ardhi Syria: Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa leo umezindua ombi la dola milioni 397 ili kukabiliana na hali ya kibinadamu kwa muda wa miezi mitatu ijayo kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoathiri mamilioni ya watu nchini Syria.

Akizindua ombi hilo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Pia tuko katika hatua za mwisho za mchakato wa kuzindua ombi kama hilo kwa ajili ya Uturuki iliyoathirika pia.’

Mara tu baada ya matetemeko hayo ya ardhi ya Syria na Uturuki Umoja wa Mataifa ulitoa haraka dola milioni 50 kupitia mfuko wake wa dharura CERF kusaidia hatua za haraka kwa waathirika.

Mahitaji ya kibinadamu ni makubwa sana

Guterres amesema mahitahi ya kibinadamu kufuatia tetemeko hilo ni makubwa sana na “juhudi za Syria zinaleta pamoja mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na washirika wa kibinadamu na watasaidia kupata msaada unaohitajika haraka wa kuokoa Maisha kwa watu takriban milioni 5 raia wa Syria ukiwemo malazi, huduma za afya, chakula na ulinzi.”
Amesisitiza kuwa njia bora ya kushikamana na watu wa Syria ni kutoa msaada wa dharura wa fedha zinazohitajika.
Pia amesema “Sote tunafahamu kwamba msaada wa kuokoa maisha haifiki kwa kasi na kiwango kinahohitajika kwa walengwa.”
Ameongeza kuwa wiki moja baada ya matetemeko ya ardhi mamilioni ya watu katika maeneo yaliyoathirika wanahaha kuishi, hawana makazi na wakikabilkiwa na mazingira mabaya ya bariki kali.

Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa na wadau “Tunafanya kila liwezekanalo kubadili hali hiyo, lakini jitihada zaidi zinahitajika. Nina ujumbe wa haraka kwa jumuiya ya kimataifa , madhila yanayowakabili binadamu hawa kutokana na janga hilo la asili yasiongezwe na vikwazo vya binadamu vya fursa, fedha na mahitaji”

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba “Msaada lazima ufikishwe kutoka kila kona Kwenda kila upande na kupitia njia zote bila vikwazo vyovyote.Wakati huu tunapozungumza msafara wa malori 11 uko njiani kuvuka mpaka kupitia Bab al-Salam na mingine mingi itafuata.”

Ukarimu na ubinadamu wa Syria hautosahaulika

Amekumbusha kwamba alipokuwa mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR alishuhudia ukarimu na ubinadamu wa watu wa Syria wa kupokea na kuwalinda wakimbizi kutoka nchi jirani na kushiriki nao rasilimali chache walizonazo.

Hivyo amesema “Moyo huo wa ukaribu ni lazima ulipwe fadhila sasa na jumuiya ya kimataifa. Ninatoa wito kwa nchi wanachama na wengine kufadhili kikamilifu juhudi hizo bila kuchelewa na kusaidia maisha ya mamilioni ya watoto, wanawake na wanaume ambayo yamepinduliwa na janga hili la kihistoria. Huu ni wakati wa mshikamano kwa ajili ya utu wa pamoja na hatua za pamoja.”