Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada zaidi wafikia manusura wa tetemeko la ardhi nchini Syria lakini haitoshelezi - UN

Familia moja kutoka eneo la Rumaila katika wilaya ya Jableh, kaskazini magharibi mwa Syria wakisimama karibu na nyumba yao iliyoharibiwa.
© UNICEF/Hasan Belal
Familia moja kutoka eneo la Rumaila katika wilaya ya Jableh, kaskazini magharibi mwa Syria wakisimama karibu na nyumba yao iliyoharibiwa.

Msaada zaidi wafikia manusura wa tetemeko la ardhi nchini Syria lakini haitoshelezi - UN

Msaada wa Kibinadamu

Msafara wa pili wenye shehena za misaada umewasili kaskazini-magharibi hii leo kusaidia manusura wa tetemeko la ardhi huku watoa misaada ya kibinadamu wakisema bado misaada zaidi inahitajika na haraka zaidi. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM linasema msafara huo wenye jumla ya malori 14 umeingia Syria kutokea Uturuki kupitia mpaka wa Bab-al Hawa ulioko eneo linaloshikiliwa na wapinzani wa serikali ya Syria. 

Eneo hilo la mpaka ndio eneo pekee lililoidhinishwa kupitisha misaada kwa mujibu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hatua ambayo imesababisha kuibua wito kutoka pande mbali mbali ikiwemo Katibu Mkuu wa UN wa kutaka kusaka mbinu zaidi au njia zaidi za kuweza kufanikisha misaada kufika maeneo yote yaliyokumbwa na tetemeko bila vikwazo vyovyote. 

Vikwazo barabarani vyakwamisha harakati 

Likipigia chepuo wito unaoongezeka wa kimataifa wa kuhakikisha misaada inafika haraka na kwa urahisi upande wa kaskazini-magharibi mwa Syria, kupitia njia mpya badala ya kutegemea mpaka wa Bab-al Hawa pekee, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP limesema liko tayari kupeleka misaada eneo hilo ijapokuwa barabara zimeharibiwa na tetemeko la jumatatu. 

 “Hii inazorotesha usambazaji wetu wa misaada,” amesema Corinna Fleischer, Mkurugenzi wa WFP Kanda ya Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Mashariki ya Ulaya, akiongeza kuwa “tunahitaji kuwa na uwezo wa kuvuma mipala, tunahitaji maafisa wa forodha waweko wa kutosha…tunahitaji pande zote kuchukua hatua sahihi hivi sasa.” 

Amesisitiza kuwa usambazaji wa misaada inayovuka mpaka inapaswa kuanza tena hivi sasa na kasi iongezwe kutoka maeneo yanayoshikiliwa na serikali Kwenda yale yanayoshikiliwa na upinzani, “hii ni kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa eneo la kaskazini-mashariki mwa Syria wanategemea misaada ya kibinadamu pakee.” 

Misaada iliyokuwa imetangulizwa awali na kuhifadhiwa kwenye bohari kabla ya tetemeko la ardhi hivi sasa inasambazwa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR likiongeza kuwa linatumai makubaliano kati yake na serikali yataweza kuruhusu ufikishaji wa haraka na wa mara kwa mara wa misaada kwenye eneo hilo. 

Mbwa wa uokoaji akishiriki katika shughuli ya uokoaji manusura kwenye vifusi kufuatia tetemeko lililokumba Uturuki. Hapa ni katika mji wa Osmaniye.
© UNOCHA/INSARAG
Mbwa wa uokoaji akishiriki katika shughuli ya uokoaji manusura kwenye vifusi kufuatia tetemeko lililokumba Uturuki. Hapa ni katika mji wa Osmaniye.

Akiba ya misaada ‘inapukutika’ 

“Akiba iliyoko inamalizika tunahitaji kupata vibali au ruhusa ili tuweze kuingiza misaada mingine zaidi,” amesema Bi. Fleischer huku akikazia wito wa kutaka kituo cha mpaka cha Bab al-Salam – ambacho pia kinawezasha kuingia kaskazini-magharibi mwa Syria kiweze kufunguliwa tena. 

Katika siku nne za mwanzo tangu tetemeko la ardhi kukumba eneo hilo, WFP imefikisha msaada kwa watu 115,000 nchini Syria na Uturuki. 

Kwa mujibu wa ripoti mpya, zaidi ya watu 22,000 wamekuta kutokana na tetemeko hilo la ardhi huku wengine wamkumi ya maelfu wakiripotiwa kuhofia kurejea kwenye majengo yao, pengine yataporomoka na hivyo wanalala kwenye magari, mahema na kwingineko ambako wanaweza kupata hifadhi wakati huu ambapo kuna baridi kali. 

WFP inapatia familia hizo vyakula vya moto na vile ambavyo viko tayari kuliwa badala ya kupika. 

“Kwa maelfu ya watu walioathiriwa na matetemeko, chakula ni moja ya kipaumbele cha sasa na kipaumbele chetu ni kuhakikisha tunafikisha kwa wale wanaohitaji kwanza na haraka,” amesema Bi. Fleischer. 

Kwa jumla, WFP inahitaji dola milioni 77 kukidhi mahitaji ya mgao wa chakula na vyakula vya moto kwa watu 874,000 walioathiriwa na tetemeko la ardhi huko Uturuki na Syria. 

Hii inajumuisha wakimbizi wapya wa ndani 284,000 nchini Syria na watu 590,000 nchin Uturuki, wakiwemo wakimbizi 45,000 kutoka nje na wakimbizi wa ndani 545,000. 

Dharura ya kiafya 

Katika hatua nyingine, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limeesma liliachia vifaa vya matibabu kwa ajili ya hospitali 16 zinazotibu manusura wa tetemeko la ardhi lililokumba eneo hilo la kaskazini-magharibi mwa Syria siku ya jumatatu. 

Jana Alhamisi, vifaa vya matibabu vikiwemo vya upasuaji kutoka kitou cha bohari ya WHO huko Dubai, Falme za kiarabu viliwasili pia Uturuki lakini “mahitaji bado ni makubwa, kwani mamia ya kliniki na hospitali Uturuki na Syria zimeharibiwa na matetemeko.” 

Wataalamu wa kimataifa wa magonjwa mahsusi wakiratibiwa na WHO wamefikishwa maeneo hayo “na wengine zaidi wanakwenda ili kuunga mkono wataalamu wa kitafa ambao tayari wanakabiliwa na kazi kubwa,” amesema Dkt, Margaret Harris, msemaji wa WHO. 

Mwanamke mmoja, ambaye nyumba yake iliharibiwa katika tetemeko la ardhi, anapumzika katika makazi ya watu waliokimbia makazi yao katika wilaya ya Jableh. Syria
© UNICEF/Hasan Belal
Mwanamke mmoja, ambaye nyumba yake iliharibiwa katika tetemeko la ardhi, anapumzika katika makazi ya watu waliokimbia makazi yao katika wilaya ya Jableh. Syria

Watu milioni 5.3 hawana makazi 

Kadri Umoja wa Mataifa na wadau wanavyoimarisha usaidizi wao, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema takribani watu milioni 5.3 nchini Syria wamesalia bila makazi kufuatia tetemeko hilo la ardhi.  

“Kulikuweko tayari na watu milioni 6.8 nchini Syria ambao walikuwa wakimbizi wa ndani. Na hii ni kabla ya tetemeko la ardhi,” amesema Sivanka Dhanapala, mwakilishi wa UNHCR nchini Syria, akizungumza kutoka mji mkuu wa taifa hilo, Damascus. 

Suala la kuwapatia watu hao malazi na vifaa vingine vya misaada limesalia kuwa kipaumbele cha hatua za UNHCR na kuhakikisha kuwa vituo vya kupokea wakimbizi hao wa ndani vina huduma za kutosha kama vile mahema, matandiko, makaratasi ya nailoni, blanketi ya kutia joto, mikeka ya kulalia na nguo za msimu wa baridi kali.