Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 300,000 walioathirika na temeko Syria wamepokea msaada wa WFP

WFP inaharakisha msaada muhimu wa chakula kwa familia nchini Syria zilizoathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi.
© Al-Ihsan Charity
WFP inaharakisha msaada muhimu wa chakula kwa familia nchini Syria zilizoathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi.

Watu 300,000 walioathirika na temeko Syria wamepokea msaada wa WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema linaendelea na juhudi za kuhakikisha kila aliyeathirika na tetemeko la ardhi nchini Syria na Uturuki anapata msaada wa chakula unahojitajika.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis mkurugenzi na mwakilishi wa WFP nchini Syria Kenn Crossley amesema kupitia ushirikiano uliopo kwa muda mrefu na akiba ya chakula iliyokuwa nayo shirika hilo limekuwa likiwasaidia washirika wake tangu mwanzo wa zahma hiyo na lilikuwa likigawa chakula cha moto ambacho kiko tayari kuliwa katika malazi mbalimbali saa chahe tu baada ya tetemeko kutokea.

Hadi kufikia leo 14 Februari shirika hilo linasema limeshawasidia watu 150,000 walioathirika na tetemeko hilo katika maeneo yote ynayodhibitiwa na serikali na yanayodhibitiwa na makundi mengine.

Maeneo yaliyofikiwa hadi sasa

Kwa upande wa Kaskazini Magharibi mwa Syria pekee WFP imewafikia watu 90,000 zaidi ya wale elfu 90 ambao hupata msaada wa kila siku kupitia mnyororo wa msaada wa chakula uliopo.

Katika maeneo yanayodhibitiwa na serikal;i ya Aleppo, Hama, Tartous na Latakkia WFP imewasaidia waathirika wa tetemeko 60,000 kwa kuwapa msaada wa dharura nah awa hawajumuishi wale ambao wamekuwa wakipokea msaada wa kawaida wa chakula.

Shirika hilo la mpango wa chakula pia limesema linaunga mkoni tarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Antonio Guterres na kukaribisha tangazo la kufunguliwa kwa njia nyingine ya kuvuka mpaka kuweza kufika Kaskazini Magharibi mwa Syria kutokea Uturuki ili kuwasaidia watu popote walipo.

Kikosi cha kiufundi na mipango cha WFP kinashirikiana kwa karibu na wadau wote wa kibinadamu ili kujipanga na kupanua wigo wan jia za kuikia Kaskasini magharibi mwa Syria kufikisha misaada ya kibinadamu.

Shirika hilo pia linapanga kuongeza misaada yake Kaskazini Magharibi mwa Syria kupitia maeneo yanayodhibitiwa na serikali kuingia eneo hilo linalodhibitiwa na makundi mengine ambayo si vikosi vya serikali.

UN na mashirika yake wako tayari

 Msafara wa malori 18 ya msaada wa chakula, pamoja na misaada mingine kutoka kwa mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa, uko tayari tangu siku kadhaa zilizopita kupeleka msaada Kaskazini-magharibi mwa Syria.

Kwa bahati mbaya, makubaliano bado hayajafikiwa kati ya pande zote kusaidia na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za kibinadamu kwa watu wanaohitaji.

WFP imesema “inahitaji pande zote kuunga mkono na kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kupitia njia zote, kuvuka mpaka na njia panda, ili kuwafikia watu wengi zaidi walioathiriwa na tetemeko la ardhi na kujaza akiba kwa ajili yao na kwa watu ambao tayari wanapokea msaada wa chakula wa kawaida wa WFP kila mwezi.”

Syria iko katika hali mbaya sana kufuatia miaka ya changamoto mfululizo. Jamii zilizo karibu zaidi na kitovu cha matetemeko ya ardhi tayari zilikuwa zikipambana na athari za miaka 12 ya migogoro na baadhi ya watu huko wako katika hali mbaya zaidi za kijamii na kiuchumi duniani.

“WFP imekuwa ikiwasaidia kikamilifu watu wa Syria tangu mwanzo wa mgogoro na inaendelea kufanya hivyo lakini inahitaji upatikanaji na fedha zaidi ili kuendeleza hatua hizo na kuuongeza.”

Matetemeko ya ardhi yamezidisha hali ambayo tayari ilikuwa moja ya majanga makubwa zaidi ya njaa ulimwenguni kuwa mbayá zaidi.

Zaidi ya nusu ya watu wana uhaba wa chakula. WFP imekuwa ikiwahudumia watu milioni 5.5 kila mwezi kwa msaada wa jumla wa chakula, wengi wao wakiwa katika maeneo ambayo sasa yameathiriwa vibaya na tetemeko la ardhi.

WFP inahitaji haraka dola milioni 396 ili kuweza kuendelea kuwasaidia watu walioathiriwa hivi karibuni na tetemeko la ardhi, pamoja na watu milioni 5.5 ambao tayari WFP imekuwa ikiwasaidia na ambao mahitaji yao na uwezo wa kukabiliana na majanga umekua mbaya zaidi.