Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wapatia huduma za matibabu wananchi CAR

Walinda amani wa UN kikosi cha 6 cha Tanzania nchini CAR wafanya matibabu kwa wananchi
Picha: Kapteni Mwijage Francins Inyoma
Walinda amani wa UN kikosi cha 6 cha Tanzania nchini CAR wafanya matibabu kwa wananchi

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wapatia huduma za matibabu wananchi CAR

Amani na Usalama

Wananchi wa eneo la Potopoto nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, wameeleza furaha yao baada ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa Kikosi cha 6 cha Tanzania kinachohudumu nchini humo chini ya MINUSCA, kutumia wataalamu wake wa afya kutoa matibabu na dawa katika Zahanati ya Potopoto wilayani Mambéré-Kadéï.

Kapteni Nashiru Bakari Mzengo Mganga Mkuu wa TANBATT 6 amekabidhi dawa kwa mganga mkuu wa Zahanati ya Potopoto katika wilaya ya Mabere Kadei hapa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Shughuli hizi zimetanguliwa na TANBATT 6 kufanya usafi katika eneo la zahanati na kisha kuwafanyia matibabu wagonjwa kadhaa waliokuja kupata huduma katika zahanati hii ya Potopoto.

Bi.Janiruh akiwa amembeba mtoto wake ni mwananchi wa eneo hili kwa niaba ya wananchi wengine anaeleza alivyoipokea hatua hiiya walinda amani wa Umoja wa Mataifa akisema, "Tanzania na wanajeshi wake wana upendo sana kwetu tangu waanze jukumu la ulinzi wa amani tumeshuhudia mambo mengi mazuri kwao moja wapo ni kama hili hapa la kutupatia matibabu na dawa za kutumia ni jambo ambalo sisi kama wananchi wa Afrika ya kati tunajivunia kuwa na walinda amani kama hawa ambapo ushirikiano walio nao kwetu ni mkubwa zaidi ya upendo. "

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Hosiptali ya Potopoto, Dkt Sineh ametoa shukrani akisema, "shukrani zetu zimfikie mkuu wa kikosi cha TANBAT6 cha  kutoka Tanzania Kwa kutoa watabibu wa afya na kuja hapa kutoa matibabu Kwa wagonjwa wetu lakini pia kuamua Kufanya usafi na kutukabidhi dawa. Upendo huu ni mkubwa sana na niwahakikishie dawa hizi zilizokabidhiwa kwetu tutahakikisha tunawatibu raia wetu Ili wafaidike na walinda amani hawa wa Tanzania."