Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANBAT 5 yakabidhi jukumu la ulinzi wa amani wa UN kwa TANBAT 6 nchini CAR

Luteni Kanali Amin Stevin Mshana (katikati), Mkuu wa TANZBATT 6 akiwasili Berbérati, Mambéré-Kadéï, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
TANZBATT 6/Kapteni Mwijage Inyoma
Luteni Kanali Amin Stevin Mshana (katikati), Mkuu wa TANZBATT 6 akiwasili Berbérati, Mambéré-Kadéï, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

TANBAT 5 yakabidhi jukumu la ulinzi wa amani wa UN kwa TANBAT 6 nchini CAR

Amani na Usalama

Kikosi cha 5 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, TANBAT 5 kilichokuwa kinahudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, kimekamilisha muda wake  na kukipisha kikosi kingine cha 6 nacho kutoka Tanzania, TANBAT 6 ambacho kitaendeleza jukumu hilo. Kutoka Berberat, Kapteni Mwijage Inyoma ni Afisa Habari wa TANBAT 6 ametuandalia taarifa hii. 

Mwaka mmoja wa pilika za kuhamasisha amani, mshikamano na kuitunza amani umekamilika kwa kikosi cha wanajeshi walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, kikosi cha 5 yaani TANBAT 5 na wanaondoka wakifurahi kwamba wametoa mchango wao kwa amani ya ulimwengu kupitia Umoja wa Mataifa (MINUSCA).  

Luteni Kanali Adam Hamis Kiiza ni Kamanda Kikosi kinachoondoka anasema, “tumefanikiwa sana. Vitendo vya waasi ambao wamekuwa wakisumbua raia kwa kipindi chote ambacho tumekuwa hapa mwakamzima vimepungua sana sana sana.” 

Luteni Kanali Adam Hamis Kiiza (mwenye kitambulisho cha UN), mkuu wa TANZABATT 5 ambao wamekabidhi jukumu kwa TANZBATT 6 kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
TANZBATT 6/Kapteni Mwijage Inyoma
Luteni Kanali Adam Hamis Kiiza (mwenye kitambulisho cha UN), mkuu wa TANZABATT 5 ambao wamekabidhi jukumu kwa TANZBATT 6 kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Luteni Kanali Kiiza ametumia pia fursa hiyo kutoa ushauri kwa kikosi kipya akieleza kuwa wachukue pale kikosi chake kilipoishia ili wamalize kabisa vitendo vibaya vya waasi. 

Kwa upande wake Mkuu wa TANBAT 6 ambao ndio wanaolipokea jukumu hilo la ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa, Luteni Kanali Stevin Mshana anaeleza mikakati aliyonayo akisema, “tutafuata taratibi za Umoja wa Mataifa kioperesheni katika kutimiza jukumu la Umoja wa Mataifa. Tutajitahidi kuboresha utaalamu, kulinda zana na vifaa vilivyopo ili tuweze kukamilisha hizo taratibu za operesheni ambazo zinahusu Umoja wa Mataifa.” 

Mmoja wa raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, mkazi wa mjini Beriberati kwa niaba ya wengine akieleza kwa lugha ya kifaransa na kwa msaada wa mkalimani, anatoa shukrani kwa walinda amani akieleza kuwa, “wanajeshi kutoka Tanzania wanachukua nafasi kubwa sana katika suala zima la kuimarisha usalama wao binafsi lakini pian a mali zao wananchi.”