Natoka gerezani nikijiamini kwani nina stadi za ufundi- Mfungwa

Katika gereza la wanawake la Bimbo, mafunzo ya kutengeneza majiko yanayotumia nishati ya jua ambayo hayachafui mazingira.
MINUSCA - Herve Cyriaque Serefio
Katika gereza la wanawake la Bimbo, mafunzo ya kutengeneza majiko yanayotumia nishati ya jua ambayo hayachafui mazingira.

Natoka gerezani nikijiamini kwani nina stadi za ufundi- Mfungwa

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Umoja wa Mataifa na wadau kwa wafungwa 50 wanawake na wanaume kwenye mji mkuu Bangui, yameanza kuwapatia nuru wafungwa hao huku wakiwa na matumaini kuwa watakapokuwa huru, stadi hizo zitasaidia kujenga upya maisha yao.

Wafungwa wanaume 43 kutoka gereza Kuu la Ngaragba na wanawake 7  kutoka kituo cha kushikilia wanawake cha Bimbo, vyote kwenye mji  mkuu wa CAR, Bangui wakijifunza stadi za ufundi, ikiwa ni sehemu kujumuisha upya wafungwa pindi wakirejea nyumbani, kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuondokana na vikundi vilivyojihami ambavyo wafuasi wako magerezani. 

Stadi ni useremala, ufundi bomba na utengenezaji wa majiko yanayotumia nishati ya jua au sola, na mafunzo yanatolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA na shirika la kimatafa la Penal Reform 

Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Umoja wa Mataifa na wadau kwa wafungwa 50 wanawake na wanaume kwenye mji mkuu Bangui.
UN/MINUSCA - Leonel - GROTHE
Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na Umoja wa Mataifa na wadau kwa wafungwa 50 wanawake na wanaume kwenye mji mkuu Bangui.

Miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo ya miezi mitatu yalioyanza Mei hadi Juni mwaka huu ni huyu ambaye jina na sura yake vimehifadhiwa. “Wametufundisha ufungaji wa bomba, usambazaji wa maji na ufungaji wa vyoo na mabafu kwenye majengo. Stadi zote hizo nitatumia nikitoka gerezani” 

Mfungwa mwingine naye anasema “Awali sikuwa na stadi yoyote. Lakini sasa naweza kutengeneza samani zangu kama meza. Kwa  hiyo nikiachiliwa huru naweza kuendeleza na kujiendeleza maisha yangu.” 

Katika gereza la wanawake la Bimbo, mafunzo ni ya kutengeneza majiko yanayotumia nishati ya jua ambayo hayachafui mazingira. 

Mfungwa huyu ambaye jina na utambulisho wake vimehifadhiwa anasema, “Punde tu nikitoka gerezani, sitapoteza muda tena iwapo Mungu akinipa uhai. Nina watoto na wajukuu wanaonitegemea. Iwapo nitapata vifaa vyangu vya kazi, nitachukua watu wasio na kazi na kuwaonesha kile nilichojifunza gerezani.” 

Wafungwa hawa watapatiwa vyeti vya ueledi katika fani zao kama uthibitisho wa mafunzo na hivyo kuweza kuendelea na shughuli hizo uraiani.