Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wametufundisha kutumia majembe – Wakulima CAR 

Walinda amani wanahamasisha jamii kufanya shughuli za maendeleo kwa ajili ya nchi yao ya Jamhuri ya Afrika ya Kati
© MINUSCA
Walinda amani wanahamasisha jamii kufanya shughuli za maendeleo kwa ajili ya nchi yao ya Jamhuri ya Afrika ya Kati

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wametufundisha kutumia majembe – Wakulima CAR 

Amani na Usalama

Wananchi wa Kijiji cha Difolo katika viunga vya mji wa Berberati mkoa wa Mambéré-Kadéï nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wamewashukuru walinda amani wa kikosi cha 6 kutoka Tanzania kinachohudumu chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo (MINUSCA) baada ya wanalinda amani hao kuwafundisha wananchi hao kulima kwa kutumia jembe la mkono badala ya kulima kwa kutumia panga.  

Katika kijiji cha Difolo kwenye moja ya maeneo ambayo awali lilikuwa pori lakini sasa kuna kila dalili kuwa miezi michache ijayo litakuwa shamba lenye kupendeza bado pilika zinaendelea hapa, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanajeshi kutoka Tanzania wakiwa katika magwanda yao wameshika majembe wanawaonesha wananchi namna ya kutumia jembe la mkono.  

Kutokana na sababu ambazo bado haziko wazi, wananchi wa maeneo haya katika jamhuri ya Afrika ya kati, ingawa kwa ugumu mkubwa hulazimika kutumia mapanga kulima kama anavyofafanua Luteni Luteni Tryaphone Aloyce Afisa wa ofisi ya mahusiano na wananchi (CMIC - Civil Military in Coordination) anasema, “kipindi chan yuma walikuwa wanatumia mapanga katika kufanya kilimo chao. Lakini sasa ingawa hatujapiga hatua kubwa sana lakini tumeanza kidogo angalau watoke kwenye kulima kwa kutumia panga waweze kutumia majembe. Jembe mtu unaweza ukalima eneo kubwa sana ukilinganisha na panga. Kwa kuwa kule nyumbani tumekuwa tukilima kwa kutumia majembe tumeona hii elimu tukiwapa wao itawafaa wataweza kulima eneo kubwa na kuweza kulima mazao mengi.  

Wananchi hawa wa kijiji cha Difolo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wameyapokeaje mafunzo haya? Mamadou Pappy ni kiongozi wa kundi hili la wananchi ambao wanashiriki katika shamba darasa hili anasema, “ninaomba nitoe shukrani zangu kwa Mkuu wa kikosi cha 6 Luteni Kanali Amini Stephen Mshana kwa kuamua kuleta maafisa wake na askari ili kuja kutoa elimu ya kilimo cha ujasiliamali kwa wanawake hawa, wiki chache zilizopita tumepata elimu kama viongozi katika wilaya yetu ya Mambere Kadei  lakini leo wemekuja pia kutupa elimu zaidi kuhusu kilimo. Asante sana na undugu wetu na walinda amani kutoka Tanzania unazidi kuonekana siku hadi siku kwa mengi tunayosaidiwa." 

Naye mwenyeki wa akina mama wa kikundi hicho   Bi, Yakele Manuset   anasema, “sisi kama akina mama tunayofuraha sana kwa askari wa tanzania kuamua kuungana na sisi na kutupa elimu ya ujasiliamali, tumepata shida sana kwa kutumia mapanga kulima lakini sasa tutakuwa na utaalaam wa kuweza kutumia jembe la mkono kulima sehemu kubwa na kujipatia mazao na kipato ikiwa ni pamoja na chakula kwa familia zetu  

Mafunzo haya ya kilimo na ujasiriamali kwa kiasi kikubwa yameelekezwa kwa wanawake, Kapteni Jenifer Mrimakifi Mkuu wa kitengo Cha jinsia wa TANBATT 6 akiwa amesimama kwenye shamba darasa waliloanza nalo na sasa nyanya zinaelekea kukaribia hatua ya kuvunwa anaeleza kwa nini wanawake zaidi, “kwa sababu wanawake wamekuwa ni waathirika wakubwa hasa pale yanapotokea machafuko. Ndio maana tumewashika mkono ili kuwawezesha wanawake wenzetu kutokana na sisi wenyewe tunavyoguswa kwa kuona wanawake wenzetu wanavyohangaika na wakipata mateso. Wanawake wamekuwa na mwitikio mkubwa.   

Je baada ya wananchi kuanza kutumia majembe badala ya mapanga, hali ya ukosefu wa chakula itabadilika hapa? Hilo ni la kusubiri kuona lakini mabadiliko chanya yameshaanza kuonekana.