Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na Pakistan waitaka jumuiya ya kimataifa kuwasaidia waathirika wa mafuriko kujikwamua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko nchini Pakistan.
UN News
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alipotembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko nchini Pakistan.

UN na Pakistan waitaka jumuiya ya kimataifa kuwasaidia waathirika wa mafuriko kujikwamua

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo akizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa kimataifa kuhusu kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi Pakiastan, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwianisha"Hatua za kishujaa za watu wa Pakistani na juhudi zetu wenyewe na uwekezaji mkubwa wa kuimarisha jumuiya zao kwa ajili ya siku zijazo". 

Katika taarifa yake Antonio Gutefrres amesema "Kuijenga upya Pakistani kwa mnepo thabiti kutatumia zaidi ya dola bilioni 16 na fedha zaidi itahitajika kwa ajili ya ujenzi wa muda mrefu.” 

Guterres amehimiza pia uungwaji mkono sio tu kwa juhudi za uokozi na ukarabati, lakini pia mipango ya kushughulikia hali mbaya ya kijamii, mazingira na changamoto za kiuchumi. 

Familia za waliofurushwa makwao kutokana na mafuriko zikipatiwa msaada wa tibalishe ili kuepusha utapiamlo nchini Pakistani
© WFP/Marco Frattini
Familia za waliofurushwa makwao kutokana na mafuriko zikipatiwa msaada wa tibalishe ili kuepusha utapiamlo nchini Pakistani

Lengo la mkutano 

Mktano huo wa kimataifa ulioandaliwa kwa pamoja na serikali ya Pakistan na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP, lengo lake ni kuhamasisha msaada wa jumuiya ya kimataifa katika kujenga mnepo wa kujikwamua kwa Pakistan kutokana na mafuriko makubwa na mabaya zaidi ya mwaka 2022. 

Guterres amesema kwa miaka mingi Pakistan umedhihirisha ukarimu wake hasa kwa kuhifadhi mamilioni ya wakimbizi wa Afghanistan, kuwapa ulinzi, na kushiriki nao rasilimali chache ilizonazo. 

“Lakini yenyewe imepitia madhila chungu nzima , kuanzia mafuriko ya mara kwa mara, tetemeko la ardhi, athari za vitendo vya kigaidi na changamoto ya wakimbizi wa ndani.Na hivyo ni wajibu wa jumuiya ya kimataifa kwenda sanjari na ukarimu huo, ikionyesha mshikamano kamili na Pakistan katika wakati huu wa hali halisi ya uhitaji. Sio mshikamano tu ni haki.” 

Njia tatu za kuonyesha mshikamano na Pakistan 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba mshikano huo unapaswa kufanyika kwa njia tatu. 

Mosi: kwa uwekezaji mkubwa unaosaidia Pakistan kujenga upya nyumba, majengo na miundombinu mingine, kuanza kazi na kilimo, na kuhakikisha upatikanaji wa teknolojia na maarifa ili kusaidia kuhimili majanga yajayo. Na natumai mkutano huu utakuwa mwanzo wa uwekezaji huu mkubwa. 

Pili: Hatua za kuleta mapinduzi ya masuala ya fedha. Mbali na majanga ya asili, Pakistan pia ni mwathirika wa maafa ya kibinadamu ya mfumo wa kifedha wa kimataifa uliofilisika kimaadili. 

Mfumo ambao unazinyima nchi za kipato cha kati msamaha wa madeni na ufadhili wa masharti nafuu ili kuwekeza katika kujenga mnepo na hatua za uokoaji. Na hiyo lazima ibadilike. 

“Narudia wito wangu kwa viongozi wa kimataifa na benki za maendeleo za kimataifa kuunganisha nguvu na kubuni njia bunifu kwa nchi zinazoendelea kufikia msamaha wa madeni na ufadhili wa masharti nafuu wakati zinapouhitaji msaada zaidi.” 

Na tatu: Mnepo unahitaji hatua za maana za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ya sasa. 

“Ikiwa kuna shaka yoyote kuhusu hasara na uharibifu nenda Pakistani. 

Utaona hasara na utaona uharibifu na utaona mustakabali wetu wa pamoja.” 

Guterres ameongeza kuwa uamuzi uliochukuliwa katika COP27 huko Sharm el Sheikh kuhusu hasara na uharibifu lazima utekelezwe. 

Na nchi zilizoendelea lazima pia zitekeleze ahadi zao za kukabiliana na hali ya kifedha maradufu, na kutoa dola bilioni 100 kila mwaka ili kusaidia ulimwengu unaoendelea. 

Ramani inayoonyesha joto la uso wa bahari (SSTs) kama ilivyochakatwa na wanasayansi wa NASA.
NASA
Ramani inayoonyesha joto la uso wa bahari (SSTs) kama ilivyochakatwa na wanasayansi wa NASA.

Sote tuko hatarini 

Katibu Mkuu amesisitiza haja ya hatua za kimataifa za kuhakikisha ongezeko la joto duniani linasalia chini ya nyuzi joto 1.5C kama ilivyokubaliwa na viongozi wa dunia kwani amesema hivi sasa, wakati uzalishaji wa gesi chafu duniani ukiendelea kuongezeka, sote tuko hatarini. 

“Leo ni Pakistan, kesho inaweza kuwa katika nchi yako. Na nimechanganyikiwa kwamba viongozi wa kimataifa hawaipi dharura hii ya maisha au kifo hatua na uwekezaji unaohitajika, kwa sababu maneno pekee hayatoshi.” 

Guterres amekumbusha kwamba “Bila hatua, janga la mabadiliko ya tabianchi linakuja kwa ajili yetu sote. Sasa ni wakati wa kuwekeza katika ujasiri wa watu wa Pakistani na kuhamasisha uwekezaji mkubwa kutoka kwa ulimwengu ili kulipa fadhikla kwa ukarimu mkubwa ambao Wapakistani wameuonyesha daima. 

Mkutano huo wa kimataifa umehudhuriwa na wakuu wa nchi, mawaziri, viongozi wa taasisi mbalimbali za kimataifa za maendeleo na fedha na wawakilishi kutoka asasi za kiraia. 

Ni mkutano wa kwanza wa wa kimataifa wa aina yake kwa ajili ya fedha za kujenga mnepo tangu COP27 ambao utazindfua “Mkakati wa Pakistan wa kujikwamua na kunenga mnepo 4RF.”