Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi la dharura la dola milioni 160 limezinduliwa kuisaidia Pakistan kukabili athari za mafuriko

Mtoto akiwa amebeba kifurushi chake wakati gamilia zikihama kwenda kwenye maeneo salama baada ya kukumbwa na mafuriko kwenye jimbo la Balochistan nchini Pakistan
© UNICEF/A. Sami Malik
Mtoto akiwa amebeba kifurushi chake wakati gamilia zikihama kwenda kwenye maeneo salama baada ya kukumbwa na mafuriko kwenye jimbo la Balochistan nchini Pakistan

Ombi la dharura la dola milioni 160 limezinduliwa kuisaidia Pakistan kukabili athari za mafuriko

Msaada wa Kibinadamu

Ombi la dharura la dola milioni 160 kusaidia Pakistan kukabiliana na mafuriko makubwa limezinduliwa na Umoja wa Mataifa, leo ukilenga kuwafikia watu milioni 5.2 walio hatarini zaidi nchini humo.

Takriban watu milioni 33 wameathiriwa na mafuriko mabaya zaidi katika miongo kadhaa na zaidi ya watu 1,000, wengi wao wakiwa watoto, wamekufa tangu katikati ya Juni wakati mvua kubwa zilipoanza kunyesha nchini Pakistan amesema  leo mjini Geneva Uswis Jens Laerke, msemaji wa ofisi ya kuratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA.

Kupitia ujumbe wake wa video wakati wa uzinduzi wa ombi hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema "Pakistani inakabiliwa na mateso. Watu wa Pakistani wanakabiliwa na mvua kubwa za Monsoon zilizosababisha madhara ya mafuriko na athari zingine kubwa."

Kwa mujibu wa Bwana. Laerke, watu 500,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko "wanapata hifadhi katika kambi za misaada huku karibu nyumba milioni moja zimeharibiwa na zaidi ya mifugo 700,000 wameangamia".

Ameongeza kuwa hali ya kibinadamu pia imechangiwa na athari kubwa kwa miundombinu.

Uharibifu wa karibu kilomita 3,500 za barabara na madaraja 150 umezuia uwezo wa watu kukimbilia maeneo salama na pia kuathiri utoaji wa misaada kwa mamilioni wanaohitaji.

Malengo matatu muhimu

Kulingana na msemaji wa OCHA mpango huo unazingatia malengo matatu muhimu: kwanza, kutoa msaada wa kuokoa maisha na uwezo wa watu kuishi, kama vile huduma za afya, chakula, maji safi na makazi.

Pili, kuzuia milipuko mikubwa ya magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na kusaidia watoto wadogo na mama zao kwa lishe.

Lengo la tatu ni kuhakikisha kwamba "watu wanaweza kupata usaidizi na ulinzi kwa njia ambayo ni salama na yenye heshima, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa familia zilizopotezana na wapendwa wao".

Matthew Saltmarsh, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba hadi sasa, hatua za shirika hilo zimelenga "msaada wa dharura kwenda katika maeneo yaliyoathirika na kutoa misaada ya dharura. Msaada huo unahusisha vifaa vya kujikinga, lakini pia, majiko ya kupikia, mablanketi, na taa za miale ya jua au sola.”

Ameongeza kuwa "Hadi sasa, tumewasilisha msaada wa thamani ya dola milioni $1.5, lakini mengi zaidi yatahitajika katika wiki zijazo na pia katika malengo ya muda mfupi, ikiwa ni pamoja na msaada wa maendeleo”.

Athari mbaya

Pakistan imevumilia hali mbaya ya hewa ya monsoon tangu Juni, ambayo ilishuhudia viwango vikubwa vya mvua kwa asilimia 67 juu ya hali ya kawaida katika mwezi huo pekee, imesema OCHA katika taarifa yake.

Hadi kufikia tarehe 27 Agosti, mvua inayonyesha nchini kote imekuwa sawa na mara 2.9 ya wastani wa miaka 30 wa kitaifa.

Kufikia sasa, wilaya 72 kote Pakistani zimetangazwa na serikali kuwa zimekumbwa na janga na wakati mvua zinaendelea kunyesha, idadi ya wilaya zilizotangazwa na kukumbwa na maafa inatarajiwa kuongezeka.

"Tunaposikia mafuriko, mara nyingi tunafikiria tu juu ya watu kuzama, lakini ni zaidi ya hayo," amesema Christian Lindmeier, msemaji wa shirika la afya duniani (WHO) .

Ameongeza kuwa "Kuna majeraha yanayotokana na vifusi na uchafu unaoelea ndani ya maji. Kuna mshtuko wa umeme kutoka kwa nyaya, na kuna ukosefu wa maji ya kunywa, ambayo siyo tu shida kwa hali ya sasa, lakini kwa hali ya wastani pia".

Msemaji huyo wa WHO pia ameonya kwamba "angalau vituo vya afya 888 vimeathiriwa vibaya na 180 kati ya hivyo vimesambaratishwa kabisa wakati huu".

 

Pakistan ni muathirika mkubwa

Kwa mujibu wa rorodha ya kimataifa ya hatari za mabadiliko ya hali ya hewa mwaka 2021na Climate Watch, Pakistan ni miongoni mwa nchi 10 zilizoathiriwa zaidi na matukio mabaya ya hali ya hewa, licha ya kuwa na kiwango cha chini cha hewa ukaa.

Clare Nullis, msemaji wa shirika la utaribi wa hali ya hewa duniani (WMO), mafuriko hayo mabaya ni "Matokeo ya mabadiliko ya tabianchi ambapo yanazidi kuwa mbaya".

Ameongeza kuwa mwezi Machi na Aprili, Pakistan "ilikuwa katika hali ngumu ya wimbi hili la joto na ukame na sasa mambo yamebadilika".