Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majanga ya tabianchi na hali ya hewa 2022 yandhihirisha haja ya kuchukua hatua zaidi: WMO

Hali ya hewa na majanga kama mafuriko makubwa, joto na ukame viliathiri mamilioni ya watu na kugharimu mabilioni mwaka 2022, wakati ishara za hadithi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa zikiongezeka.
© WMO/Kureng Dapel
Hali ya hewa na majanga kama mafuriko makubwa, joto na ukame viliathiri mamilioni ya watu na kugharimu mabilioni mwaka 2022, wakati ishara za hadithi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa zikiongezeka.

Majanga ya tabianchi na hali ya hewa 2022 yandhihirisha haja ya kuchukua hatua zaidi: WMO

Tabianchi na mazingira

Masuala ya hali ya hewa, maji na majanga yanayohusiana na tabianchi, ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa, joto na ukame vimeathiri mamilioni ya watu na kugharimu mabilioni ya dola mwaka huu, huku ishara na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na binadamu vikiongezeka kwa mujibu wa taarifa ya tathimini iliyotolewa leo na shirika la umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO.

Taarifa hiyo inasema “matukio ya mwaka 2022 kwa mara nyingine tena yamesisitiza haja ya wazi ya kufanya mengi zaidi kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi  kwa ufuatiliaji bora wa suala hili na kuimarisha miapango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kupitia upatikanaji wa tahadhari ya mapema.” 

WMO inasema miaka minane iliyopita iko mbioni kuwa mika nane yenye joto zaidi kwenye rekodi ya dunia.  

Takwimu za joto duniani kwa mwaka 2022 zitatolewa katikati ya mwezi Januari. Lakini taarigfa hiyo inasema kuendelea kwa tukio la kupoa la La Niña, ambalo sasa liko katika mwaka wake wa tatu, kunamaanisha kuwa mwaka 2022 hautakuwa mwaka wenye joto zaidi katika rekodi.  

Lakini athari hii ya kupoeza itakuwa ya muda mfupi na haitabadilisha mwelekeo wa joto wa muda mrefu unaosababishwa na viwango vya rekodi kubwa vya gesi chafuzi zinazozua joto katika angahewa yetu. 

Viwango vya joto barani Ulaya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Afrika ni vya juu na vinatishai afya za binadamu, kilimo na mazingira
WMO Video screen shot
Viwango vya joto barani Ulaya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Afrika ni vya juu na vinatishai afya za binadamu, kilimo na mazingira

Wastani wa joto 2033 kuwa kati ya nyuzi joto 1.08 °C na 1.32°C 

Utabiri wa hali ya joto duniani wa kila mwaka wa ofisi ya utabiri wa hali ya hewa ya Met ya Uingereza unapendekeza kwamba wastani wa halijoto duniani kwa mwaka 2023 utakuwa kati ya nyuzi joto 1.08 °C na 1.32°C pamoja na makadirio ya kati ya nyuzi joto 1.20 °C juu ya wastani wa kipindi cha kabla ya maendeleo ya viwanda kati yam waka 1850- 1900.  

WMO inasema huu utakuwa mwaka wa kumi mfululizo ambapo halijoto imefikia angalau nyuzi joto 1°C juu ya viwango vya kabla ya viwanda.  

Kuna uwezekano japo wa muda mfupi wa kukiuka kiwango cha kikomo cha nyuzi joto 1.5°C cha makubaliano ya Paris na kunaongezeka kadri muda unavyopita. 

Katibu Mkuu wa WMO Profesa. Petteri Taalas amesema."Mwaka huu tumekabiliwa na majanga kadhaa ya hali ya hewa ambayo yamegharimu maisha ya watu wengi na uwezo wa watu kuishi, na kudhoofisha afya, chakula, nishati na uhakika wa maji na miundombinu. Theluthi moja ya Pakistan ilifurika, na hasara kubwa za kiuchumi na majeruhi ya binadamu vilitokea. Mawimbi ya joto yanayovunja rekodi yameshuhudiwa nchini Uchina, Ulaya, Kaskazini na Amerika Kusini. Na ukame wa muda mrefu katika Pembe ya Afrika unatishia janga la kibinadamu,”  

 Ameongeza kuwa "Kuna haja ya kuimarisha utayari wa kukabiliana na matukio hayo makali na kuhakikisha kwamba tunafikia lengo la Umoja wa Mataifa la tahadhari ya mapema kwa wote katika miaka mitano ijayo,"  

Mkaa unaotokana na miti unachangia katika uharibifu wa mazingira
FAO/Giulio Napolitano
Mkaa unaotokana na miti unachangia katika uharibifu wa mazingira

Kinachohitajika kufanywa 

Taarifa hiyo wa WMO inasisitiza kwamba tahadhari za mapema, kuongeza uwekezaji katika mfumo wa msingi wa uangalizi wa kimataifa na kujenga mnepo wa kuhimili hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi itakuwa miongoni mwa vipaumbele vya WMO mwaka 2023 mwaka ambao jumuiya ya WMO inaadhimisha miaka 150. 

WMO pia itachagiza njia mpya ya ufuatiliaji wa uzalishaji na vyanzo vya hewa ukaa, methane na nitrojeni oxide kwa kutumia mkakati wa kimataifa wa ufuatiliaji yaani Global Atmosphere Watch, satelaiti na modeli za uigaji.  

Profesa Taalas anasema “Hii inaruhusu ufahamu bora na muhimu wa tabia ya gesi chafuzi katika angahewa halisi. Kuna kwa mfano kutokuwa na uhakika mkubwa kuhusiana na nguvu ya mifereji ya hewa ukaa katika anga na vyanzo vya methane, ambayo itafuatiliwa vyema kwa mbinu mpya.” 

Uchafuzi wa hali ya hewa unaosababisha madhara ya kiafya kote ulimwenguni ikiwemo, New Delhi India
UN india
Uchafuzi wa hali ya hewa unaosababisha madhara ya kiafya kote ulimwenguni ikiwemo, New Delhi India

Viashiria vya hali ya Hewa 

Taarifa hiyo ya WMO imesema gesi za chafuzi ni moja tu ya viashiria vya hali ya hewa sasa katika viwango vilivyozingatiwa.  

Kiwango cha bahari, maudhui ya joto ya bahari na tindikal pia viko katika rekodi ya juu inayoshuhudiwa.  

Kiwango cha kupanda kwa kina cha bahari kimeongezeka mara mbili tangu 1993 kwa mujibu wa shirika hilo.  

“Kimeongezeka kwa karibu milimita 10 tangu Januari 2020 hadi rekodi mpya ya juu mwaka huu. Miaka miwili na nusu iliyopita pekee imechangia asilimia 10 ya kupanda kwa jumla kwa kina cha bahari tangu vipimo vya satelaiti kuanza kutumika karibu miaka 30 iliyopita, “kulingana na ripoti ya WMO ya hali ya hewa duniani mwaka 2022. 

2022 umeshuhudia athari mbaya ya barafu katika milima ya Alps ya Ulaya, na dalili za awali za kuyeyuka kwa barafu hiyo kulikovinja rekodi.  

Barafu ya Greenland ilipotea kwa kiasi kikubwa kwa mwaka wa 26 mfululizo na mvua ilinyesha badala ya theluji kwenye kilele cha mlima huo kwa mara ya kwanza mwezi Septemba. 

Tathmini mpya ya utawala wa kitaifa wa bahari na anga ya Marekani imeonyesha jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyochochea joto, mvua na dhoruba kwenye eneo la Arctic. 

Barafu ya mlima ambayo inapungua kwa sababu ya halijoto inayoongezeka na theluji kidogo katika Wilaya ya Kargil, India.
© UNICEF/Srikanth Kolari

Ingawa 2022 haujavunja rekodi ya joto lakini ulighubikwa na matukio 

Kwa mujibu wa taarifa ya WMO ingawa mwaka 2022 haukuvunja rekodi za joto duniani, kulikuwa na idadi ya rekodi za joto za kitaifa katika sehemu nyingi za dunia. 

Sehemu kubwa ya ulimwengu wa kaskazini ilikuwa na joto na kavu sana. 

Mfano India na Pakistan zimeshuhudia joto lililovunja rekodi mwezi Machi na Aprili.  

Uchina ilikuwa na wimbi kubwa la joto na la muda mrefu tangu rekodi za kitaifa kuanza na msimu wa joto wa pili kwa ukame kwenye historia ya rekodi.  

Sehemu kubwa za Ulaya zilighubikwa na vipindi vya mara kwa mara vya joto kali. Uingereza ilishuhudia rekodi mpya ya kitaifa tarehe 19 Julai, wakati halijoto ilipanda zaidi ya  nyuzi joto 40°C kwa mara ya kwanza.  

Hii iliambatana na ukame unaoendelea na unaosababisha uharibifu mkubwa na pia moto wa nyika. 

Katika Afrika Mashariki, mvua imekuwa chini ya wastani katika misimu minne mfululizo ya mvua, ambayo ni muda mrefu zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa muda wa miaka 40, na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu unaoathiri mamilioni ya watu, kuharibu kilimo na kuua mifugo, hasa nchini Ethiopia, Kenya na Somalia. 

Mito Chari na Logone imefurik huko N'Djamena Chad baada ya mvua kubwa iliyosababisha mafuriko
© UNICEF/Aldjim Banyo
Mito Chari na Logone imefurik huko N'Djamena Chad baada ya mvua kubwa iliyosababisha mafuriko

Mafuriko yasiyo ya kawaida 

Taarifa hiyo ya tathimini inasema mvua iliyovunja rekodi mwezi Julai na Agosti ilisababisha mafuriko makubwa nchini Pakistan.  

Kulikuwa na angalau vifo 1,700 na watu milioni 33 walioathirika na watu milioni 7.9 walikimbia makazi yao.  

Mafuriko hayo yalikuja kwa nguvu baada ya wimbi la joto kali mwezi Machi na Aprili nchini India na Pakistani. 

Eneo kubwa lililo katikati ya sehemu ya Kati-Kaskazini mwa Argentina, na pia kusini mwa Bolivia, Chile ya kati, na sehemu kubwa ya Paraguay na Uruguay, lilipitia viwango vya joto vilivyovunja rekodi wakati wa mawimbi ya joto mara mbili mfululizo mwishoni mwa mwezi Novemba na mapema Desemba 2022. Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa kimataifa katika mtandao wa World Weather Attribution umesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yalifanya msimu wa mapema wa joto kuwa karibu mara 60 zaidi.