Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia yaanza kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua inayolenga zaidi ya watoto milioni 15.5

Kampeni ya chanjo ya surua inayolenga watoto milioni 14 ilizinduliwa nchini Ethiopia. (Maktaba)
© UNICEF/Nahom Tesfaye
Kampeni ya chanjo ya surua inayolenga watoto milioni 14 ilizinduliwa nchini Ethiopia. (Maktaba)

Ethiopia yaanza kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua inayolenga zaidi ya watoto milioni 15.5

Afya

Taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, imeeleza kuwa Wizara ya Afya ya Serikali ya Shirikisho (MoH) la Ethiopia imezindua rasmi kampeni jumuishi ya chanjo ya surua nchini kote tangu tarehe 22 Desemba 2022 katika hafla iliyosimamiwa na Waziri wa Afya wa Jimbo Dkt Dereje Duguma katika Kituo cha Afya cha Siriti katika Mji Mdogo wa Akaki Kaliti huko Addis Ababa.

Uzinduzi huo wa kitaifa ulifanyika kwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wafadhili, wadau wa chanjo, viongozi wa dini na jumuiya na vyombo vya habari.

Waziri wa Nchi Dkt. Dereje Duguma aliwapongeza washirika wote waliounga mkono juhudi hizi na kuzitaka ofisi za afya za mikoa na wafanyakazi wa afya kutumia fursa hii kufanya kampeni ya chanjo yenye ufanisi na inayoenea na kuongeza kinga ya walengwa. Pia alitoa wito kwa wazazi na walezi wote kushiriki kikamilifu wakati wa kampeni jumuishi ya chanjo ya surua kwa kuwapatia watoto wao chanjo.

Shughuli jumuishi za chanjo ya ziada ya surua (SIAs) zinalenga watoto milioni 15.5 wenye umri wa miezi 9-59 kote nchini Ethiopia, ikiwa ni pamoja na watu ambao ni vigumu kuwafikia katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame na migogoro.

Huduma nyingine za kuokoa maisha zimeunganishwa na kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua, ikiwa ni pamoja na chanjo ya kawaida kwa watoto ambao hawajachanjwa au wale ambao hawajakamilisha dozi, huduma za lishe kwa watoto: uchunguzi wa utapiamlo uliokithiri, matone ya vitamini A, na dawa ya minyoo dhidi ya vimelea vya matumbo; utambuzi wa fistula ya uzazi kwa wanawake; utambuzi wa miguu ya watoto; na chanjo ya COVID-19.

Akizungumza kwa niaba ya wadau mwengine wa chanjo, Kaimu Mkuu wa Shirika la Chanjo la WHO Ethiopia, Dkt Paul Mainuka amesema, “ninaipongeza Wizara ya Afya ya Ethiopia kwa hatua iliyochukuliwa kupunguza hatari ya milipuko ya surua nchini na kuifanya milipuko inayoendelea kufikia mwisho, hivyo kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa na vifo vinavyoweza kuzuilika vinavyosababishwa na surua,” na kisha akasaongeza akisema, "pia ni jambo la kupongezwa kuwa kampeni hiyo imeunganishwa na afua zingine za kuokoa maisha kama vile chanjo ya COVID-19 na huduma za lishe."

Nchini Ethiopia, ugonjwa wa surua unasalia kuwa tatizo kubwa la kiafya huku milipuko kadhaa ikitokea katika maeneo tofauti ya nchi. Ili kukabiliana na hili, Ethiopia ilipitisha na kuanza kutekeleza mikakati muhimu ya kupunguza mzigo wa surua na kuelekea kutokomeza kupitia kuimarisha chanjo ya kawaida na SIAs, ufuatiliaji na udhibiti wa kesi.

WHO iliunga mkono kampeni hii kifedha na kiufundi na imetuma zaidi ya wataalam 100 kusaidia utekelezaji wa kampeni katika shughuli za kabla, ndani na baada ya kampeni, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa ubora wa utoaji wa huduma wakati wa kampeni.