Chonde chonde wasafiri pateni chanjo dhidi ya Surua- WHO

27 Juni 2019

Kufuatia ongezeko la hivi karibuni la visa vya ugonjwa wa surua katika maeneo mbalimbali duniani hata katika nchi zilizoendelea,  shirika la afya ulimwenguni limetoa angalizo hususan kwa wasafiri kupata upya chanjo dhidi ya ugonjwa huo iwapo hawana uhakika kama waliwahi kupatiwa au la.

WHO imetoa angalizo hilo leo kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi ikisema kuwa hivi sasa ugonjwa huo umesambaa  kwa kasi kwa watu ambao bado hawajapatiwa chanjo hiyo.

Shirika hilo limesema kwa watoto wadogo ambao hawajachanjwa dhidi ya Surua, wako hatarini zaidi kuambukizwa na kwamba mtu mwenye kinga ndogo hususan ambaye hakupatiwa chanjo mbili  dhidi ya Surua anaweza kuambukizwa.

Kwa mantiki hiyo WHO inasema ili kuepusha ugonjwa huo kusambaa kwenye mataifa mengine, wasafiri wote lazima wahakikishe wamepata chanjo mbili za Surua.

Halikadhalika, wasafiri wasio na uhakika kuhusu hali yao ya chanjo, angalau wapate dozi moja ya chanjo ya Surua, na chanjo hiyo ifanyike siuk 15 kabla ya safari.

Habari njema kwa mujibu wa WHO ni kwamba chanjo ya Surua inaweza kutolewa sambamba na chanjo wapatiwazo wasafiri kama ile ya homa ya manjano.

Kwa upande wa watoto wachanga wenye umri wa kuanzia miezi 6, WHO inapendekeza chanjo ya ziada ya Sura iwapo watoto hao wanaelekea nchi ambayo ina mlipuko wa Surua.

Watoto wenye umri wa kati ya miezi 6 hadi 9 ambao wanapata chanjo ya ziada ya Surua, wapatiwe pia dozi mbili za Surua ambazo zinapendekezwa kwa mujibu wa taratibu za chanjo za kitaifa,” imesema WHO.

Hata hivyo WHO imesema chanjo dhidi ya Surua haipaswi kupatiwa wanawake wajawazito.

Surua huambukizwa kwa njia ya kikohozi, chafya na magusano ya moja kwa moja na mgonjwa au kupitia majimaji ya pua au koo.

Virusi vya Surua husalia na uwezo wa kuambukiza vikiwa hewani au eneo la wazi kwa hadi saa mbili na virusi hivyo vinaweza kuambukizwa na mgonjwa kuanzia siku ya 4 kabla ya kuanza vipele na siku 4 baada ya vipele kusambaa.

Dalili za mwanzo za Surua ni homa kali inayoanza kati ya siku 10 hadi 12 baada ya kuambukizwa virusi, homa ambayo hudumu kwa kati ya siku 4 hadi 7.

Mafua, kikohozi, macho mekundu na vidoa vyeupe ndani ya mashavu vinaweza kutokea pia mwanzoni na baada ya siku kadhaa vipele huibuka usoni na sehemu ya juu ya mashavu.

Surua huweza kusababisha kifo na pia kutokuona, ubongo kujaa maji na kuhara.

TAGS: Surua, WHO, wasafiri

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud