Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zambia: FISH4ACP kusaidia uvuvi endelevu wa dagaa Kapenta na samaki buka

Wavuvi ziwa Tanganyika wkikagua mavuno.
UN News/Devotha Songorwa
Wavuvi ziwa Tanganyika wkikagua mavuno.

Zambia: FISH4ACP kusaidia uvuvi endelevu wa dagaa Kapenta na samaki buka

Ukuaji wa Kiuchumi

Mpulungu, eneo la kaskazini mwa Zambia. Kusini mwa Ziwa Tanganyika. Hapa mitumbi na boti za wavuvi zinasafiri hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Tanzania na Burundi. Ziwa refu zaidi duniani lenye maji baridi linazigusa nchi zote hizo nne, sio tu kijografia, bali pia kwa ustawi wa watu.

“Ninamiliki nyavu na mitumbwi mitatu. Ninavua kapenta na buka.” Huyo ni Davis Sikamba, Mvuvi katika Ziwa Tanganyika upande wa Zambia. Anaposema kapenta anazungumzia dagaa ambao katika nchi jirani ya Tanzania wanaita Dagaa Kigoma, na anaposema buka, ni samaki ambao majirani zao Tanzania wanaita Migebuka.

Anaendelea kueleza kuwa, “kuna uhitaji mkubwa dagaa hao aina ya kapenta na samaki buka.”

Mmoja wa wachuuzi wa dagaa na samaki ni huyu Catherine Kalyati, yeye pia ni mchakataji kwani anaanza na hatua ya kwanza kama anavyoeleza,.

“Ninaagiza kapenta kutoka kwa wavuvi. Tunapoamka asubuhi tunaandaa vifaa ambavyo tutaenda navyo maloni. Huko tunasubiri wavuvi wanaporejea tunapima samaki tunaenda kukausha. Ushiriki mkubwa wa wanawake katika biashara ya dagaa ni kununua, kukausha na kuuza.Watu wa Zambia wanapenda kula dagaa hawa Kapenta, wengi tunawapata kutoka DRC na Tanzania na hata humu humu Zambia. Dagaa wote wanaenda kwenye soko la Mpulungu ambako kila kitu kinauzwa.”

Bila kuelimisha wavuvi kuhusu uvuvi endelevu, huenda Catherine na wenzake wakakosa kipato na lishe kwani kama anavyoeleza Mvuvi Davis Sikamba ambaye amejitambulisha awali kuwa anamiliki mitumbwi mitatu ya uvuvi…siku hizi baadhi ya wavuvi wenzake wanavua samaki wengi w umri mdogo sana. Na kwa hivyo wakiendelea hivyo, basi wavuvi kama yeye ambao wanasubiri samaki wafikie umri unaofaa, watakasoma samaki.

Hali anayoisema mvuvi huyu inathibitishwa na mchakataji mchuuzi, Catherine ambaye anadai kwamba, biashara ya dagaa siku hizi si yenye faida kubwa kama ilivyokuwa awali,

“Hakuna nyavu za viwango vya ukubwa wa dagaa hawa kapenta na wavuvi wanavua hadi vitoto ambavyo bado vinahitaji kukua.”

Mfanyabiashara huyu anataja tatizo jingine akisema wakati wa msimu wa mvua wanakabiliana na changamoto kubwa. Jua halitokei mara nyingi dagaa wanaharibika na kwa hivyo anasema kwamba wangependa kutafuna namna nyingine ya kukausha dagaa.

Hapo bila shaka ndipo unapoingia Mradi wa FISH4ACP ambao ni mkakati wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kwa kushirikiana na  Muungano wa Afrika, AU na ule wa nchi za Karibea na Pasifiki OACPS, kuhakikisha minyororo ya thamani ya uvuvi na ufugaji wa samaki barani Afrika, Karibea na Pasifiki kuwa endelevu zaidi.