Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yakatili maisha ya zaidi ya watu 120 DRC, Guterres atoa pole

Vijiji kadhaa na maeneo ya ukulima yalifurika wakati mvua kubwa iliposababisha Mto Mutahyo kufurika mjini Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Sibylle Desjardins
Vijiji kadhaa na maeneo ya ukulima yalifurika wakati mvua kubwa iliposababisha Mto Mutahyo kufurika mjini Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mafuriko yakatili maisha ya zaidi ya watu 120 DRC, Guterres atoa pole

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ameshtushwa na idadi ya watu waliopoteza maisha na uharibu mkubwa uliosababishwa na mafuriko makubwa kuwahi kulikumba nchini Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo DRC, tangu mwaka 2019. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York Marekani Antonio Guterres amesema “Mvua kubwa zinazonyesha na kusababisha mafuriko mjini Kinshasa na katika baadhi ya majimbo ya DRC yamesambaratisha nyumba na mashamba, pamoja na shule na miundombinu mingine ya umma.” 

Kwa mujibu wa duru za habari zaidi ya watu 120 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na mafuriko hayo yaliyoambatana na maporomoko ya udongo na kujeruhi wengine wengi. 

Hali hiyo imemfanya Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi aliyekuwa ziarani Marekani kwa ajili ya mkutano baina ya Marekani na Muungano wa Afrika AU kukatisha ziara na kurejea nyumbani ambako kumetangzwa siku tatu za maombolezo kwa ajili ya waliopoteza maisha. 

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika , serikali  na watu wote wa DRC huku akiwatakia ahuweni ya haraka majeruhi. 

Amesisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unaonyesha mshikamano na DRC ukisaidia hatua za kukabiliana na hali hiyo. 

Duru zinasema mji wa Kishasa wenye wakati wapatao milioni 15 umeathirika sana huku nyumba, barabara na miundombinu mingine ikifunikwa na maji.