Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huu ni ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miaka 40, Mamilioni ya Waethiopia hatarini:UN

UN Ethiopia/Getachew Dibaba
Takriban mifugo milioni moja wamekufa kutokana na ukame katika eneo la Somali nchini Ethiopia.
UN Ethiopia/Getachew Dibaba

Huu ni ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miaka 40, Mamilioni ya Waethiopia hatarini:UN

Tabianchi na mazingira

Jimbo la Somali lilioko Mashariki mwa Ethiopia limekumbwa na misimu mitatu ya kiwango kidogo cha mvua kilicho chini ya wastani, hali ambayo inazidisha madhila  ya kibinadamu kwa watu wapatao milioni 3.5, ambao ni zaidi ya nusu ya wakazi wa eneo hilo ambao tayari walikuwa katika shida.

Kwa sababu ya ukame, Zeineba, mwenye umri wa miaka 60, alilazimika kuingia katika uamuzi mgumu zaidi wa maisha yake, wa kuacha makazi yake na kuhamia kijiji kingine, ili kuokoa maisha yake na ya familia yake.

"Mifugo yangu iliangamia kwa kukosa maji na malisho, na haikuweza kustahimili ukame mkali tena. Inatia uchungu sana,” analalamika Zeineba.

Katika jimbo la Somali, kama ilivyo katika maeneo mengine ya wafugaji, mifugo ni njia muhimu ya kuweza kuishi kwa watu wengi, na ufunguo wa kuzalisha mapato katika masoko ya ndani.

Umoja wa Mataifa unasema mamilioni ya watu kama Zeineba wamepoteza uwezo wa kujikimu kimaisha, na kulazimika kuhamia mahali ambapo wanaweza kupokea msaada wa kibinadamu kutoka kwa jamii zinazowapokea, serikali au mashirika ya kibinadamu.

Hali ilipozidi kuwa mbaya kijijini kwao, Zeineba alianza kutembea kwa miguu na watoto wake saba. Iliwachukua siku saba kufika kwenye kituo cha Higlo cha misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wakimbizi wa ndani (IDPs).

Zeineba akiwa na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu Ethiopia Dkt. Catherine Sozi.
UN Ethiopia/Getachew Dibaba
Zeineba akiwa na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu Ethiopia Dkt. Catherine Sozi.

Hali ni mbaya

"Huu ni ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka arobaini," anasema Rais wa jimbo la Somali, Mustafe Mohammed Omer. "Serikali ilichukua hatua kwa wakati kuhusu athari za ukame kwa kutoa msaada wa kibinadamu.

Pia tutaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza athari za ukame kwa watu.

"Lakini hali ni mbaya", anaendelea Bw. Omar. "Kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka kunahitaji rasilimali nyingi. Kuweka rasilimali zote za kanda katika kukabiliana na ukame pia kutaharibu mipango mikubwa inayoendelea ya maendeleo ambayo ina athari za muda mrefu na za kuleta mabadiliko kwa jamii zetu”.

Kulingana na taarifa za hivi karibuni kuhusu ukame zilizotolewa na ofisi ya Bwana Omar, wastani wa mifugo milioni moja pia imekufa katika maeneo 10 yaliyoathiriwa zaidi na ukame katika jimbo la Somali.

Mifugo katika ukanda huu wote wako katika hali mbaya kiafya, na wengi zaidi wanatarajiwa kuangamia kutokana na ongezeko la magonjwa katika msimu ujao wa mvua.

Kampeni za chanjo na malisho ya mifugo ili kuokoa kizazi cha mifugo hiyo  zinahitajika haraka.

Wakimbizi wa ndani katika eneo la Shabelle, Somali Ethiopia.
UN Ethiopia/Getachew Dibaba
Wakimbizi wa ndani katika eneo la Shabelle, Somali Ethiopia.

Maandalizi ya mafuriko na ukame

Wakati huohuo Umoja wa Mataifa na washirika walioko katika eneo hilo wanazisaidia familia zilizoathirika kwa chakula , maji, lishe, malazi na vifaa vingine visivyo vya chakula.

“Maandalizi ya kuwezesha na kusaidia kwa wakati kutokana na hali ya kibinadamu inayoendelea, kujenga mnepo   na kuhimili janga la mabadiliko ya tabianchi ni muhimu katika kupunguza athari za ukame kwa mamilioni ya watu kwenye jimbo hilo” amesema Catherine Sozi, the mratibu mkazi na wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia.

Ameongeza kuwa mafuriko yanaweza kutokea katika msimu ujao wa mvua hali ambayo itahitaji uratibu na rasilimali za kutosha kuweza kuzilinda jamii ambazo tayari zimeathirika vibaya na ukame.

Ufadhili mpya unahitakjika haraka kushughulikia mahitaji yanayoongezeka ya watu walioathirika ikiwemo wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahoifadhi.

Umoja wa Mataifa unasaidia mipango ya juhudi za muda mrefu za serikali na jamii ili kujiandaa vyema kukabiliana na ukame na hatari zingine katika siku za usoni.

Na unafanyakazi kuboresha uratibu baina ya vyombo vya kikanda vya masuala ya kibinadamu.