Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yaongeza kasi ya operesheni za kibinadamu Kaskazini mwa Ethiopia

Msafara wa malori ya WFP yakipeleka chakula na lishe kwa Adi Harush, Mai Aini, Mekelle na Shire huko Tigray, Ethiopia.
WFP Ethiopia
Msafara wa malori ya WFP yakipeleka chakula na lishe kwa Adi Harush, Mai Aini, Mekelle na Shire huko Tigray, Ethiopia.

WFP yaongeza kasi ya operesheni za kibinadamu Kaskazini mwa Ethiopia

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo mjini Addis Ababa, Ethiopia, limesema limekabidhi zaidi ya tani 2,400 za chakula, matibabu, lishe na vifaa vingine vya kuokoa maisha katika eneo la Tigray nchini Ethiopia kufuatia kusainiwa kwa makubaliano ya amani mapema mwezi huu na kufunguliwa tena kwa shoroba zote nne za barabara. 

Hata hivyo, WFP inaeleza kuwa uwasilishaji wa msaada ndani ya Tigray haulingani na mahitaji ya WFP na wadau wake wanaoshirikiana katika zoezi hilo kwani wanahitaji haraka kufikia maeneo yote ya kanda ili kupeleka msaada wa chakula na lishe kwa watu milioni 2.3 walio katika mazingira magumu. 

Hali ilivyo katika maeneo yote ya vita na ukame nchini Ethiopia: 

Malori 96 yamesafirisha zaidi ya tani 2,400 za chakula - zinazotosha kulisha takriban watu 170,000 - na lita 100,000 za mafuta hadi Tigray tangu Novemba 15 wakati WFP iliporejelea operesheni kwa kutumia shoroba zote nne za barabara zilizofunguliwa tena. 

Kundi la uratibu linaloongozwa na WFP limewezesha usafirishaji wa tani 250 za mizigo ya kibinadamu hadi Tigray kutoka Gondar, Kombolcha na Semera kwa wadau wanane wanaoshirikiana, ikiwa ni pamoja na vifaa vya matibabu kwa njia ya anga. 

Kwa mara ya kwanza kabisa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma ya Kibinadamu ya Anga (UNHAS) linaendesha zamu ya ndege kusafirisha abiria na mizigo ya kibinadamu katika uwanja wa ndege wa Shire huko Tigray. WFP imetuma mzigo wa kwanza kwa ndege ya abiria ya UNHAS kwenda Mekelle tangu mwisho wa Agosti, baada ya kupokea kibali cha shirikisho (Ethiopia) kwa safari za ndege za abiria kuanza tena Mekelle.Safari za kawaida za UNHAS kwenda Mekelle lazima ziendelee. 

“Licha ya ufikiaji mpya wa kibinadamu kupitia Amhara katika wilaya katika ukanda wa kaskazini-magharibi na kusini mwa Tigray, ufikiaji katika baadhi ya maeneo ya mashariki na kati ya Tigray unabakia kuwa na kikwazo - na kuathiri hadi akina mama na watoto 170,000 wanaohitaji msaada wa chakula.” Inafafanua WFP. 

Chakula kinasambazwa kwa watu 450,000 kaskazini mwa Ethiopia walioathiriwa na mzozo.
© WFP/Sinisa Marolt
Chakula kinasambazwa kwa watu 450,000 kaskazini mwa Ethiopia walioathiriwa na mzozo.

WFP tayari imepeleka chakula kwa zaidi ya watu 100,000 huko Mai Tsebri katika ukanda wa kaskazini-magharibi na Alamata katika ukanda wa kusini tangu barabara za Tigray kufunguliwa tena. WFP pia ilifikia watu 540,000 huko Mekelle mapema Novemba. Tangu mwanzoni mwa Novemba, WFP imefikia asilimia 29 ya watu milioni 2.1 wanaopata msaada wa chakula katika eneo la Tigray. 

WFP pia inaeleza kuwa, “inaendelea kutoa msaada wa chakula katika mikoa jirani ya Afar na Amhara. Huko Afar, WFP imepeleka msaada wa chakula kwa watu 650,000 mara tatu mwaka huu.” Duru ya nne inaendelea hivi sasa na watu 180,000 (asilimia 27 ya watu waliolengwa) wamefikiwa hadi sasa. Huko Amhara, WFP kwa sasa inapeleka msaada wa chakula kwa watu 675,000 kwa mara ya nne mwaka huu na watu 611,000 (asilimia 90 ya watu waliolengwa) wamefikiwa hadi sasa. 

Kaskazini mwa Ethiopia, mzozo wa miaka miwili umesababisha zaidi ya watu milioni 13.6 kuhitaji msaada wa chakula cha kibinadamu. Tathmini ya hivi karibuni ya WFP ya Dharura ya Usalama wa Chakula kuhusu hali ya Tigray, iliyochapishwa mwezi Agosti, iligundua watu milioni 5.4 - asilimia 90 ya eneo hilo - wanaohitaji msaada wa chakula. Familia huko Amhara na Afar pia zimeathirika ambapo watu milioni 7 na milioni 1.2 mtawalia wanahitaji msaada wa chakula. 

Kote Ethiopia kwa ujumla, watu milioni 22 wanahitaji msaada wa chakula ambao ni pamoja na watu milioni 9.8 katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame kusini na kusini mashariki mwa nchi hiyo, ambapo misimu minne ya mvua iliyoshindwa mfululizo imesababisha upungufu wa mazao, mamilioni ya vifo vya mifugo na watoto milioni 2.2 wakiwa na utapiamlo mkali. WFP inawafikia watu milioni 2.8 walioathiriwa na ukame katika eneo la Somalia kila baada ya wiki sita kwa msaada wa dharura wa chakula, fedha taslimu na lishe na pia inasaidia zaidi ya wafugaji 85,000 wa kilimo ili kujenga uwezo wao wa kustahimili majanga ya tabianchi siku zijazo. 

Ufadhili wa ziada lazima upatikane ili kusaidia mahitaji ya haraka na ya muda mrefu ya watu walioathiriwa na migogoro na majanga ya hali ya hewa. WFP inalenga kufikia zaidi ya watu milioni 11 nchini Ethiopia kwa msaada wa kibinadamu katika kipindi cha miezi sita ijayo lakini inasema inakabiliwa na upungufu wa ufadhili wa dola za Marekani milioni 422.