Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya amani Ethiopia ni muhimu kumaliza janga linaloendelea- UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa AntónioGuterres akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani kuhusu Ethiopia.
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa AntónioGuterres akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani kuhusu Ethiopia.

Mazungumzo ya amani Ethiopia ni muhimu kumaliza janga linaloendelea- UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani leo na kusema suala la kurejeshwa haraka kwa mazungumzo ya amani nchini Ethiopia ni suala la dharura ili hatimaye mgogoro unaoendelea uweze kupata suluhu ya kisiasa na ya kudumu.

Guterres amesema udharura hauna ubishi kwa kuzingatia hali ya usalama Ethiopia inaelekea kushindwa kudhibitiwa, ghasia na uharibifu umefikia viwango vya kutisha huku utangamano wa kijamii ukizidi kumomonyoka.

Vikosi vya Eritrea viondoke Ethiopia

Mathalani amesema chuki kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia zinasambaa hivyo ametaka zikome mara moja ikiwemo kuondoka kwa haraka kwa vikosi vya kijeshi vya Eritrea nchini Ethiopia.

“Hakuna suluhu ya kijeshi, jamii ya kimataifa lazima ishirikiane kurejesha amani Ethiopia,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa mashambulizi yanafanyika bila kuchagua maeneo, ikiwemo maeneo ya makazi, yakisababisha vifo vya watu wengi zaidi wasio na hatia kila uchao huku miundombinu muhimu ikiharibiwa na hivyo kukwmaisha wananchi kupata huduma za msingi.

Mama aliyefurushwa akiipikia familia yake huko Afar, Ethiopia.
© WFP/Claire Nevill
Mama aliyefurushwa akiipikia familia yake huko Afar, Ethiopia.

Mashambulizi yameshamiri tangu mwezi Agosti mwaka huu na kusababisha maelfu ya watu kukimbia makwao.

Sasa Katibu Mkuu anarejelea tena wito wake kwa pande kinzani kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu inayotaka raia walindwe, halikadhalika watoa huduma za kibinadamu ambao wanashambuliwa na hata kuuawa wakati wakisambaza misaada ya kibinadamu.

Mahitaji ya kibinadamu ni makubwa

Kwa mujibu wa Guterres, hata kabla ya kuanza upya kwa mapigano mwezi Agosti mwaka huu, tayari watu milioni 13 walikuwa wanahitaji msaada wa kibinadamu kwenye majimbo ya Afar, Tigray na Amhara.

Upelekaji misaada huko Tigray umekwama kwa zaidi  ya wiki 7 ilhali huko Amhara na Afar usambazaji umevurugika.

Wakati akisema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia harakati za Muungano wa Afrika wa kumaliza jinamizi la mzozo Ethiopia kwa nji ya haraka iwezekanayo, Katibu Mkuu amesihi pande kinzani kuruhusu upelekaji wa misaada ya kibinadamu.