Hakuna chakula, hakuna mafuta, hakuna ufadhili: Operesheni za WFP kaskazini mwa Ethiopia zimekwama 

14 Januari 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP leo limeonya kwamba shughuli zake za kuokoa maisha kupitia chakula kaskazini mwa Ethiopia zinakaribia kusitishwa kwa sababu mapigano makali yamezuia upitishaji wa mafuta na chakula. 

Taarifa ya WFP iliyotolewa hii leo katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa inasema kuongezeka kwa mzozo kaskazini mwa Ethiopia kunamaanisha kuwa hakuna msafara wa WFP ambao umefika Mekelle tangu katikati ya Desemba. Akiba ya chakula kilichoimarishwa na lishe kwa ajili ya matibabu ya watoto na wanawake wenye utapiamlo sasa kimemalizika, na mzigo wa  mwisho wa nafaka, kunde na mafuta ya WFP utasambazwa wiki ijayo. 

Michael Dunford, Mkurugenzi wa WFP wa Kanda ya Afrika Mashariki amesema sasa ilipofikia inawabidi kuchagua, “nani abaki na njaa ili kuzuia mwingine asife njaa. Tunahitaji uhakikisho wa mara moja kutoka kwa wahusika wote kwenye mzozo uwepo wa njia salama kote kaskazini mwa Ethiopia. Misaada ya kibinadamu haitiririki kwa kasi na kiwango kinachohitajika. Ukosefu wa vyakula na mafuta unamaanisha kuwa tumeweza tu kufikia asilimia 20 ya zile tunazopaswa kuwa nazo katika usambazaji huu wa hivi kariuni zaidi katika Tigray. Tuko kwenye ukingo wa janga la kibinadamu."  

Zaidi ya mwaka mmoja katika mzozo kaskazini mwa Ethiopia, takriban watu milioni 9.4 wanahitaji msaada wa chakula cha kibinadamu. Hili ni ongezeko la watu milioni 2.7 kutoka miezi minne iliyopita. Wakati huo huo, kwa sababu ya mapigano, ugawaji wa chakula uko chini sana. 

WFP inapanga kuwafikia watu milioni 2.1 kwa msaada wa chakula huko Tigray; 650,000 katika Amhara; na 534,000 katika Mkoa wa Afar. 

Shirika hilo pia linaonya kuwa huenda ikakosa chakula na lishe kwa mamilioni ya watu kote nchini Ethiopia kuanzia mwezi ujao kutokana na ukosefu wa fedha ambao haujawahi kushuhudiwa. WFP inataka dola za Kimarekani milioni 337 zaidi kuwasilisha msaada wa dharura wa chakula Kaskazini mwa Ethiopia na dola milioni 170 kufikia wale walioathiriwa na ukame mkali katika eneo la Somali katika kipindi cha miezi sita ijayo. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter