Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya lazima iwe kitovu katika majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi COP27: WHO

Mwanamke akijarivu kuvuka maji ya mafuriko mjini Jakusko jimbo la Yobe Nigeria
© WFP/Arete/Ozavogu Abdul
Mwanamke akijarivu kuvuka maji ya mafuriko mjini Jakusko jimbo la Yobe Nigeria

Afya lazima iwe kitovu katika majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi COP27: WHO

Tabianchi na mazingira

Katika mkesha wa mazungumzo muhimu ya mabadiliko ya tabianchi COP27, yanayoanza kesho huko Sharm-el Sheikh nchini Misri, shirika la afya la Umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO, limekumbusha kwamba mzozo wa mabadiliko ya tabianchi unaendelea kuwafanya watu kuwa wagonjwa na kuhatarisha maisha na kwamba afya lazima iwe msingi wa mazungumzo haya muhimu.

WHO inaamini kuwa mkutano huo lazima umalizike kwa mafanikio katika malengo manne muhimu ambayo ni “kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga mnepo dhidi ya hali hiyo, ufadhili na ushirikiano ili kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi ipasavyo.”

Shitrika hilo linasema COP27 itakuwa fursa muhimu kwa ulimwengu kuja pamoja na kujitolea tena kuhuisha lengo la makubaliano ya Paris la la kuhakikisha kiwango cha joto kinasalia kuwa nyuzi joto 1.5 °C.

Shirika hilo limeendelea kusema kwamba “Tunawakaribisha waandishi wa habari na washiriki wa COP27 kujiunga na WHO katika mfululizo wa matukio ya ngazi ya juu na kutumia muda katika nafasi ya ubunifu kwenye banda la afya. Lengo letu litakuwa ni kuweka tishio la kiafya linalotokana na janga la mabadiliko ya tabianchi na hatua za kulidhibiti kuwa katikati ya majadiliano. Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri afya ya watu na yataendelea kufanya hivyo kwa kasi zaidi kama hatua za haraka hazitochukuliwa.”

Picha iliyopigwa toka angani ikionyesha theluji katika mlima Kilimanjari ikiyayuka sababu na mabadiliko ya tabianchi
UN Photo/Mark Garten
Picha iliyopigwa toka angani ikionyesha theluji katika mlima Kilimanjari ikiyayuka sababu na mabadiliko ya tabianchi

Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri afya za wengi

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhamon Ghebreyesus amesema "Mabadiliko ya tabianchi yanafanya mamilioni ya watu kuwa wagonjwa au kuwa katika hatari zaidi ya magonjwa duniani kote na uharibifu unaoongezeka wa matukio ya hali ya hewa huathiri vibaya jamii maskini na zilizotengwa. Ni muhimu kwamba viongozi na watoa maamuzi wanaokutana katika COP27  kuweka afya katika kiini cha mazungumzo."

Ameongeza kuwa “Afya yetu inategemea afya ya mifumo ya ikolojia inayotuzunguka, na mifumo ya ikolojia hii sasa iko chini ya tishio la ukataji miti, kilimo na mabadiliko mengine katika matumizi ya ardhi na maendeleo ya haraka ya ukuaji wa mijini.”

Ameendelea kusema kuwa uvamizi unaoendelea zaidi katika makazi ya wanyama unaongeza fursa kwa virusi hatari kwa wanadamu kufanya mabadiliko kutoka kwa wanyama wao. 

Kati ya mwaka 2030 na 2050, mabadiliko ya tabianchi yanatarajiwa kusababisha takriban vifo 250,000 vya ziada kwa mwaka kutokana na utapiamlo, malaria, kuhara na shinikizo la joto kali.

Pia amesema gharama za uharibifu wa moja kwa moja kwa afya yaani, bila kujumuisha gharama katika sekta zinazoamua mustakbali wa afya kama vile kilimo na maji na usafi wa mazingira, inakadiriwa kuwa kati ya dola bilioni 2-4 kwa mwaka ifikapo 2030.

Maji yakiwa ziwa yakiwa yamefurika katika wilaya ya Kousseri katika jimbo la Far kaskazini mwa Cameroon
© UNHCR/Moise Amedje Peladai
Maji yakiwa ziwa yakiwa yamefurika katika wilaya ya Kousseri katika jimbo la Far kaskazini mwa Cameroon

Afya ya watu iko hatarini 

Kwa mujibu wa WHO ongezeko la halijoto duniani ambalo tayari limetokea linasababisha hali mbaya ya hewa ambayo huleta joto kali na ukame, mafuriko makubwa na vimbunga vinavyozidi kuwa na nguvu na pia dhoruba za kitropiki. Mchanganyiko wa mambo haya inamaanisha athari kwa afya ya binadamu inaongezeka na kuna uwezekano wa kuharakisha athari hizo.

“Lakini kuna nafasi ya matumaini, haswa ikiwa serikali zitachukua hatua sasa kuheshimu ahadi zilizotolewa huko Glasgow mwezi Novemba 2021 na kwenda mbali zaidi katika kutatua mzozo wa mabadiliko ya tabianchi”.

WHO inatoa wito kwa serikali kuongoza awamu ya haki, ya usawa na ya haraka kutoka kwa nishati ya mafuta kisukuku na kuingia kwenye mpito kwa siku zijazo kuhamia kwenye nishati safi. 

Pia kumekuwa na maendeleo ya kutia moyo juu ya ahadi za utokomezaji wa hewa ukaa na WHO inataka kuundwa kwa mkataba wa kutoeneza mafuta kisukuku ambayo yanasababisha makaa ya mawe na nishati nyingine zenye madhara kwa anga ili ziondolewe kwa njia ya haki na usawa. 

Hii ingewakilisha mojawapo ya michango muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Shirika hilo la afya ulimwenguni limesisitiza kwamba “Uboreshaji wa afya ya binadamu ni jambo ambalo raia wote wanaweza kuchangia, iwe kupitia kukuza maeneo ya kijani kibichi zaidi ya mijini, ambayo huwezesha kukabiliana na hali ya hewa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huku ikipunguza kasi ya uchafuzi wa hewa, au kampeni ya kuounguza misururu ya magari barabarani na uboreshaji wa mifumo ya usafiri wa ndani. Ushirikishwaji wa jamii na ushiriki katika vit dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni muhimu ili kujenga uwezo wa kustahimili na kuimarisha mifumo ya chakula na afya, na hii ni muhimu sana kwa jamii zilizo hatarini na nchi zinazoendelea za visiwa vidogo (SIDS), ambazo zinabeba mzigo mkubwa wa matukio mabaya ya hali ya hewa.”

Taarifa imeendelea kusema kwamba watu milioni 31 katika eneo kubwa la Pembe ya Afrika wanakabiliwa na njaa kali na watoto milioni 11 wanakabiliwa na utapiamlo wakati eneo hilo likikabiliwa na ukame mbaya zaidi katika miongo ya hivi karibuni. 

Mabadiliko ya tabianchi tayari yana athari kwa uhakika wa chakula na ikiwa hali ya sasa itaendelea, mambo yatakuwa mabaya zaidi. 

Mfano mafuriko nchini Pakistan ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi na yameharibu maeneo mengi ya nchi hiyo.

Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari ya moto wa nyika
Unsplash/Matt Palmer
Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari ya moto wa nyika

Athari zitadumu muda mrefu sana

Who inasema athari zitaendelea kuonekana kwa miaka mingi ijayo. Zaidi ya watu milioni 33 wameathiriwa na karibu vituo vya afya 1500 vimeharibiwa.

Lakini hata jumuiya na maeneo ambayo hayafahamu sana hali mbaya ya mabadiliko ya tabianchi lazima yaongeze uwezo wao wa kuwa na mnepo, kama tulivyoona katika mafuriko na mawimbi ya joto hivi karibuni katika eneo la Ulaya ya kati. 

WHO inahimiza kila mtu kufanya kazi na viongozi wao wa ndani kuhusu masuala haya na kuchukua hatua katika jamii zao.

Sera ya mabadiliko ya tabianchi sasa lazima iweke afya katika kitovu na kukuza sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambazo zitaleta manufaa ya kiafya kwa wakati mmoja. 

Sera ya mabadiliko ya tabianchi inayozingatia afya ingesaidia kuhakikisha kunakuwa na sayari ambayo ina hewa safi, maji safi na uhakika wa chakula na chenye usalama zaidi, mifumo bora zaidi ya afya na ulinzi wa kijamii na, kwa sababu hiyo, watu wenye afya bora.

“Uwekezaji katika nishati safi utaleta faida za kiafya ambazo zitalipa uwekezaji huo mara mbili. Kuna hatua zilizothibitishwa zinazoweza kupunguza utoaji wa hewa chafuzi ambazo ni za muda mfupi, kwa mfano kutumia viwango vya juu zaidi vya uzalishaji wa magari, ambavyo vimehesabiwa kuokoa takriban maisha milioni 2.4 kwa mwaka, kupitia uboreshaji wa hali ya hewa na kupunguza ongezeko la joto duniani kwa takriban nyuzi joto 0.5 °C. ifikapo 2050.” limesema shirika hilo la afya duniani.

Pia gharama ya vyanzo vya nishati mbadala imepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka michache iliyopita, na nishati ya jua sasa ni nafuu zaidi kuliko makaa ya mawe au gesi katika nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani.