Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP27 yafungua pazia, ni ukurasa mpya wa kufanya mambo tofauti :UNFCCC

Simon Stiell mkuu wa UNFCCC akizungumza katika ufunguzi wa COP27
UN Japan/Momoko Sato
Simon Stiell mkuu wa UNFCCC akizungumza katika ufunguzi wa COP27

COP27 yafungua pazia, ni ukurasa mpya wa kufanya mambo tofauti :UNFCCC

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP27 umefungua pazia leo huko Sharm el-Sheik, Misri, na unapaswa kuuelekeza ulimwengu kwenye utekelezaji wa mipango iliyokubaliwa hapo awali ya kukabiliana na changamoto kubwa za ubinadamu, amesema wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Simon Stiell, katibu mtendaji mpya wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa (UNFCCC).

"Leo enzi mpya inaanza na tunaanza kufanya mambo kwa njia tofauti. Paris ilitupa makubaliano, Katowice na Glasgow walitupa mpango huo na Sharm el-Sheik inatuhamisha kwenye utekelezaji. Hakuna mtu anayeweza kuwa abiria tu katika safari hii. Hii ndiyo ishara kwamba nyakati zimebadilika,” Bwana Stiell amewaambia wajumbe waliokusanyika katika chumba kikuu cha mkutano huo kwenye kituo cha kimataifa cha mikutano cha Tonino Lamborghini.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi amesema viongozi wote wawe Marais, mawaziri wakuu au watendaji wakuu watawajibishwa kwa ahadi walizotoa mwaka jana huko Glasgow.

"Kwa sababu sera zetu, biashara zetu, miundombinu yetu, matendo yetu, yawe ya kibinafsi au ya umma, lazima yawiane na mkataba wa Paris na mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi", amesisitiza.

Mkataba wa UNFCCC ulianza kutumika tarehe 21 Machi 1994 ili kuzuia kuingiliwa na hatari kwa binadamu na mfumo wa hali ya hewa.

Leo hii mkataba huo ulioidhinishwa na nchi 198, una wanachama karibu wote. Mkataba wa Paris, uliokubaliwa mwaka wa 2016, unafanya kazi kama nyongeza ya mkataba huo.

Nje ya chumba na mkutano wa COP27 Sharm El-Sheikh.
UNFCCC/Kiara Worth
Nje ya chumba na mkutano wa COP27 Sharm El-Sheikh.

Timiza kile kilichoahidiwa

Akikubali hali tata ya sasa ya kisiasa na ya kijiografia, Bwana Stiell amesema kuwa COP27 ni fursa ya kuunda fursa salama ya kisiasa, inayolindwa dhidi ya chochote kinachoendelea huko nje, kufanya kazi na kuleta mabadiliko ya ulimwengu.

"Hapa Sharm el-Sheikh, tuna jukumu la kuharakisha juhudi zetu za kimataifa za kubadilisha maneno yetu kuwa vitendo", amesisitiza.

Katibu Mtendaji huyo wa UNFCCC amesisitiza hatua tatu muhimu za utekelezaji wa mkutano huo ambazo ni

1. Onyesha mabadiliko katika utekelezaji kwa kugeuza mazungumzo kuwa vitendo madhubuti.

2. Maendeleo thabiti kwenye mikondo muhimu ya kazi ya kupunguza, kurekebisha, fedha na muhimu zaidi kupunguza hasara na uharibifu.

3. Kuimarisha utoaji wa kanuni za uwazi na uwajibikaji katika mchakato mzima.

"Ninakaribisha mipango ya kina ya jinsi tunavyotekeleza kile tulichoahidi", amewaambia wajumbe waliokusanyika.

Uchimbaji wa mafuta ghafi ni moja ya visababishi vikubwa vya utoaji wa hewa chafuzi. Hii ni sehemu ya mafuta kisukuku ambayo Katibu Mkuu wa UN anataka jamii ya kimataifa iachane nayo.
© Unsplash/Zbynek Burival
Uchimbaji wa mafuta ghafi ni moja ya visababishi vikubwa vya utoaji wa hewa chafuzi. Hii ni sehemu ya mafuta kisukuku ambayo Katibu Mkuu wa UN anataka jamii ya kimataifa iachane nayo.

Hakuna kuruhusu kurudi nyuma

Bwana Stiell, akijinadi ka mkuu wa uwajibikaji, amesema kuwa nchi 29 sasa zimejitokeza na mipango iliyoimarishwa ya kitaifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi tangu COP26, ikiwa ni nchi tano zaidi tangu kuchapishwa kwa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya UNFCCC NDC ya wiki iliyopita, lakini bado si nchi nyingi.

"Kwa hiyo sasa niko hapa, naangalia nchi 170 ambazo zinapaswa kurejea na kuimarisha ahadi zao za kitaifa mwaka huu," amesema.

Amewakumbusha wajumbe kwamba mwaka jana mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Glasgow ulikubaliwa katika COP26, na alitarajia watimize ahadi zao.

"Shikilia ahadi zako na ongeza jitihada hapa Misri. Sitakuwa mlinzi wa kurudi nyuma,” amesema.

Mchakato uwe jumuishi

Kwa maneno ambayo yanaashiria shangwe katika chumba cha mkutano, mkuu huyo wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa wanawake na wasichana lazima wawekwe katikati ya maamuzi na hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

"Uwezeshaji wao unasababisha utawala bora na matokeo bora," amesema, pia akiangazia umuhimu wa mashirika ya kiraia na vijana katika mchakato wa COP27.

Watu wakiandamana Nürnberg ujerumani  kama sehemu ya mgomo kuhusu mabadiliko ya tabianchi
© Unsplash/Markus Spiske
Watu wakiandamana Nürnberg ujerumani kama sehemu ya mgomo kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Urais Mpya

Alok Sharma, Rais wa COP26 anayewakilisha Uingereza, alipitisha kijiti na mkutano kwa Rais mpya wa Misri, Sameh Shoukry, wakati wa kikao cha ufunguzi wa mkutano wa COP27.

Bwana Sharma ametathimini mafanikio yaliyopatikana Glasgow mwaka jana, kama vile kukamilisha kile kiitwacho kitabu cha sheria cha Paris, miongozo ya jinsi makubaliano hayo yanavyowasilishwa, kutekelezwa na kuweka ahadi kubwa zaidi za kifedha.

"Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema “mustakabali wetu wa pamoja wa muda mrefu hauko kwenye nishati ya kisukuku na ninakubaliana naye, kwa moyo wote", amesema.

Kulingana na Rais wa COP26, ikiwa ahadi zote zilizotolewa mwaka jana, ikiwa ni pamoja na ahadi za kutozalisha kabisa hewa ukaa, zingetekelezwa, dunia itakuwa katika njia muafaka ya kufikia nyuzi joto 1.7 ifikapo mwisho wa karne hii.

"Bado hatujafikia nyuzi joto 1.5C, lakini ni maendeleo," amesema, akitambua ukubwa wa changamoto ambayo dunia inakabiliana nayo.

Akirejea Bwana Stiell, amewataka viongozi kuchukua hatua, licha ya changamoto zilizopo za kijiografia.

"Pamoja na changamoto zote kama wakati wetu wa sasa, kutochukua hatua ni kosa kubwa na kunaweza tu kuahirisha janga la tabianchi, hivyo ni lazima tuwe na uwezo wa kuzingatia zaidi ya jambo moja kwa wakati mmoja", amehimiza.

Misri yahimiza utekelezaji

Rais wa COP27 Sameh Shoukry ametoa wito kwa wajumbe kuongeza azma na kuanza kutekeleza ahadi ambazo tayari zimetolewa.

"Kutoka kwenye mazungumzo na ahadi hadi enzi ya utekelezaji ni kipaumbele," amesema, baadaye akipongeza nchi ambazo tayari zimeshiriki mipango ya kitaifa ya mabadiliko ya tabianchi.

Bwana Shoukry ameongeza kuwa dola bilioni 100 zilizoahidiwa kuchangishwa na nchi zilizoendelea kwa nchi zinazoendelea zinapaswa kutolewa, na fedha lazima pia ziwe katikati ya majadiliano haya.

"Mazungumzo katika muda wa wiki mbili zijazo yatazaa matunda. Nawaomba nyote msikilize kwa makini na kujitolea kutekeleza na kugeuza ahadi za kisiasa kuwa makubaliano na maelewano na maandishi na maazimio ambayo sote tunaweza kuyatekeleza,” amesisitiza.

Pia ameonya kwamba "michezo isiyozalisha chochote haitakuwa na washindi" na kwamba matokeo ya mazungumzo yataathiri uwezo wa kuishi na maisha ya mamilioni ya watu duniani kote wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Hatuwezi kumudu uzembe au mapungufu yoyote, hatuwezi kutishia mustakabali wa vizazi vijavyo”, amesisitiza.

watoto wakipungia wakiwa kwenye maji ya mafuriko Palangka Raya katikati mwa Kalimantan, Indonesia.
© Greenpeace/Pram
watoto wakipungia wakiwa kwenye maji ya mafuriko Palangka Raya katikati mwa Kalimantan, Indonesia.

Hasara na uharibifu

Pia leo Jumapili, vipengele vya ajenda ambavyo vitajadiliwa kwa muda wa wiki mbili zijazo katika COP27 vilikubaliwa wakati wa utaratibu wa ufunguzi wa mkutano.

Hasara na uharibifu”, kipengele ambacho bado hakikuwa na uhakika mbele ya mkutano huo, hatimaye kiliingia katika ajenda baada ya kuwasilishwa na wapatanishi kutoka Kundi la G77 na Uchina ambalo kimsingi linajumuisha mataifa yote yanayoendelea na baada ya majadiliano ya kina kati ya nchi zinazoendelea na wanachama 194 wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi.

Amesema mabadiliko ya tabianchi, kupitia matukio mabaya ya hali ya hewa kama vile vimbunga vya kitropiki, hali ya jangwa na kupanda kwa kina cha bahari, husababisha uharibifu mkubwa kwa nchi.

Kwa sababu kukithiri kwa haya majanga ya asili kunasababishwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi chafuzi, hasa kutoka nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda, nchi zinazoendelea ambazo mara nyingi zimeathirika zaidi  zimekuwa zikibishana kwa muda mrefu kuwa zinapaswa kupokea fidia.

Suala la malipo haya, linalojulikana kama "hasara na uharibifu" sasa litakuwa mada kuu ya mjadala katika COP27.

Unataka kujua zaidi? Tazama ukurasa wetu wa matukio maalum, ambapo unaweza kupata habari zetu zote za mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi COP27, ukijumuisha hadithi na video, maelezo, na jarida letu la kila siku.