Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya vielelezo vya wakati wetu lakini pia ni moja ya vitisho vya kiafya duniani

Jua likizama katika eneo la mwambao wa ziwa Elton nchini Urusi
© UNESCO/A. Popov/Lake Elton Biosphere Reserve - Russian Federation
Jua likizama katika eneo la mwambao wa ziwa Elton nchini Urusi

Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya vielelezo vya wakati wetu lakini pia ni moja ya vitisho vya kiafya duniani

Tabianchi na mazingira

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus leo amewasihi viongozi wa wa dunia kuilinda afya dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema ndani ya kipindi cha chini ya wiki mbili zijazo ataungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na viongozi wengine wa dunia katika mkutano wa mabadiliko ya tabiachi kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

“Mkutano huu muhimu zaidi utaonesha ahadi kamili ambazo serikali zinafanya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na kupata na kuboresha afya na ustawi wa raia wao.” Ameeleza Dkt. Ghebreyesus

Mbili ya ahadi hizo zimeandaliwa na WHO na wadau wake. Ya kwanza ni kuhakikisha kuwa hewa inafikia viwango vya ubora vya WHO kufikia mwaka 2030. 

Ahadi ya pili ni kutoa rasilimali fedha kuwalinda watu dhidi ya matokeo mabaya ya kiafya yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Hii leo chini ya asilimia 0.5 ya ufadhili wa kimataifa kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi unaelekezwa kwenye afya, na nchi ambazo ziko hatarini zaidi hususani nchi za visiwa vidogo zinazoendelea, wanapokea sehemu ndogo tu ya kiasi hicho. Nchi zinaombwa kuongeza kiasi zaidi kuwalinda watu dhidi ya matokeo ya majanga ya tabianchi.” Anasisitiza Dkt. Ghebreyesus

Dkt. Ghebreyesus amesema zimesalia siku kumi na mbili kwa viongozi kutia saini ahadi hizo na hivyo akazisihi nchi nyingine ambazo hazijatoa ahadi kujiunga na wale ambao tayari wameahidi kuchukua hatua kuwalinda watu dhidi ya mawimbi ya joto kali, mafuriko na vimbunga vinavyohusishwa na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hatari ya utapiamlo, malaria, diarrhea na msongo utokanao na joto kali.

Mkutano wa tabianchi na mkutano wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu afya inafanyika siku moja.