Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Ethiopia na uongozi wa Tigray kwa makubaliano ya amani- Guterres

Wanawake na watoto wakisubiri msaada wa chakula kwenye eneo la mgao la Adimehamedey huko jimboni Tigray nchini Ethiopia.
© WFP/Claire Nevill
Wanawake na watoto wakisubiri msaada wa chakula kwenye eneo la mgao la Adimehamedey huko jimboni Tigray nchini Ethiopia.

Heko Ethiopia na uongozi wa Tigray kwa makubaliano ya amani- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza kutiwa saini kwa makubaliano kati ya serikali ya Ethiopia na Jeshi la ukombozi la Tigray, TPLF yenye lengo la kuleta amani ya kudumu kaskazini mwa taifa hilo lililogubikwa na vita tangu mwaka 2020.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Jumatano jioni jijiji New York, Marekani inamnukuu Katibu Mkuu akisema, “makubaliano haya ni hatua muhimu ya kwanza kuelekea kumaliza mapigano ya miaka miwili yaliyosababisha vifo na kutoweka kwa mbinu za kujipatia kipato kwa wananchi wengi wa Ethiopia.”

Wadau tumieni fursa ya makubaliano ya leo

Katibu Mkuu ametoa wito kwa wananchi wa Ethiopia na jamii ya kimataifa kuunga mkono hatua hiyo ya kijasiri iliyochukuliwa leo na serikali ya Ethiopia na uongozi wa jimbo la Tigray.

Ameahidi kutoa usaidizi kwa pande husika katika utekelezaji wa makubaliano hayo na “amewasihi waendelee na mazungumzo kwenye masuala ambayo bado hayajafikiwa ufumbuzi kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu ya kisiasa, kumaliza mapigano na kurejesha nchi kwenye mwelekeo wa amani na utulivu.”

Guterres pia ametoa wito kwa wadau wote kutumia fursa ya sasa ya kukoma kwa uhasama ili kuimarisha utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa rai ana wakati huo kurejesha huduma za umma ambazo zinahitajika kwa kiasi kikubwa.

Heko Muungano wa Afrika

Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo pia kupongeza Muungano wa Afrika, AU na jopo lake la ngazi ya juu likiongozwa na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, kwa kufanikisha mazungumzo kati ya serikali ya Ethiopia na viongozi wa Tigray, halikadhalika Afrika Kusini kwa kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.

“Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia hatua zinazofuatia za mchakato huo unaoongozwa na Muungano wa Afrika,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa wanaendelea kuhamasisha msaada unaohitajika zaidi ili kupunguza machungu kwenye maeneo yaliyoathirika na mzozo huo.