UN yakaribisha uteuzi wa wajumbe watatu AU kwa ajili ya kutatua mzozo wa Ethiopia 

21 Novemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amerkaribisha hatua ya jana Ijumaa ya Muungano wa Afrika AU, ya uteuzi wa wajumbe watatu wa ngazi ya juu ili kusaidia juhudi za kusaka suluhu ya amani ya mgogoro wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana. Guterres amempongeza mwenyekiti wa AU, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kwa jitihada zake na kuahidi uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa katika juhudi hizo. 

Pia mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa shukran zake kwa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwa kuwezesha mchakato huu wa amani. 

 Katibu Mkuu amerejea kusisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kuunga mkono juhudi za amani katika kuelekea kuhakikisha kwamba Ethiopia inakuwa taifa la amani, imara na leye mafanikio. 

 Mzozo kwenye jimbo la Tigray ulizuka mapema mwezi huu baada ya waziri mkuu Abiy Ahmed mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kuviamuru vikosi vya jeshi la serikali kuu kushambulia makao makuu ya jeshi la ukombozi la watu wa Tigray kwa madai kwamba vikosi hivyo vya upinzani vya Tigray vililishambulia jeshi la serikali.  

Kwa mujibu wa duru za mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, mzozo huo ambao bado unaendelea umeshakatili maisha ya watu wengi na wengine kwa mamia kujeruhiwa humu zaidi ya watu 200,000 wakifungasha virango  na kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya Tigray. 

Wakimbizi hao ambao wengi ni wanawake na watoto wanakimbilia katika nchi jirani ya Sudan. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter