Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaingiwa hofu na mwendelezo wa mapigano Tigray

Usambazaji wa msaada wa chakula na WFP katika jamii Ethiopia.
© WFP/Claire Nevill
Usambazaji wa msaada wa chakula na WFP katika jamii Ethiopia.

UN yaingiwa hofu na mwendelezo wa mapigano Tigray

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza wasiwasi wake mkubwa juu ya mwendelezo wa mapigano katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia, akisema mapigano hayo yana madhara makubwa kwa raia.

Guterres ameeleza hayo leo kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric jijini New York, Marekani.

Amesema mapigano hayo yanaathiri raia hasa katika kile ambacho tayari ni hali mbayá ya kibinadamu.

Ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa chuki baina ya pande zinazokinzana.

Ghasia za hivi karibuni

Mapigano yaliibuka tena mwezi Agosti mwaka huu baada ya kipindi cha makubaliano ya miezi mitano cha sitisho la mapigano ili kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Tigray waliokuwa hawajapata msaada kwa muda mrefu.

Harakati za usambazaji wa misaada zinakwamisha na ukosefu wa nishati ya mafuta, huku mawasiliano yakiwa yamekatwa Tigray yote, navyo vyombo vya habari vikieleza kuwa makamanda wa jeshi la Tigray wakidai kuwa Eritrea imezindua mashambulizi kuunga mkono vikosi vya serikali ya Ethiopia.

Mtoto akiwa amekaa katika gari lililo ungua moto huko Tigray Kaskazini mwa Ethiopia
© UNICEF/ Christine Nesbitt
Mtoto akiwa amekaa katika gari lililo ungua moto huko Tigray Kaskazini mwa Ethiopia

Raia na wahudumu wa kibinadamu wanauawa

Hali ya usalama si tete kwa raia pekee bali pia kwa watoa misaada ya kibinadamu ambapo Kamati ya Kimataifa ya Uokozi, IRC ambayo inashirikiana na Umoja wa Mataifa imeripoti leo kuwa mmoja wa watumishi wake aliuawa Ijumaa kwenye shambulio huko Tigray, wakati akisambaza misaada kwa wanawake na watoto kwenye mji wa Shire.

Mtumishi mwingine alijeruhiwa kwenye shambulio hilo huku raia watatu wakiuawa na watatu wakijreruhiwa kwenye shambulio la bomu.

IRC inasema watoa misaada yakibinadamu na raia hawapaswi kulengwa kwenye mashambulio.

Hadi sasa hakuna upande wowote uliokiri kuhusika kwenye shambulio hilo, ingawa Shire na maeneo mengine ya Tigray yameshuhudia msururu wa mashambulio kutoka angani tangu mwezi Agosti.

UN inaunga mkono harakati za AU

“Katibu Mkuu amesisitiza uungaji wake mkono wa mchakato wa usuluhishi unaoongozwa na Muungano wa Afrika, AU,” amenukuliwa Guterres katika taarifa hiyo.

Halikadhalika amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia urejeshaji wa haraka wa mazungumzo ili hatimaye kupata suluhu la kudumu la kisiasa kwenye mzozo huo unaozidi kuleta majanga kila uchao.