Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatari ya baa la njaa bado ni jinamizi linaloizonga Somalia: WFP Dunford

Michael Dunford, Mkurugenzi wa WFP Pembe ya Afrika akihojiwa na UN News.
UN/ Leah Mushi
Michael Dunford, Mkurugenzi wa WFP Pembe ya Afrika akihojiwa na UN News.

Hatari ya baa la njaa bado ni jinamizi linaloizonga Somalia: WFP Dunford

Msaada wa Kibinadamu

Ukame uliolighubika eneo la Pembe ya Afrika kwa miongo minne mfululizo umesababisha changamoto kubwa kwa mamilioni ya raia wa Kenya, Ethiopia na Somalia nchi ambayo maeneo mengi yanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na hatihati ya kutumbukia kwenye baa la njaa. Mashirika ya misaada ya kibinadamu likiwepo la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP yako mstari wa mbele kuwasaidia watu wenye uhitaji hususani wa chakula.

Akizungumza na UN News Mkurugenzi wa WFP Pembe ya Afrika Michael Dunford amesema hofu ya baa la njaa bado ni mtihani mkubwa hasa nchini Somalia.

Tweet URL

Amesema, “kwa bahati mbaya bado baa la njaa bado ni tishio nchini Somalia, tathimini inaendelea na tunaweza kushuhudia kabla ya mwisho wa mwaka huu au pengine mapema mwakani kutangazwa kwa hali ya baa la njaa katika badhi ya shehemu Somalia, kinachoniogopesha zaidi ni kwa sababu hadi wakati huo tuna tatizo kubwa la mvua, ukame utaendelea na huenda tunashuhudia hali hiyo ikitokea pia katika baadhi ya nchi za jirani.” 

Hali hiyo imesababisha kupanda kwa gharama za chakula Ukanda mzima na bwana Dunford alipoulizwa endapo mradi wa bahari Nyeusi wa kusafirisha nafaka umesaidia chochote kupunguza gharama hizo za chakula katika Pembe ya Afrika amesema, “bila shaka umekuwa na tija ndio maana ni muhimu saba ukaendelea, sio tu kwa upatikanaji wa bidhaa lakini pia mbolea. Unajua kwamba ukanda huo ni mzalishaji mkubwa wa mbolea na kiasi kikubwa kinapelekwa kwenye pembe ya Afrika. Kupungua kwa bei ya mbolea kunamaanisha kuongezeka kwa mazao kwa wakulima na hatimaye kuongeza uhakika wa chakula. Hivyo sababu zote zinahitaji kutiliwa maanani na wafanya maamuzi. Kwa hakina hatutaki kuona kwamba baada ya majadiliano mengi mradi huo unaruhusiwa kuteleza”