Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazalia mapya ya nzige kuongeza hatari Pembe ya Afrika:FAO

Nzige wa jangwani.
Picha: FAO/G.Tortoli
Nzige wa jangwani.

Mazalia mapya ya nzige kuongeza hatari Pembe ya Afrika:FAO

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO, leo limeonya kwamba kuna tishio kubwa la kutokuwa na uhakika wa chakula na maisha kwenye pembe ya Afrika kutokana na mlipuko wa nzige na mazalia mapya ya wadudu hao hatari.

Ripoti iliyotolewa leo na shirika hilo kuhusu hali ya mlipuko wa nzige wa jangwani inasema hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi kutokana na mazalia mapya ambayo yanaongeza idadi ya nzige Ethiopia, Kenya na Somalia.

FAO inasema Sudan Kusini na Uganda ziko katika hatari na pia kuna hofu ya makundi mapya ya nzige Eritrea, Saudi Arabia, Sudan na Yemen. Afisa wa utabiri wa nzige wa FAO Keith Cressman amesema “Makundi ya nzige yameanza kutaga mayai na kizazi kipya kitaongeza idadi ya nzige. Juhudi za haraka lazima zifanyike kukomesha mazalia mapya ili kulinda maisha ya wakulima na wafugaji.”

Kwa mujibu wa FAO huu ni mlipuko mbaya zaidi wa nzige wa jangwani kushuhudiwa katika ukanda huo kwa miongo kadhaa. Maelfu ya ekari za mazao na malisho zimeharibiwa vibaya nchini Ethiopia, Kenya na Somalia huku kukiwa na uwezekano wa athari kubwa katika Pembe ya Afrika ambako tayari watu milioni 11.9 hawana uhakika wa chakula.

Na uwezekano wa uharibifu kutokana na nzige hao ni mkubwa kwani imeelezwa kwamba kundi la nzige likivamia kilomita moja linaweza kula mazao ambayo ni sawa na mlo wa siku moja wa watu 35,000.

Kenya, nzige hao wamejikita katika maeneo ya Kaskazini na Katikati na wameshaathiri kaunti 13 na wengine wameanza kutaga mayai ambayo yataanguliwa mapema Februari na nzige wapya kushamiri kuanzia Aprili.

FAO inahitaji dola milioni 70 ili kusaidia operesheni na hatua za haraka kuweza kulinda maisha na kuzuia hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu kuwa mbaya zaidi.