Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa WFP walisha zaidi ya wasomali milioni 4 kwa mwezi 

WFP ikigawa msaada wa chakula Somalia wakati wa COVID-19 (kutoka maktaba)
WFP/Ismail Taxta
WFP ikigawa msaada wa chakula Somalia wakati wa COVID-19 (kutoka maktaba)

Msaada wa WFP walisha zaidi ya wasomali milioni 4 kwa mwezi 

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP linaendelea kufikisha msaada wa kuokoa maisha wa chakula na lishe kwa mamilioni ya watu nchini Somalia hasa wakati huu ambao nchi hiyo imeghubikwa na hatari ya kutumbukia kwenye baa la njaa. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika hilo hii leo mjini Geneva Uswisi zaidi ya watu milioni 4 wanapokea msaada wa dharura wa kibinadamu kwa mwezi ikiwemo chakula ili kuzuia baa la njaa wakati Pembe ya Afrika ikilabiliwa na ukame mkali kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40. 

Ongezeko la msaada huo limesaidia kuliweka kando baa la njaa kwa sasa, lakini WFP inasema hali katika maeneo mengi nchini Somalia bado ni mbaya huku maisha ya watu na uwezo wao wa kuishi vikipotea. 

Shirika hilo hivi sasa linakimbizana na muda ili kuepusha baa la njaa lililotabiriwa na idadi ya vifo ambayo huenda ikifikia maelfu ya watu. 

Kilichofanywa na WFP hadi sasa 

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita WFP imeongeza zaidi ya mara mbili idadi ya watu inaowafikia na msaada wa chakula na fedha taslim kutoka watu milioni 1.7 mwezi April hadi kufikia watu milioni 4.4 mwezi August. 

Watu wengine 45,000 watoto na kina mama wamepokea msaada wa lishe kutoka WFP mwezi August wakati shirika hilo lilipoongeza idadi ya watu inaowasaidia na vituo vya matibabu. 

Shirika hilo limesema linaendelea kupanua wigo wa msaada wake ili kufika hata katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika ya vijijini ikiwemo  katika wilaya za Baidoa na Burhakaba ambayo yako katika hatihati ya baa la njaa. 

Msaada wa chakula na wa kuhamisha fedha kwa njia ya simu za rununu umekuwa mkombozi mkubwa kwa watu hao. 

WFP ndio shirika kubwa zaidi la kibinadamu nchini Somalia likiwa na ofisi 12 nchi nzima na linatoa msaada katika kila jimbo. 

Pamoja na kuwashukuru wahisani ambao wanalipihga jeki shirika hilo, WFP imesema ina pengo la dola milioni 412 ili kuweza kutekeleza operesheni zake kwa miezi sita ijayo hadi kufika Machi 2023 ikiwemo upungufu wad ola milioni 315 za msaada wa kuokoa maisha wa chakula na lishe.