Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ethiopia: Usafirishaji haramu binadamu udhibitiwe Tigray, Afar na Amhara

Kundi la wakimbizi wa ndani kutokana na mzozo wa Tigray wakiwa kwenye kambi huko jimboni Afar nchini Ethiopia
© UNHCR/Alessandro Pasta
Kundi la wakimbizi wa ndani kutokana na mzozo wa Tigray wakiwa kwenye kambi huko jimboni Afar nchini Ethiopia

Ethiopia: Usafirishaji haramu binadamu udhibitiwe Tigray, Afar na Amhara

Haki za binadamu

Wanawake na wasichana katika majimbo ya Trigray, Afar na AMhar nchini Ethiopia wanazidi kuwa hatarini kutekwa na kusafirishwa kiharamu ili kutumikishwa kingono wakati wakikimbia machafuko kwenye mzozo unaoendelea kaskazini mwa nchi hiyo, wamesema wataalamu wa Umoja wa Mataifa kupitia taarifa yao waliyoitoa leo huko Geneva, Uswisi.

Wataalamu hao wameonya kuwa mzozo huo usiomalizika umeongeza hatari ya usafirishaji haramu binadamu kwa ajili ya kutumikishwa kingono kama aina moja ya ukatili wa kingono kwenye mizozo.

“Tuna hofu juu ya ripoti ya kwamba wakimbizi na wakimbizi wa ndani wanawake na watoto wa kike huko Tigray, Afar na Amhara wanatekwa wakati wakijaribu kukimbia maeneo ya mzozo kuelekea maeneo salama,” wamesema wataalamu hao na tunahofia usafirishaji wa binadamu hasa kwa minajili ya utumikishaji kingono hasa utumwa wa kingono,” wamesema wataalam hao.

Wakimulika Tigray, wamesema Watoto wako hatarini zaidi kusafirishwa kiharamu na kutumikishwa kingono kwa sababu kwenye jimbo hilo mamia ya Watoto wametengana na familia zao.

Wanataka hatua za dharura zichukuliwe ili kuzuia kitendo hicho hasa kwa kutambua kuwa raia wa Eritrea wako hatarini Zaidi, na wakati huo huo kutoa msaada kwa ulinzi kwa watu wote bila kujali rangi, kabila, utaifa, hali ya ulemavu, umri au jinsia.

“Kuendelea kushindwa kufikisha misaada ya kibinadamu kwenye jimbo hilo ni hofu kubwa. Tunatoa wito kwa hatua za kitaifa, kati yan chi na kimataifa zichukuliwe ili kuzuia ai azote za usafirishaji haramu Watoto na kuhakikisha wanalindwa,” wamesema wataalamu  hao.

Mikakati ya kutosheleza haijachukuliwa kubaini manusura wa usafirishaji haramu ili kuwalinda na kuwapatia msaada waweze kujikwamua kutoka madhila hayo kwa kuzingatia machungu na kiwewe kinachowakumba baada ya Mikasa hiyo, wamesema wataalamu hao.

Watekelezaji wa uhalifu huo wawajibishwe

Na kama hiyo haitoshi, wamesema kushindwa kuwajibisha watekelezaji wa uhalifu huo wa kibinadamu na uhalifu wa kivita kunaweka mazingira ya kukwepa sheria na kuruhusu vitendo hivyo kusambaa na watekelezaji kutoadhibiwa.

Wametoa wito kwa wadau wote kuhakikisha manusura wa usafirishaji haramu binadamu wanapata msaada wa kutosha wa matibabu, ikiwemo huduma za afya ya uzazi na usaidizi wa kisaikolojia.

Tayari wataalamu hao wamekuwa wakiwasiliana na serikali za Eritrea na Ethiopia.

Mapigano kwenye majimbo ya Tigray, Amhara na Afar nchini Ethiopia  yalianza tarehe 3 mwezi Novemba mwaka 2020 kati ya vikosi vya kijeshi vya Tigray na jeshi la serikali ya Ethiopia.