Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa kusafirisha nafaka wa Bahari Nyeusi: Ni nini, na kwa nini ni muhimu kwa dunia 

Wafanyakazi katika bandari ya Dar Es Salaam wakipakia magunia ya ngano kuelekea Afrika ya Kati (kutoka Maktaba)
© FAO/Giuseppe Bizzarri
Wafanyakazi katika bandari ya Dar Es Salaam wakipakia magunia ya ngano kuelekea Afrika ya Kati (kutoka Maktaba)

Mpango wa kusafirisha nafaka wa Bahari Nyeusi: Ni nini, na kwa nini ni muhimu kwa dunia 

Msaada wa Kibinadamu

Tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulipoanza, mauzo ya nafaka kutoka Ukraine, pamoja na chakula na mbolea kutoka Urusi, yameathirika sana. Changamoto za usambazaji zimesukuma bei kupanda zaidi na kuchangia mgogoro wa chakula ulimwenguni kote.

Mpango wa kusafirisha nafaka wa Bahari Nyeusi, unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki, ulianzishwa ili kurjesha mauzo muhimu ya chakula na mbolea kutoka Ukraine hadi kwingineko duniani. Hapa kuna mambo muhimu ya kuelewa. 

1) Mpango wa kupata vifaa muhimu kusongesha tena mchakato 

Ukraine, mojawapo ya nchi wauzaji wakubwa wa nafaka duniani, kwa kawaida hutoa karibu tani milioni 45 za nafaka kwenye soko la kimataifa kila mwaka lakini, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini humo, mwishoni mwa Februari 2022, shehena ya nafaka iliyorundikana kwenye ghala, na kwenye meli hina njia salama ya kusafiroshwa na kutoka bandari za Ukraine, na njia za bara bara nchi kavu haziwezi kufidia. 

Hii imechangia kupanda kwa bei ya vyakula muhimu kote ulimwenguni. Ikiunganishwa na ongezeko la gharama ya nishati, nchi zinazoendelea zimesukumwa kwenye ukingo wa kutolipa madeni na kuongezeka kwa idadi ya watu kujikuta kwenye hatihati ya njaa kubwa. 

Tarehe 22 Julai, Umoja wa Mataifa, Shirikisho la serikali ya Urusi, Uturuki na Ukraine walikubaliana Mpango wa kusafirisha nafaka wa Bahari Nyeusi, katika hafla ya kutia saini mpango huo iliyofanyika katika mjini Istanbul Uturuki. 

Mkataba huo unaruhusu mauzo ya nje ya nafaka kutoka Ukraine, vyakula vingine na mbolea, ikiwa ni pamoja na amonia, kuanza tena kusafirishwa kupitia njia salama ya kibinadamu ya baharini kutoka bandari tatu kuu za Ukraiine ambazo ni Chornomorsk, Odesa, na Yuzhny/Pivdennyi, hadi kwingineko duniani. 

Ili kutekeleza mpango huo, kituo cha uratibu wa pamoja (JCC) kilianzishwa mjini Istanbul, kikijumuisha wawakilishi wakuu kutoka Shirikisho la Urusi, Uturuki, Ukraine, na Umoja wa Mataifa. 

Kulingana na taratibu zilizotolewa na JCC, meli zinazotaka kushiriki katika mpango huo zitakaguliwa nje ya Istanbul ili kuhakikisha kuwa hazina shehena, kisha kusafiri kupitia mpango wa kibinadamu ukanda wa baharini hadi bandari za Ukraine kupakia shehena.  

Ukanda huo umeanzishwa na JCC na kufuatiliwa kwa saa 24 siku zote za wiki ili kuhakikisha njia salama ya vyombo vinavyosafirisha shehena.  

Meli zinazosafirisha shehena hiyo ya chakula katika safari za kurejea pia zitakaguliwa katika eneo la ukaguzi karibu na Istanbul. 

Kituo Mpango wa nafaka  wa Bahari Nyeusi
UN News
Kituo Mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi

2) Mamilioni ya tani za nafaka yaondoka Ukraine 

Usafirishaji  wa nafaka kupitia mpango huo ulianza kuondoka kuanzia tarehe 1 Agosti.  

Kufikia mwisho wa mwezi huo, zaidi ya meli 100, zilizobeba zaidi ya tani milioni moja za nafaka na vyakula vingine, zilikuwa zimeondoka Ukraine.  

Kufikia katikati ya Septemba JCC iliripoti kwamba takriban tani milioni tatu zimesha ondoka Ukraine, kuashiria maendeleo chanya. Inatarajiwa kwamba, hatimaye, hadi tani milioni tano zitauzwa nje ya nchi kila mwezi. 

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, asilimia 51 ya shehena hadi sasa (kufikia katikati ya mwezi Septemba) imekuwa mahindi, asilimia 25 ya ngano, asilimia 11 ya alizeti, asilimia sita ya mbegu za rapa, asilimia tano ya shayiri, asilimia moja ya maharagwe ya soya na asilimia moja ya vyakula vingine. 

Mwanamke akipembua ngano nchini India (Kutoka Maktaba)
World Bank/Ray Witlin
Mwanamke akipembua ngano nchini India (Kutoka Maktaba)

3) Takriban theluthi moja ya nafaka zinakwenda kwa nchi za kipato cha chini 

Asilimia 25 ya shehena imekwenda kwa nchi za kipato cha chini na cha kati.  

Misri (asilimia 8), India na Iran (asilimia 4 kila moja), Bangladesh, Kenya na Sudan (asilimia 2 kila moja), Lebanon, Yemen, Somalia, Djibouti (asilimia 1%) na Tunisia (chini ya asilimia moja). ) 

Hii ni pamoja na meli zilizokodishwa na Umoja wa Mataifa zinazopeleka msaada wa kibinadamu wa chakula  kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani (WFP) lililonunua ngano kwa ajili ya Pembe ya Afrika na Yemen. Meli mbili zilizokodishwa na Umoja wa Mataifa tayari zimeondoka Ukraine, huku nyingine mbili zikitarajiwa hivi karibuni.  

WFP kufikia sasa imenunua tani 120,000 za ngano kusaidia misaada ya kibinadamu katika Pembe ya Afrika, Yemen na Afghanistan. 

Meli ya kwanza iliyokodishwa na WFP ilitia nanga nchini Djibouti tarehe 30 Agosti kusaidia kukabiliana na ukame katika Pembe ya Afrika.  

Meli ya pili iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa, iliyosheheni tani 37,500 za ngano, ilisafiri tarehe 30 Agosti na kutia nanga nchini Uturuki tarehe 3 Septemba, ambapo ngano itasagwa na kuwa unga. 

Kisha unga huu utapakiwa kwenye meli tofauti ambayo itaelekea Yemen kusaidia operesheni za msaada wa kibinadamu za WFP huko.  

Meli ya tatu na ya nne zilizokodishwa na WFP pia zitasambaza ngano kwa shughuli za misaada. 

Baadhi ya asilimia 25 ya nafaka imekwenda katika nchi zz kipato cha kati ikiwa ni pamoja na TUturuki, Uchina na Bulgaria na asilimia 50 kwa nchi zenye kipato cha  juu kama vile Uhispania, Uholanzi, Italia, Jamhuri ya Korea, Romania, Ujerumani, Ufaransa, Ugiriki, Ireland na Israel. 

Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa nafaka zote zinazotoka katika bandari za Ukraine kutokana na Mpango huo wa kusafirisha nafaka huwanufaisha watu wanaohitaji, kwani husaidia kutuliza mgogoro wa masoko, na kupunguza mfumuko wa bei za vyakula. 

Katibu Mkuu António Guterres akitazama nafaka zikipakiwa kwenye meli ya Kubrosliy mjini Odesa, Ukraine.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu António Guterres akitazama nafaka zikipakiwa kwenye meli ya Kubrosliy mjini Odesa, Ukraine.

4) Bei za vyakula zinashuka 

Kuna dalili kubwa kwamba Mpango huo unafanikiwa katika mojawapo ya malengo yake makuu, kupunguza bei ya vyakula. 

Katika mkutano na waandishi wa habari katikati ya mwezi Septemba, Rebeca Grynspan, katibu mkuu wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo UNCTAD, na Amir Abdulla, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi walikaribisha ukweli kwamba bei ya chakula imeshuka kwa miezi mitano katika mstari, tathimini ya bei ya chakula imepungua kwa karibu asilimia 14 kutoka kilele chake hapo Machi mwaka huu. 

Bwana Abdulla alieleza kuwa kushuka kwa bei kunamaanisha kwamba wale waliokuwa wakihifadhi nafaka, kwa matumaini ya kuuza kwa faida kubwa, sasa wanauza, jambo ambalo lilimaanisha kwamba sasa kuna usambazaji mkubwa wa chakula katika masoko, na kusababisha kushuka zaidi kwa bei.  

Bi Grynspan, ambaye pia ni mratibu wa timu ya kikosi kazi cha Umoja wa Mataifa iliyoundwa kusaidia nchi zinazosaidia kukabiliana na misukosuko ya mara tatu ya kiuchumi iliyozidishwa na athari za vita vya Ukraine, alidokeza kwamba hii inaleta mabadiliko makubwa katika gharama za kimataifa za mgogoro wa maisha. 

Duniani kote, watu milioni 345 katika zaidi ya nchi 80 kwa sasa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, wakati hadi watu milioni 50 katika nchi 45 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa bila msaada wa kibinadamu. 

Mwezi Agosti, mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasley alitangaza kufunguliwa bandari za Bahari Nyeusi kuwa "Ni jambo muhimu zaidi ambalo tunaweza kufanya hivi sasa kusaidia wenye njaa duniani".  

Alionya kwamba, wakati hii peke yake haitazuia njaa duniani, kurejesha nafaka ya Ukraine kwenye masoko ya kimataifa kungeboresha nafasi ya kuzuia mzozo wa chakula duniani usizidi kuongezeka. 

Katibu Mkuu António Guterres (Kushoto) na Rais ecep Tayyip Erdoğan wakati wa sherehe za utiaji saini wa mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi mjini Istanbul Uturuki
UNIC Ankara/Levent Kulu
Katibu Mkuu António Guterres (Kushoto) na Rais ecep Tayyip Erdoğan wakati wa sherehe za utiaji saini wa mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi mjini Istanbul Uturuki

5) Ushirikiano unaoendelea ni muhimu kwa mafanikio endelevu 

Umoja wa Mataifa unafahamu vyema kwamba kuhakikisha shehena zinasafiri vizuri nje ya bandari za Ukraini kutahitaji ushirikiano unaoendelea wa Ukraine na Urusi. 

Bwana. Abdulla amesifu "Moyo wa ushirikiano kati ya wahusika katika mpango huo.” 

Pia alibainisha jukumu maalum ambalo Uturuki na Umoja wa Mataifa wanalo katika kuhakikisha mchakato unaendelea. 

Lakini amesema “Bila kuwa na ishara iliyo wazi ya mwisho wa vita , mustakbali haujulikani.” 

Mpango wa sasa unaweza kurefushwa zaidi ya siku zake 120 za awali baada ya tarehe ya kutiwa saini ambayo ni 22 Julai, ikiwa wahusika watachagua hilo. Mawazo katika timu ya JCC huko Istanbul tayari yanageukia upanuzi wa mpango huo.  

Bwana. Abdulla bado ana matumaini, akielezea kwamba "kwa juhudi za upatanishi za Umoja wa Mataifa, halitakuwa suala la kujadiliwa".