Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi umeongezewa muda:UN

Kamanda wa MV Brave katika bandari ya Hodeidah Yemen ikiwa imebeba nafaka ya unga wa ngano kutoka Ukraine  kuelekea Uturuki Oktoba 2022
© WFP/Mohammed Nasher
Kamanda wa MV Brave katika bandari ya Hodeidah Yemen ikiwa imebeba nafaka ya unga wa ngano kutoka Ukraine kuelekea Uturuki Oktoba 2022

Mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi umeongezewa muda:UN

Amani na Usalama

Mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi, uliotiwa saini mjini Istanbul Uturuki tarehe 22 Julai 2022, umeongezwa muda.

Kwa mujibu wa taaifa iliyotolewa leo mjini New York Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric “Mpango huo unaruhusu kuwezesha usambazaji salama nje wa mauzo ya nafaka, vyakula na mbolea zinazohusiana na uzalishaji wa chakula, ikiwa ni pamoja na mbolea ya amonia, kutoka bandari maalum za Ukraine.”

 Katika mihula miwili ya kwanza, takriban tani milioni 25 za nafaka na vyakula zimesafirishwa hadi katika nchi 45, na kusaidia kupunguza bei ya chakula duniani na hivyo kuleta utulivu wa masoko.

“Tunatoa shukrani zetu kwa serikali ya Uturuki kwa msaada wa kidiplomasia na kiutendaji kwa mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi.” Ameingeza msemaji huyo ya Umoja wa Mataifa.

Mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi, pamoja na mkataba wa maelewano juu ya kukchagiza kuhusu bidhaa za chakula na mbolea za Kirusi kwenye masoko ya dunia, ni muhimu kwa uhakika wa chakula duniani, hasa kwa nchi zinazoendelea umesisitiza Umoja wa Mataifa.

Taarifa hiyo imehitimisha kwa kusema kwamba “Tunasalia na nia ya dhati kwa mikataba yote miwili na tunazihimiza pande zote kuzidisha juhudi zao ili kuitekeleza kikamilifu.”