Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi kujitoa mpango wa nafaka Bahari Nyeusi ni pigo kwa wengi, lakini hatukati tamaa - UN

Timu za pamoja za ukaguzi zinashirikiana nchini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.
© UNODC/Duncan Moore
Timu za pamoja za ukaguzi zinashirikiana nchini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

Urusi kujitoa mpango wa nafaka Bahari Nyeusi ni pigo kwa wengi, lakini hatukati tamaa - UN

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake makubwa kufuatia kitendo cha Urusi cha sio tu kujiondoa katika Mpango wa kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi bali pia kuondoa hakikisho lake la ulinzi kwenye eneo la majini huko kaskazini magharibi mwa Bahari Nyeusi.

Guterres ameelezea masikitiko hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Katibu amesema masikitiko yake yanazingatia ukweli kwamba Mpango huo tangu uanzishwe mwezi Julai mwaka jana kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari mwaka huo wa 2022, umefanikisha usafirishaji wa zaidi ya tani milioni 32 za ujazo kutoka bandari za Ukraine.

Miongoni ni tani 752,000 zilizosafirishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP kwa ajili ya kunusuru mamilioni ya watu waliokuwa wanakumbwa zaidi na njaa duniani ikiwemo Afghanistani, Pembe ya Afrika na Yemen.

“Mpango wa kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi pamoja na Makubaliano ya Maelewano ya kufanikisha usafirishaji wa bidhaa za vyakula na mbolea kutoka Urusi vimekuwa uti wa uhai katika kufanikisha uhakika wa kupata chakula, halikadhalika nguzo ya matumaini katika dunia iliyogubikwa na changamoto na mizozo,” amesema Katibu Mkuu.

Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi unaruhusu kiasi kikubwa cha mauzo ya chakula cha kibiashara kutoka bandari tatu muhimu za Kiukreni katika Bahari Nyeusi.
UN News
Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi unaruhusu kiasi kikubwa cha mauzo ya chakula cha kibiashara kutoka bandari tatu muhimu za Kiukreni katika Bahari Nyeusi.

Mpango ulikuwa muarobaini kwa mamilioni walio na njaa

Guterres amesema wakati uzalishaji na upatikanaji wa chakula ukiwa umevurugwa na mizozo, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la bei ya nishati na sababu kadha wa kadha, makubaliano hayo yalisaidia kupunguza bei za vyakula kwa zaidi ya asilimia 32 kuanzia mwezi Machi mwaka jana.

Katibu Mkuu amesema kinachosikitisha zaidi, pamoja na kujiodoa kwenya Mpango huo, Urusi imesitisha pia ahadi yake ya kufanikisha usafirishaji bila vikwazo vyovyote wa vyakula, mafuta ya alizeti na mbolea kutoka bandari za Ukraine, ahadi ambayo imewekwa bayana kwenye Aya ya 1 ya Makubaliano ya Maelewano ya kati ya Urusi na Umoja wa Mataifa.

Ingawa ushiriki kwenye makubaliano haya ni chaguo, jambo la kusikitisha ni kwamba kwa watu wanaohaha kokote kule na nchi zinazoendelea, si chaguo. Mamia ya mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa na walaji wanakumbana na janga la ongezeko la gharama ya maisha,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa watu hao ndio watalipa gharama ya Urusi kujitoa kwenye Mpango husika kwani tayari leo asubuhi bei ya ngao imeongezeka.

Rais Putin amepuuza waraka wetu kwake

Amesema anatambua baadhi ya vikwazo vilivyosalia katika biashara ya kigeni ya vyakula na mbolea kutoka Urusi “na ndio maana alimtumia barua Rais Vladmir Putin wa Urusi yenye pendekezo jipya kuhusu Mpango wa kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi.”

Guterres ameeleza kinagaubaga kilichomo kwenye barua hiyo, mathalani utulivu katika soko la mbolea kutoka Urusi kutokana na Makubaliano ya Maelewano, kama ilivyothibitishwa na Umoja wa wauzaji wa nafaka nje ya Urusi na Chama cha wazalishaji wa mbolea nchini Urusi.

Halikadhalika, hatua zilizochukuliwa na Umoja wa Mataifa za kufanikisha biashara katika maeneo yaliyokuwa na changamoto na vikwazo kama vile Uingereza, Marekani na Muungano wa Ulaya.

Guterres amesema cha kusikitisha Urusi  imepuuza yaliyomo kwenye barua hiyo na kwamba uamuzi wa leo wa Urusi utakuwa ni ‘mwiba’ kwa watu wenye uhitaji kila mahali.

Timu ya pamoja ya ukaguzi ikiwa kazini chini ya mpango wa usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi
© UNODC/Duncan Moore
Timu ya pamoja ya ukaguzi ikiwa kazini chini ya mpango wa usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi

Hatua ya Urusi haitukatishi tamaa

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema “uamuzi wa Urusi hautazuia juhudi zetu za kufanikisha vyakula na mbolea kutoka Ukraine na Urusi kufikia masomo mbalimbali duniani bila vikwazo vyovyote. Na ni kwa msingi huo natambua juhudi za serikali ya Uturuki.”

Hivyo basi amesema katika kusonga mbele, lengo letu lazima liwe kuendelea kufanikisha uhakika wa upatikanaji wa chakula na bei ziwe tulivu. Hii itaendelea kuwa kipaumbele cha juhudu zangu kwa kuzingatia ongezeko la machungu ya binadamu kutokana na uamuzi wa leo.

Mpango wa kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi ulitiwa saini tarehe 13 mwezi Julai mwaka jana wa 2022 huko Istanbul, Uturuki.

Hadi mwezi Julai mwaka huu wa 2023, zaidi ya tani milioni 32 za bidhaa za chakula zimesafirishwa kutoka bandari tatu za Bahari Nyeusi za Ukraine hadi nchi 45 katika mabara matatu.