Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN itaendelea kusaka suluhu na haki ya amani kwa watu wa Ukraine:Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) akiwa Kyiv, Ukraine amesisitiza tena kuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
UN /Vitalii Ukhov
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) akiwa Kyiv, Ukraine amesisitiza tena kuwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

UN itaendelea kusaka suluhu na haki ya amani kwa watu wa Ukraine:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani kwa mara ya tatu nchini Ukraine katika mud awa chini yam waka mmoja amewaahidi watu wa taifa hilo wanaokabiliwa na vita kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea bila kuchoka kusaka suluhu ya vita hiyo na haki ya amani .

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kyvi hii leo Antonio Guterres amesema ziara hii ni ya kuoinyesha mshikamano na kujidhatiti kwa Umoja wa Mataifa kusaka suluhu ya vita inayoendelea nchini humo.

“Msimamo wa Umoja wa Mataifa, ambao nimeueleza mara kwa mara, uko bayana kabisa kwamba uvamizi wa Urusi kwa Ukraine ni ukiukaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa. Uhuru, uhuru wa kujitawala, umoja na uadilifu wa eneo la Ukraine lazima udumishwe, ndani ya mipaka yake inayotambulika kimataifa.”

Lengo letu kuu liko wazi vile vile anesema Guterres ambalo ni haki ya amani kulingana na mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria ya kimataifa na azimio la hivi karibuni la Baraza Kuu la kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanza kwa vita ya Ukraine.

“Hadihaki hiyo ya amani iweze kupatikana, tunaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza athari za mzozo ambao tayari umesababisha mateso makubwa kwa watu wa Ukraine na athari kubwa kwa Ulimwengu mzima.”

Katibu Mkuu António Guterres kushoto akijadili hali ya Ukraine na Rais Volodymyr Zelenskyy.
UN Photo/Vitalii Ukhov
Katibu Mkuu António Guterres kushoto akijadili hali ya Ukraine na Rais Volodymyr Zelenskyy.

UN itaendelea kuwasaidia watu wa Ukraine

Katibu Mkuu amesema tangu kuanza kwa vita Umoja wa Mataifa umesalia chini humoili kupeleka misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa mamilioni ya watu Ukraine.

“Ninataka kueleza mshikamano wangu wadhat na waathirika wote wa vita. Kwa wale waliopoteza maisha na wapendwa wao. Kwa wale ambao wameona matumaini yao yamepotea au walilazimika kukimbia kuokoa maisha. Wote wanastahili uwajibikaji Madhubuti kwa wahusika wa vita.”

Umoja wa Mataifa pia umefanya kazi kubwa kusaidia kuwahamisha raia walionaswa katika kiwanda cha chuma cha Azovstal.

Mchango wa mashirika ya UN

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia amezungumzia mchango mkubwa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Ukraine katika kusaidia akisema mathalani shirika la kimataifa la nishati ya atomiki IAEA limehamasishwa kikamilifu kujaribu na kuhifadhi ulinzi na usalama wa vinu vya nishati ya nyuklia nchini Ukrainia, ikiwa ni pamoja na huko Zaporizhzhia.

Pia amesema mpango wa nafaka wa bahari Nyeusi, ulioafikiwa mwezi Julai mwaka jana huko Istanbul Uturuki, umetoa tani milioni 23 za nafaka kutoka bandari za Ukraine.

Hatua hiyo imechangia kupunguza gharama za kimataifa za chakula na imetoa ahueni muhimu kwa watu, ambao pia wanalipa gharama kubwa ya vita hivi, haswa katika nchi zinazoendelea.

“Kwa hakika, tathimini ya bei ya chakula ya shirika la chakula na kilimo na Umoja wa Mataifa FAO imeshuka kwa karibu asilimia 20 zaidi ya mwaka jana.

Mauzo ya Ukraine pamoja na Urusi ya chakula na mbolea ni muhimu kwa uhakika wa chakula na bei ya chakula duniani.” Amesisitiza Katibu Mkuu

Katibu Mkuu António Guterres  kushoto akikutana na Rais Volodymyr Zelenskyy mjini Kyiv.
UN Photo/Vitalii Ukhov
Katibu Mkuu António Guterres kushoto akikutana na Rais Volodymyr Zelenskyy mjini Kyiv.

Mpango wa nafaka wa baharí Nyeusi

Guterres amesema “Ninataka kusisitiza umuhimu wa kuendelea kwa usafirishaji wa mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi tarehe 18 Machi na kufanya kazi ili kuunda mazingira ya kuwezesha matumizi makubwa zaidi ya miundombinu ya usafirishaji kupitia Bahari Nyeusi, kulingana na malengo ya mpango huo.”

Pia amezungumzia ulinzi na usalama karibu na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kuwa ni muhimu.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia na wakati huo huo, tutaendelea kuunga mkono suluhisho za matatizo ya kibinadamu popote inapowezekana kwa kila nyanja kama vile kupanua wigo wa ubadilishanaji wa sasa wa wafungwa wa vita hadi utakapokamilika.

Kuhusu mauaji yanayoendelea katika vita hiyo Guterres amesema “Picha za hivi majuzi za kushtua za mwanajeshi wa Ukraine akionekana kuuawa kikatili ni ukumbusho mwingine wa kusikitisha kwamba sheria za vita lazima ziheshimiwe kabisa na kila wakati.”

Amemaliazia mkutano wake na waandishi wa habari akihimiza kwamba “Ni lazima tufuatilie malengo haya yote, tukitambua kwamba kila moja wapo lina thamani yenyewe. Ninaweza kuwahakikishia kwamba tutaendelea kutafuta suluhu na amani ya haki kwa watu wa Ukraine na dunia nzima.”