Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu UN apongeza hatua ya serikali ya Tigray

Mkimbizi wa ndani akiwa amebeba mwanae huko Mekelle, mji mkuu wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.
©UNICEF/ Esiey Leul
Mkimbizi wa ndani akiwa amebeba mwanae huko Mekelle, mji mkuu wa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Katibu Mkuu UN apongeza hatua ya serikali ya Tigray

Amani na Usalama

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha tangazo la serikali ya jimbo la Tigray nchini Ethiopia la kuzingatia mpango wa sitisho la mapigano na hatimaye kusaka kwa amani suluhu ya mzozo unaoendelea kaskazini mwa nchi hiyo.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imo kwenye taarifa iliyotolewa Jumapili usiku wa tarehe 11 mwezi Septemba mwaka huu wa 2022.

Guterres amesema anatiwa moyo na tangazo la utayari wa serikali hiyo ya jimbo la Tigray wa kushiriki kwenye mchakato bora wa amani unaoongozwa na Muungano wa Afrika, AU.
 
“Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande husika kwenye mchakato huo kutumia fursa ya sasa kwa ajili ya amani, na kuchukua hatua ili kutokomeza kabisa ghasia na mazungumzo yachukue nafasi yake,” imesema taarifa hiyo.

Kundi la wakimbizi wa ndani kutokana na mzozo wa Tigray wakiwa kwenye kambi huko jimboni Afar nchini Ethiopia

Amesisitiza kuwa pande husika zishiriki kikamilifu kwenye mchakato huo unaoongozwa na Muungano wa Afrika na ziweke mazingira rafiki ili mazungumzo yaweze kufanyika.

Katibu Mkuu amesisitiza juu ya utayari wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia mchakato huo.

Tamko la serikali ya jimbo la Tigray la kuzingatia sitisho la mapigano limetolewa wakati Ethiopia ikisherehekea mwaka mpya kwa kalenda ya taifa hilo ambapo Guterres ametumia pia fursa hiyo kuwatakia mwaka mpya wenye amani na fanaka.

Tigray na utayari wake kwa sasa

Vyombo vya habari vimenukuu taarifa iliyotolewa na serikali ya jimbo la Tigray ikisema kuwa wako tayari kushiriki kwenye mchakato huo ili kumaliza mzozo uliodumu kwa takribani miaka miwili sasa.

Timu ya jimbo la Tigray katika mchakato wa mazungumzo ya amani inajumuisha msemaji wa jeshi la ukombozi wa Tigray, TPLF pamoja na Jenerali kutoka kikosi hicho na kwa mujibu wa taarifa ya kikosi hicho, ujumbe huo uko tayari kwenda kushiriki mazungumzo bila kikwazo chochote.

Mwezi Juni mwaka huu, serikali ya Ethiopia iliunda kama ya mashauriano na vikosi kutoka jimbo la Tigray.