Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha hatua ya sitisho la mapigano Ethiopia 

Watoto waliofurushwa makwo wakichota maji Mekelle, mjii mkuu wa ukanda wa Tigray, Ethiopia.
© UNICEF/Esiey Leul
Watoto waliofurushwa makwo wakichota maji Mekelle, mjii mkuu wa ukanda wa Tigray, Ethiopia.

UN yakaribisha hatua ya sitisho la mapigano Ethiopia 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha tangazo la sitisho la mapigano lisilo na ukomo lililotangazwa na serikali ya Ethiopia, sitisho ambalo linaanza mara moja ili kufanikisha usambazaji wa huduma na misaada ya kibinadamu na tayari mamlaka za jimbo la Tigray zimeahidi kulizingatia. 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani ametangaza kauli hiyo ya Katibu Mkuu huku akisema kuwa “mapigano nchini Ethiopia yamesababisha machungu kwa mamilioni ya wananchi katika majimbo la Afar, Amhara, Tigray, Benishangul Gumz na Oromia.” 

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema “hatua hizi chanya lazima zitekelezwe saas kwa vitendo ili hali kwenye maeneo hayo iweze kuwa nzuri. 

Ni kwa mantiki hiyo Bwana Guterres anasisitiza wito wa kurejesha huduma za umma jimboni Tigray ikiwemo huduma za kibenki, umeme na mawasiliano sambamba. 

Ametoa wito pia kwa pande zote kufanikisha harakati za utoaji wa huduma za kibinadamu katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mzozo wa Tigray. 

“Katibu Mkuu amesihi pande zote pia kwenye mzozo zitumia fursa ya sasa kuchukua hatua zinazohitajika ili kuwa na sitisho la mapigano la kudumu,” ametamatisha Bwana Dujarric katika taarifa yake kwa wanahabari. 

Makubaliano hayo ya sitisho la mapigano lisilo na ukomo yamefikiwa jana wakati huu ambapo mapigano hayo yaliyodumu kwa miezi 16 sasa yamesababisha zaidi ya watu milioni mbili kukimbia makazi yao. 

Huduma za msingi za kibinadamu zimekuwa zikiwafikia kwa taabu baadhi ya wakazi walio kwenye maeneo yenye mzozo huku wengine wakiwa wanakosa kabisa huduma hizo.

Mwezi uliopita taarifa kutoka Ethiopia zilizotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chaklua duniani, WFP zilimnukuu mjamzito mmoja akisema kuwa kuna siku zinapita bila mlo, na wakati mwingine inabidi kupatia kwanza watoto chakula ndipo watu wazima waweze kula kilichobakia.