Hali ya Tigray inasikitisha mno- Guterres

3 Julai 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa huko Lisbon, Ureno ameelezea masikitiko  yake kutokana na hali inayoendelea huko jimboni Tigray nchini Ethiopia.
 

 

Guterres amesema “ninasikitishwa sana na hali ya sasa ya Tigray nchini Ethiopia,” akiongeza kuwa “uharibifu wa miundombinu ya kiraia haikubaliki kabisa.”

Katibu Mkuu amesema ni muhimu sana kuwa na sitisho halisi la mapigano ambalo litafungua njia ya mazungumzo yatakayowezesha kupata suluhu la kudumu la kisiasa.

Amesisitiza kuwa kuwepo kwa vikosi vya kigeni kunazidi kuchochea mapambano na kwamba ni lazima kuwekwe njia ya huduma za kibinadamu kufikia wahitaij bila kikwazo chochote jimboni Tigray.

Kauli ya Katibu Mkuu inakuja wakati hapo jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilijulishwa kuwa hali ni mbayá kwani watu 400,000 wana njaa ya kupindukia jimboni Tigray.

Halikadhalika takribani watu milioni 1.7 wamepoteza makazi kutokana na mapigano jimboni Tigray kati ya vikosi vya serikali na kikosi cha ulinzi wa Tigray ambapo 60,000 kati yao wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Sudan. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter