Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame na mabadiliko ya tabianchi vyazidisha adha ya maji Afrika:WMO

WFP inatekeleza mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuzisaidia jamii kujiandaa kukabiliana na changamoto za maji na mabadiliko ya tabianchi
© WFP/Alice Rahmoun
WFP inatekeleza mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuzisaidia jamii kujiandaa kukabiliana na changamoto za maji na mabadiliko ya tabianchi

Ukame na mabadiliko ya tabianchi vyazidisha adha ya maji Afrika:WMO

Tabianchi na mazingira

Inaonyesha jinsi hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi yanavyodhoofisha afya na usalama wa binadamu, uhakika wa chakula na maji na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Changamoto ya maji na hatari nyingine kama vile ukame usioisha na mafuriko makubwa vinaathiri sana jamii za Kiafrika, uchumi na mifumo ya ikolojia, huku mifumo ya mvua ikitatizika, barafu inatoweka na maziwa muhimu yanapungua kina cha maji.
Pia kuongezeka kwa mahitaji ya maji pamoja na usambazaji mdogo na usiotabirika kunatishia kuzidisha migogoro na watu kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la hali ya Hewa Duniani (WMO).
Ripoti hiyo ya hali ya hewa barani Afrika kwa mwaka 2021 inatoa taarifa za kisayansi za kuaminika kuhusu mwenendo wa hali ya joto na viashiria vingine vya hali ya hewa. 
Inasema Afŕika inachangia tu takriban asilimia 2% hadi 3% ya uzalishaji wa gesi chafuzi duniani lakini inateseka kwa kiasi kikubwa kutokana na matokeo ya athari za gesi hiyo chafuzi.
Katibu Mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas katika ripoti hiyo amesema "Hali mbaya ya mgogoro na baa la njaa inalonyemelea katika Pembe ya Afrika iliyokumbwa na ukame wa muda mrefu inaonyesha jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuzidisha changamoto ya maji, na kutishia maisha ya mamia ya maelfu ya watu na kudhoofisha jamii, nchi na kanda nzima,"