Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti mpya ya mabadiliko ya tabianchi ni historia ya zahma kubwa: UN 

Joto kali la kupindukia ni moja ya majanga yaliyokatili maisha ya watu wengi katika historia yakisababisha mamilioni ya watu kufungasha virago
© Unsplash/Emerson Peters
Joto kali la kupindukia ni moja ya majanga yaliyokatili maisha ya watu wengi katika historia yakisababisha mamilioni ya watu kufungasha virago

Ripoti mpya ya mabadiliko ya tabianchi ni historia ya zahma kubwa: UN 

Tabianchi na mazingira

Ripoti mpya ya shirika la utabiri wa hali ya hewa la Umoja wa Mataifa WMO, iliyotolewa  leo Jumapili, inaonyesha kuwa miaka minane iliyopita imekuwa ya joto zaidi katika historia ya rekodi, ikichochewa na kuongezeka kwa viwango vya gesi chafuzi. 

Ripoti hiyo ya utafiti wa 2022 wa hali ya hewa duniani unaonyesha dalili za kuongezeka kwa hali ya hewa ya dharura, ambayo ni pamoja na kuongezeka maradufu kwa kiwango cha kupanda kwa kina cha maji ya bahari tangu 1993, hadi kufikia kiwango cha rekodi mpya ya juu zaidi mwaka huu, na dalili za kuyeyuka kwa barafu kusiko na kifani kwenye milima ya Alps ya barani Ulaya. 

Ripoti kamili ya 2022 inatazamiwa kutolewa katika msimu wa kchipukizi wa mwaka 2023, lakini utafiti wa wakati huu umetolewa kabla ya COP27, mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, ili kuongeza ufahamu wa kiwango kikubwa cha matatizo ambayo viongozi wa dunia wanapaswa kukabiliana nayo, ikiwa wanataka kuwa na matumaini yoyote ya kupata suluhu na udhibiti wa mzozo wa mabadiliko ya tabianchi duniani. 

"Kadiri ongezeko la joto linavyoongezeka, ndivyo athari zinavyozidi," amesema mkuu wa WMO Petter Taalas, ambaye amezindua ripoti hiyo katika hafla iliyofanyika Sharm El-Sheikh, Misri, kunakofanyika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa mwaka huu.  

Ameongeza kuwa "Tuna viwango vya juu sana vya hewa ukaa angani sasa hivi kiasi kwamba kiwango cha chini cha kusalia na nyuzi joto 1.5C cha mkataba wa Paris hakifikiwi. Tayari kumechelewa kwa barafu nyingi na kuyeyuka kutaendelea kwa mamia kama sio maelfu ya miaka, na kuleta athari kubwa kwa uhakika wa maji ". 

Barafu ya mlima ambayo inapungua kwa sababu ya halijoto inayoongezeka na theluji kidogo katika Wilaya ya Kargil, India.
© UNICEF/Srikanth Kolari
Barafu ya mlima ambayo inapungua kwa sababu ya halijoto inayoongezeka na theluji kidogo katika Wilaya ya Kargil, India.

Hali mbaya kila kona ya dunia 

Kwa mujibu wa WMO ripoti hiyo ni orodha ya kutatanisha ya matukio ya hali mbaya ya hewa yanayotia wasiwasi, yanayotokea wakati tayari kuna viwango vya rekodi ya juu vya hewa ukaa, methane, na hewa ya nitrojeni ambazo ni gesi kuu tatu za uchafuzi mkubwa zinazochangia ongezeko la joto duniani  ambalo kwa sasa linakadiriwa kuwa karibu nyuzi joto 1.15C juu ya viwango vya kabla ya maendeleo ya viwanda. 

Katika eneo lote la milima ya Alps,ripoti inasema upotezaji wa unene wa wastani wa kati ya mita tatu na zaidi ya nne wa barafu umerekodiwa, wakati huko Uswisi, theluji yote iliyeyuka wakati wa msimu wa kiangazi, ikiwa ni mara ya kwanza hii imetokea katika historia iliyorekodiwa, tangu mwanzo wa karne hii, kiasi cha kiwango cha barafu nchini kimeshuka kwa zaidi ya theluthi moja. 

Pia ripoti imeongeza kuwa kuongezeka kuyeyuka kwa barafu duniani kote kumesababisha viwango vya kina cha bahari kupanda zaidi ya miaka 30 iliyopita, katika viwango vinavyoongezeka kwa kasi.  

Kiwango cha ongezeko la joto la bahari pia kimekuwa cha juu sana katika miongo miwili iliyopita, mawimbi ya joto baharini yanazidi kuongezeka, na viwango vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea katika siku zijazo. 

Utafiti huo unaelezea athari za ukame na mvua nyingi, mfano Kenya, Somalia, na Ethiopia zinakabiliwa na upungufu wa mazao na uhaba wa chakula, kwa sababu ya msimu mwingine wa kiwango kidogo cha mvua za chini ya wastani, wakati zaidi ya theluthi moja ya nchi ya Pakistan ilikumbwa na mafuriko mwezi Julai na Agosti, kama matokeo ya mvua iliyovunja rekodi, na kusababisha karibu watu milioni 8 kuyahama makazi yao.  

Kanda ya kusini mwa Afrika ilikumbwa na mfululizo wa vimbunga kwa muda wa miezi miwili mwanzoni mwa mwaka, na huku Madagascar ikikubwa na mvua kubwa na mafuriko makubwa, na Septemba, Kimbunga Ian kilisababisha uharibifu mkubwa na kupoteza maisha ya watu huko Cuba na Kusini Magharibi mwa Florida. 

Sehemu kubwa za Ulaya zilighubikwa na vipindi vya mara kwa mara vya joto kali mfano Uingereza ilishuhudia rekodi mpya ya kitaifa tarehe 19 Julai, wakati hali ya joto iliongezeka na kufikia zaidi ya nyuzi toto 40 ° C kwa mara ya kwanza.  

Hii iliambatana na ukame unaoendelea na unaoharibu mazingira kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kuzuka kwa moto wa nyika. 

Ukame mkali Pembe ya Afrika, Ethiopia, Somalia na Kenya unaathiri mamilioni ya watu
UNICEF/Raphael Pouget
Ukame mkali Pembe ya Afrika, Ethiopia, Somalia na Kenya unaathiri mamilioni ya watu

Tahadhari ya mapema kwa wote 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumapili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameielezea ripoti  hiyo ya WMO kama ni "kipindi cha machafuko ya hali ya hewa," ambayo inaelezea kasi ya janga la mabadiliko ya tabianchi, ambayo yanaharibu maisha na uwezo wa watu kuishi katika kila bara. 

Dunia ikiwa inakabiliwa na kutoepukika kwa majanga ya mabadiliko ya tabianchi na hali mbaya ya hewa duniani kote, Bwana. Guterres “atazindua mpango kazi katika mkutano huo wa COP27 ili kufikia lengo la tahadhari ya mapema kwa wote katika miaka mitano ijayo.” 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa mifumo ya tahadhari ya mapema ni muhimu ili kulinda watu na jamii kila mahali. "Lazima tuchukue hatua dhidi ya ishara ya zahma kwa sayari yetu, kwa hatua kabambe na hatua za kuaminika za mabadiliko ya tabianchi. COP27 lazima iwe ndio mahali pa kufanya hivyo na lazima iwe wakati wa sasa."