Tishio la mabadiliko ya tabianchi linaendelea kuongezeka Afrika:WMO Ripoti

26 Oktoba 2020

Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la Umoja wa utabiri wa hali ya hewa WMO ikitanabaisha hali ya sasa na mustakabali wa hali ya hewa katika bara la Afrika inaonyesha kwamba mwaka 2019 ulikuwa miongoni mwa miaka mitatu yenye joto la kupindikia katika historian a mwenendo unatarajiwa kuendelea  ukisababisha watu kutawanywa na athari katika kilimo. 

Mbali yah apo ripoti inasema hali hiyo pia inaathari kubwa katika afya, uhakika wa chakula na maendeleo. 

Barani Afrika kwa mujibu wa ripoti hiyo , ongezeko la joto na kupanda kwa kina cha bahari, mabadiliko katika mwenendo wa mvua na hali zingine mbaya za hewa vinatishia afya, uhakika wa chakula na maji, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

UNOCHA/Otto Bakano
Mamia ya maelfu ya watu wanaoishi nchini Burkina Faso hawana uhakika wa chakula

Changamoto zilizopo 

Katika ripoti hiyo “Mwenendo wa hali ya hewa Afrika 2019” Katibu mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema “mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiwakumba watu walio hatarini zaidi na kuchangia kutokuwepo kwa uhakika wa chakula, watu kutawanywa na uhaba wa rasilimali muhimu ya maji.” 

Taalas ametaja majanga kadhaa ya miezi ya hivi karibbuni barani Afrika ikiwemo mafuriko, uvamizi wa nzige wa jangwani na mfululizo wa ukame uliosababishwa na La Nina. Pia ameongeza kuwa changamoto kubwa za kibinadamu na kiuchumi zimezidishwa na kuzuka kwa janga la COVID-19

Naye katibu mtendaji wa kamisheni ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika UNECA, Vera Songwe amesema “Kiwango kidogo cha kukubalika na matumizi ya taarifa za huduma za mabadiliko ya tabianchi hasa katika mipango na utekelezaji wa maendeleo Afrika vimechangia sehemu ya uhaba wa taarifa za kuaminika na za hali ya hewa. Hivyo ripoti hii mpya itasaidia kushughulikia pengo hilo.” 

WFP/Photolibrary
Picha kutoka angani ikionesha baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Idai huko Msumbiji.

Mabadiliko dhahiri 

Ripoti inasema mwaka 2019 ulikuwa miongoni mwa miaka mitatu iliyokuwa na joto la kupindukia katika historia ya bara la afrika n ani hali ambayo inatarajiwa kuendelea. 

Makadirio mapya yanajojumuisha kipindi cha 2020 hadi 2024 yanaonyesha kuendelea kwa ongezeko la joto na kupungua kwa kiwango cha mvua hususan katika maeneo ya Kaskazini na Kusini mwa bara hilo, na kuongezeka kwa mvua katika ukanda wa sahel. 

Makadirio hayo ya Umoja wa Mataifa pia ynaonyesha kwamba eneo kubwa la Afrika litazidi kiwango cha nyuzi joto 2C ambacho ni cha juu zaidi ya ilivyokuwa kabla ya mapinduzi ya viwanda katika miongo miwili ya karne hii.  

Ripoti inasema sehemu kubwa ya Afrika joto limeongezeka kwa zaidi ya nyuzi joto 1C tangu mwaka 1901 kukiambatana na siku nyingi zilizoghubikwa na jua kali na joto la kupindukia ukiwemo mwaka 2019. 

WMO/Cornel Vermaak
Ukame barani Afrika utaathiri uzalishaji wa nafaka, imesema ripoti ya WMO iliyozinduliwa leo

Kupanda kwa kina cha bahari 

Kuhusu kupanda kwa kina cha bahari ripoti inasema ongezeko la kina cha maji ya bahari kilifikia milimita 5 kwa mwaka katika maeneo mengi na kupita kiwango hicho katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi. Hivi ni viwango vya juu zaidi ya vile vya wastani vywa kimataifa ambavyo ni milimita 3-4 kwa mwaka. 

Kwa mujibu wa ripoti kumomonyoka kwa ufukwe wa bahari ni changamoto nyingine kubwa hasa Afrika Magharibi. Mathalani asilimia 56 ya pwani ya Benini, Cote d’Ivoire, Senegal na Togo inamomonyoka na hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi. 

Ripoti pia imeorodhesha matukio yaliyokuwa na athari kubwa mwaka 2019 kama vile kimbunga Idai kilichoikumba Msumbuji na kuelezwa kuwa ni moja ya vimbunga vilivyosababisha uharibifu mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika eneo la Kusini mwa dunia. 

Mwaka huohuo wa 2019 Afrika Kusini ilikabiliwa na ukame mbaya na Kusini Mashariki mwa bara hilo hali ilibadilika kutoka ukame, hadi mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyoambatana na mvua kubwa na mafuriko hayo pia yameathiri eneo la Sahel na viunga vyake. 

University of Plymouth/Carey Marks
Eneo la wamasai nchini Tanzania limekumbwa na kiwango kikubwa cha ongezeko la mmomonyoko wa udongo

Uhakika wa chakula 

Katika nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara idadi ya watu wenye utapiamlo imeongezeka kwa asilimia 45.6 tangu mwaka 2012 imesema ripoti hiyo. 

Afrika ambako kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa bara hilo na kuwahakikishia mamilioni ya watu kuishi, makadirio ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa yanaonyesha kwamba ongezeko la joto linaweza kuleta athari kubwa katika uzalishaji wa kilimo na uhakika wa chakula. 

Hatari kubwa ni Pamoja na kupungua kwa uzalishaji na ongezeko la uharibifu wa mazao kutokana na wadudu, magonjwa na athari za mafuriko. 

Na ifikapo katikati ya karne hii mazao makuu ya nafaka yatapata athari kubwa. Na katika hali mbaya makadirio ya kipato cha wastani yanatarajiwa kushuka kwa asilimia 13 katikka maeneo ya Magharibi na Katikati mwa Afrika. asilimia 11 Kaskazini mwa afrika na asilimia 8 Mashariki na Kusini mwa Afrika. 

© FAO/Haji Dirir
Nzige wa Jangwani ambao kwa muda wamevamia maeneo ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, sasa wamevamia nchi za kusini mwa Afrika.

Afya na uchumi 

Kwa mujibu wa ripoti joto kali na mvua nyingi vinaongeza hatari ya kuumwa na wadudu na kusamba kwa magonjwa kama homa ya kidingapopo, malaria na homa ya manjano. 

Zaidi yah apo imeongeza kuwa magonjwa mapya yanazuka hata katika maeneo ambayo awali hayakuwepo. Mwaka 2017 karibu asilimia 93 ya vifo vya malaria duniani vilitokea barani Afrika. 

Wakati makadirio ya joto yakitarajiwa kuongezeka kati ya nyuzi joto 1C hadi 4C barani humo , pato la taifa linatarajiwa kushuka kati ya asilimia 1.25 hadi asilimia 12.12. 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud