Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawasilisha sehena ya misaada kwa ajili ya watoto na wanawake walioathirika na mafuriko nchini Pakistan

Watoto waliohamishwa na mafuriko wakisubiri kuchota maji salama ya kunywa huko Balochistan, Pakistan.
© UNICEF/Azam
Watoto waliohamishwa na mafuriko wakisubiri kuchota maji salama ya kunywa huko Balochistan, Pakistan.

UNICEF yawasilisha sehena ya misaada kwa ajili ya watoto na wanawake walioathirika na mafuriko nchini Pakistan

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF hii leo limewasilisha tani 32 za dawa za kuokoa maisha na vifaa vingine vya dharura ili kusaidia watoto na wanawake walioathiriwa na mafuriko kote nchini Pakistan.

Taarifa iliyotolewa leo kutona nchini Pakistana na shirika hili imeeleza shehena hiyo iliwasili Karachi kutoka Kitengo cha Ugavi cha UNICEF kilichoko Copenhagen nchini Denmark na kukabidhiwa kwa serikali ya Pakistan ambapo ulipokelewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Idadi ya Watu ya Mkoa wa Sindh.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Pakistan Abdullah Fadil ametaja sehena hiyo kuwa imepakia dawa, vifaa tiba, tembe za kusafisha maji, vifaa vya kujifungulia kwa usalama, virutubisho vya lishe na kwamba vitatumwa mara moja kwa watoto na familia zinazovihitaji zaidi katika baadhi ya wilaya 72 zilizoathirika zaidi.

"Mafuriko yamewaacha watoto na familia bila kupata mahitaji ya kimsingi ya maisha. Msaada huu ni muhimu na unaokoa maisha, lakini ni tone tu la kile kinachohitajika. Hatari ya mlipuko wa magonjwa yatokanayo na maji kama vile kipindupindu, kuhara, dengi na malaria, inazidi kuongezeka kila siku huku watu wakilazimika kunywa maji machafu na kujisaidia haja ndogo. Hatari ya mbu, kuumwa na nyoka, magonjwa ya ngozi na kupumua pia yanaongezeka. Tunahitaji usaidizi wa haraka ili kuwasaidia watoto kung’ang’ania kuishi.”

Fadil amesema shehena ya pili ya tani 34 za vifaa vya msaada wa kibinadamu inatarajiwa kuwasili Jumanne tarehe 06 Septemba, ikiwa imebeba dawa za kutibu magonjwa ya vimelea, vifaa vya kufufua na kufunga uzazi, virutubishi vidogo kwa akina mama wajawazito, vifaa vya elimu na vifaa vya kujiburudisho kwa ajili ya kusaidia watoto kukabiliana na kiwewe.

Kwa kutumia vifaa vya dharura vilivyowekwa tayari, UNICEF imetoa huduma za dharura na vifaa vya haraka vya thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 2 katika wiki zilizopita. Hizi ni pamoja na maji ya kunywa, vidonge vya kusafisha maji, vifaa vya usafi, dawa, chanjo, virutubisho vya lishe kwa watoto, wajawazito na wanaonyonyesha, na vyandarua.

Kama sehemu ya ombi la Umoja wa Mataifa la dola milioni 160 kusaidia kukabiliana na mafuriko ya kitaifa, UNICEF inaomba dola milioni 37 kufikia watoto na familia zinazohitaji msaada wa kuokoa maisha.

Pakistan imekumbwa na mvua kubwa za monsoon tangu katikati ya Juni, ambazo zimesababisha hasara kubwa, majeraha na uharibifu wa miundombinu.
© WFP/Haris Khalid
Pakistan imekumbwa na mvua kubwa za monsoon tangu katikati ya Juni, ambazo zimesababisha hasara kubwa, majeraha na uharibifu wa miundombinu.

WHO na tathmini ya magonjwa 

Hii leo pia shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO imetoa tathmini ya magonjwa na vifo vilivyotokana na mafuriko nchini Pakistan ambapo limeeleza zaidi ya watu 1290 walipoteza maisha na watu 12,500 kujeruhiwa. 

Zaidi ya vituo vya afya 1460 viliathirika, kati ya hivyo 432 vimeharibiwa kabisa na 1028 vimeharibika kiasi na pia upatikanaji wa vituo vya huduma za afya, wahudumu wa afya na dawa muhimu na vifaa tiba ni mdogo.

Milipuko ya magonjwa inayoendelea ya kuharisha, homa ya matumbo, surua, na polio iko katika hatari ya kuongezeka zaidi.

Kuongezeka kwa maambukizi ya malaria bado ni tishio na wagonjwa wengi tayari wameripotiwa katika kliniki katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.

Uchunguzi wa awali wa magonjwa unaonesha kuwa makumi ya maelfu ya watu wametambuliwa kuwa wagonjwa walioathiriwa na kuhara, malaria, magonjwa ya kupumua, magonjwa ya ngozi na macho, typhoid na wengineyo.

Familia zinanusurika na mafuriko sasa hazina makao baada ya kuhamia eneo salama huku maji ya mafuriko yakikumba vijiji vya mkoa wa Balochistan nchini Pakistan.
© UNICEF/A. Sami Malik
Familia zinanusurika na mafuriko sasa hazina makao baada ya kuhamia eneo salama huku maji ya mafuriko yakikumba vijiji vya mkoa wa Balochistan nchini Pakistan.

Kuhusu Mafuriko Pakistan 

Mvua kubwa za masika zimeacha theluthi moja ya nchi hiyo ikiwa chini ya maji, na kuathiri zaidi ya watu milioni 33. Nusu ya watu hao ni watoto ambao ni angalau milioni 3.4 na watu milioni 6.4 wanahitaji msaada wa kibinadamu.  

Takriban watu 634,000 waliyakimbia makazi yao wanaoishi katika kambi.

Shughuli za kutoa misaada na uokoaji bado ni ngumu sana kutekeleza kwani barabara nyingi zimeharikibwa vibaya na maji ya mafuriko. Angalau kilomita 5,000 (maili 3,200) za barabara na karibu madaraja 160 yameharibiwa au kuvunjika.

TAGS: UNICEF, WHO, Pakistan, Mafuriko, Mabadiliko ya tabianchi, mvua za monsoon